Thursday, January 9, 2014

DEKULA KAHANGA 'Vumbi'


DEKULA  KAHANGA “VUMBI”

Mafanikio katika maisha ni lazima mtu kuwa na malengo, nia na dhamira ya dhati, kujiamini  na hatimaye kufanya maamuzi magumu. Maneno haya yametamkwa na mwanamuziki wa dansi Dekula Kahanga maarufu kwa jina la ‘vumbi’ambaye safari yake ya kwenda kupiga muziki huko Ulaya ilitokea katika bendi ya Maqius Original ya  hapa Tanzania.

Moja kati ya maamuzi magumu aliyoyafanywa mwanamuziki huyo lile la kondoka bendi hiyo iliyompa chati iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Lang’ata Kinondoni jijini Dar es Salaam na kutokomea hadi  Sweden bila kujua atakuwa mgeni wa nani huko ugenini.

Anaeleza kwamba hivi sasa hajutii maamuzi yake kwa vile tayari amepata mafanikio makubwa akiwa ni pamoja na kumiliki bendi yake iitwayo Dekula Band. Bendi hiyo hupiga  muziki kwa mkataba mara mbili kwa mwezi katika ukumbi wa Lala Vin, mjini Stockholm nchini Sweden.

Bendi hiyo ina  wanamuziki mahiri  wenye vipaji vingi toka nchi mbalimbali hapa duniani wakiwemo akina Luhembwe Mwanahita ‘Bobo Sukari’ (kuimba na Show), Sammy  Kasule (Injinia, kuimba, Bass,Drums na Keyboard), Joe Gerald Nnaddibanga(kuimba, Conga na Show),Christina Frank, na Marceline Kouakoua.

Wengine ni yeye Dekula Kahanga(Solo na rhythm), Arne Winald (Keyboard) kwa pamoja huufanya muziki wao kukubalika kimataifa hadi kupelekea kupata mialiko lukuki ndani na nje ya nchi ya Sweren zikiwemo za Ulaya, Asia, Marekani, Japan,  Falme za kiarabu na Afrika.

Anaelezea mafanikio mengine ni kutengeneza mahusiano mema kwa baadhi ya watu toka nchi mbalimbali wanazotembelea na sasa anaweza kuongea  kwa ufasaha lugha tano tofauti za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Lingala na Kiswidish.

Dekula Kahanga ni  alizaliwa Aprili 02, 1962 katika kijiji cha Lumera, Wilaya ya Kivu  Kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ni baba wa familia akiwa na mke na watoto watatu na yeye ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kadhaa wa mzee Aloyce Obeid Dekula aliyekuwa mfanyakazi wa Shirika la reli katika serikali iliyokuwa ikiongozwa na rais Mobutu Seseseko Kuku Ng’endu wa Zabanga.


Alipata elimu Sekondari hadi kidato cha nne karika miji Bukavu na  Uvira.
na kumaliza elimu hiyo mwaka 1979.
Mwaka uliofuatia wa 1980 safari yake katika muziki ilianza kwa kujiunga na bendi za Bavy National, na Grand Mike jazz, ambako alikutana na wanamuziki akina Kyanga Songa na Issa Nundu.

Akiwa Kivu, ‘Vumbi’ alikuwa msikilizaji mzuri wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo ilikuwa ikisikika vyema wakati huo na alizitamani nyimbo zilizokuwa zikiporomoshwa na bendi za Morogoro Jazz, Tabora Jazz, Cubzn Marimba, JUWATA Jazz, Mlimani Park na Orchestra Safari Sound.

Anamtaja John Luanda aliyekuwa akimiliki bendi ya Chamwino Jazz kuwa ndiye chanzo cha yeye kuingia hapa Tanzania baada ya kuwachukua toka Kongo yeye na wenzake akina Bwami Fanfan, Sisco Lunanga na Baposta ili  kujiunga katika bendi yake iliyokuwa ikipiga muziki Manzese maeneo ya Tandale jijini Dar es Salaam.

‘Mewenye bahati habahatishi’ ndivyo anavyosema mkung’utaji huyu wa gita la Solo Dekula Kahanga ‘Vumbi’ kwamba mwaka 1980 alikutana na mwanamuziki  Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Viking’ katika Ofisi za Ubalozi wa Kongo hapa nchini.

 Nguza Viking  wakati huo alikuwa mpiga gita la Solo pia akiwa mmoja kati ya  wanahisa na viongozi wa bendi ya Orchestra Maquis du Zaire, hapo alimpa mwaliko yeye na wenzake kwenda kuburudisha kwenye ukumbi wa White House uliokuwa maeneo ya Ubungo Kibo jijini Dar es Salaam.

Dekula alikubali mwaliko huo kisha weekend moja walifika na kupewa nafasi ya kuburudisha kwa muda mfupi ambapo waliutumia vyema na kuweza kuzikonga nyoyo za wanamuziki wa bendi hiyo ya Maquis  na wapenzi wa muziki waliokuwa mamefurika wakishuhudia vijana hao.

Baada ya kuburudisha usiku huo hazikupita  siku nyingi Dekula akaitwa na uongozi wa bendi ya Maquis du Zaire akina Chibangu Katai (mzee Paul), Mutombo Lufungula (Audax) na Mbuya Makonga (Adios) wakimtaka aandike barua ya kuomba ajiunge na bendi yao kwa mkataba wa kazi isiyo na mshahara ili kuziba nafasi ya Nguza Vicking ambaye tayari alikuwa ameanza mgomo baridi.
Naye aliona kama ngekewa imemshukia kwa kuitwa katika bendi kubwa ya Maquis du Zaire. Hakufanya ajizi alikubali kaunndika barua na akajiunga na bendi hiyo.

Vumbi anakumbuka siku mmoja wakipiga muziki ukumbi wa Temeke Stereo, alimuona kwa mbali Nguza Vicking akiwa kajibanza pembeni mwa ukuta ukumbini humo akisikiliza nyuzi alivyokuwa akizicharaza.

Baada ya kumuona anasema aliingiwa na tashwishwi isiyo mfano na kujiona kama anamvunjia heshima Nguza na kuomba ampishe ili aje kushika nafasi yake. Lakini viongozi wake akiwemo Chibangu Katai (mzee Paul) na  Ilunga Lubaba, walimtaka aendelee kupiga gita hilo.

Dekula Kahanga anasema alimudu akizipiga nyimbo zote alizokuwa zikipigwa na Nguza zikiwemo za Makumbele, Ngalula, Seya, Malokelee, Karubandika, Dora mtoto wa Dodoma, Nimepigwa Ngwala na nyingine nyingi kiasi kwamba wapenzi wa muziki walishindwa kutofautisha upigaji wa gitaa la Solo kati yake na Nguza katika mitindo yao ya Bishe bishe, Kamanyola, Ogelea piga mbizi na Zembwela.

Aliendelea kulivurumisha gita hadi  mwisho wa onyesho na baada ya hapo kwa adabu zote alikwenda kumsalimia na Nguza pale alipokuwa kajibanza, naye hakusita kumsifia kwa kazi  nzuri.

Taharuki kati ya uongozi wa  Maquis du Zaire  na Nguza ziliendelea  kupamba moto hatimaye aliondoka rasmi bendi hiyo na akaanzisha bendi yake ya Orchestra Sambulumaa akiwa na wanamuziki wengine akiwemo mwanaye Papii Kocha.

Bendi hiyo  haikudumu kwa kipindi kirefu kufuatia matatizo yaliyomikumba familia yake akiwemo yeye na watoto wake wote wa kiume kwa kufunguliwa kesi ya ubakaji wa wanafunzi wa shule ya msingi maeneo ya Sinza jijini
Dar es Salaam.

Kesi hiyo ilichukua muda mrefu kusikilizwa hatimaye mahakama Kuu  aliwatia hatiani yeye  Nguza na mwanaye Papi Kocha na kuhukumiwa kutumikia kifungo  cha maisha gerezani.

Miaka ya 1989 na 1990 Dekula alikuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa Maquis Original. Maquis Original lilikuwa jina jipya lililo badilishwa toka Maquis du Zaire baada ya kuhamia katika ukumbi Lang’ata, Kinondoni.

Dekula alivutia wapenzi wake kwa upigaji wa gita  hasa pale wimbo wa Ngalula ulipokuwa ukipigwa huku  mwimbaji Tshimanga Kalala Assosa akimpandisha mori, akipaza sauti kwa kumuita Vumbiii,Vumbiii,Vumbiii kila mara kama kibwagizo cha  wimbo huo.

Vumbi anawakumbuka baadhi wanamuziki aliokuwanao katika bendi ya  Maquis du Zaire na Maquis Original kwa wakati huo  wakiwemo waimbaji akina Mbuya Makonga ‘Adios’ Mutombo Lufungula ‘Audax’ Mukubule Lulembo ‘Parashi’, Kiniki Kieto, Tshimanga Kalala Assosa, Issa Nundu, Kasalo Kyanga.

Wapiga gita la Solo walikuwemo akina Chimbwiza Nguza Mbangu”Nguza Vicking”, Ilunga Lubaba na Suleiman Mbwana ‘Cocks’.

 Anawataja wapigaji wa gita la  kati  walikuwepo akina Mulenga Kalonji ‘Vata’ Omari Makuka  na Steven Kaingilila Mauffi. Gita zito la besi lilikuwa likiungurumishwa na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’ na Mujjos wa Bayeke.

Wapuliza midomo ya Bata walikuwa Mafumu Billar  ‘Bombenga’ Majengo Bakari, Mukuna Roy ‘ Mukuna wa Mukuna’, Akulyake Suleiman ‘King Maluu’, Alex Kanyimbo na Khatibu Iteitei.

Wengine anawataja Kanku  Kelly Ilunga Bizoo, Mpoyo Kalenga, Kaumba Kalemba na Ngenda Kalonga kwa upande wa Trampet na Drums walikuwepo Mbuya Makonga ‘Adios’ na Matei Joseph.


 Pia hakumsahau Kiongozi  wa wacheza shoo, Nkulu Wabangoi na wapiga Tumba akina Siddy Morris na Pulukulu Wabandoki Motoo ambao wote kwa pamoja waliifanya Maquis kuwa tishio kwa bendi zingine hapa nchini.

Dekula anaeleza kwamba alipofika Stockholm alianza kuchacharika mitaani  akitafuta bendi ya kupiga. Kwa bahati nzuri mwaka 1993  akakutana na mwanamuzi toka Uganda aitwaye  Sammy Kasule nao kwa pamoja wakaamua kuanzisha bendi yao ikiitwa  Makonde Group.

Mapema mwaka 1999, Dekula Kahanga alifyatua Album iitwayo Bolingo Ekesemi iliyosheheni nyimbo za ‘Dunia kuna mambo’ na ‘Mpenzi Asha’

Dekula anajivunia kuwa mwanamuziki wa kwanza mwaafrika huko Sweden baada ya kufyatua Album  iitwayo DEKULA Sultan Qaboos, yenye nyimbo za Sultan Qaboos, Mon Amour, Babylon, Mayanga, Rozina, Mambo leo na Nostalgie  nyimbo ambazo hupigwa  katika vituo vingi vya redio duniani.

Usemi wa ‘Mtaka cha Uvunguni sharti ainame’ ulimpata Dekula pale alipotaka kupata  unafuu wa maisha nchini Sweden ambao ni lazima uwe raia wa nchi hiyo. Hivyo alilazimika kuomba uraia kwa kufuata taratibu zote.

Dekula alitoa mfano wa Shubiri kwamba ni chungu lakini ni dawa, hivyo alifikia  maamuzi mengine magumu zaidi ya kuukana uraia wa nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC).

Hivi sasa yeye na wanamuziki wenzake wa bendi hiyo ni  raia halali wa nchi ya Sweden na wanaweza kusafiri kwenda nchi nyingi za Marekani Ulaya Asia na kwingineko pasipo kubughuziwa kwa kuomba VISA.

Mwanamuziki huyo ambaye kwa tabia ni mpole japo ni mcheshi, ametoa mwito kwa Vijana chipukizi  katika muziki kujifunza kupiga Ala ili wafikie viwango vya kuwa  wanamuziki na kuwaasa kaachana na anasa za dunia sisizo na maslahi kwao.

Vilevile amewaonya  kuondokana na ulevi wa  sifa toka kwa washabiki ambazo huwavimbisha vichwa na kusababisha kijisahau majukumu yaliyo mbele yao.

Dekula kwa kuona vijana wa kizazi hiki hawana munkari wa kujifunza kupiga Ala za muziki, ametoa ahadi kwamba atajitahidi  kwa kadri ya uwezo wake siku za usoni kuanzisha bendi hapa nchini itakayokuwa ikitumia Ala za muziki za kisasa ili vijana wa Tanzania wajifunze.

Mwisho.

No comments: