Monday, September 7, 2015

ABETI MASEKINI ‘ALIYEWATOA’ TSHALA MUANA NA MBILIA BEL



ABETI MASEKINI ‘ALIYEWATOA’ TSHALA MUANA NA MBILIA BEL

Jina la Abeti Masekini lilikuwa maarufu masikioni mwa wapenda muziki nchi za Afrika ya Mashariki na Kati mnamo miaka ya 1960. Alikuwa mwanamuziki aliyefanya juhudi za ziada ili 'kuwatoa' baadhi ya wanamziki wanaotamba hivi sasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Elisabeth Finant ndiyo majina yake kamili aliyezaliwa Novemba 09, 1954 katika mji wa Kisangani, Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mama huyo alitokea katia familia yenye ukwasi mkubwa yenye watoto wanane. Baba yake mzazi mzee Jean Fionant, alikuwa Chotara wa mchanganyioko wa Ukongomani na Ubelgiji.
Mwaka 1961 Masekini alipatwa na pigo baada ya Baba yake kauawa kikatili mjini Mbujimayi kutokana matatizo ya Kisiasa.
Mzee Finant alikua mwanachama wa cha MLC, kilichokuwa kikiongozwa na hayati Emery Patrice Lumumba.
Lumumba alikuwa Waziri Mkuu wa zamani nchini DRC Kongo ambae pia anaelezwa kuwa ndie Shujaa wa Uhuru wa nchi hiyo.

Kufuatia hali hiyo ikampelekea mama yake Abeti Masekini kuchukua uamuzi wa kuhamia katika jiji la Kinshasa, ili apate kujihifadhi akiwa na wanawe.

Walipofika Kinshasa, mama yake alimchukua Abeti Msekini akarejesha darasani kwenye shule iliyokuwa ikijulikana kwa Jina la ‘Lycee Ycee Sacre Ceur, Kwa sasa inaitwa  ‘Bosongani’.

Baada ya kumaliza shule ya sekondari, Masekini akaajiriwa kama Katibu kwenye Ofisi ya Waziri wa Utamaduni.

Aliwashangaza baadhi ya ndugu zake na Familia kuona  Abeti  Masekini alipoamua kujiuzuru kwenye kazi aliokua nayo. Akaelekeza mawazo yake kwenye  fani ya muziki, ndipo wakati akajipachika jina la ‘Betty’.
Mwaka 1971 chini ya usimamizi wa mwanamuziki  ‘Gerard Madiata’, palitokea mashindano ya kumtafuta mwanamuziki chipukizi. ‘Betty’akaamua kushiriki kwenye mashindano hayo, ambayo kwa bahati mbaya hajafaulu.
Changamoto ya kupenda muziki ndipo ilipoongezeka huku akiwa mdogo akichipukia mwenye umri wa miak 17 wakati huo.
Ili apate kuruhusiwa kudumbwiza katika unenguaji kwa jina lake  mwenyewe, ilibidi ajiongezee miaka mitatu zaidi,  akawa anasema yeye ni mkubwa wa miaka 20.
Abeti akisaidiwa na kaka yake ‘Jean Abumba’ ambae alikuwa mpiga gitaa mashuhuri, akawa kila siku anafanya onesho kwenye vilabu vidogodogo Jijini Kinshansa.

Abeti Masekini alikutana na Gerard Akueson, aliyekuwa raia wa nchi ya  Togo katika jiji la Kinshasa mwaka 1971. Hapo ndipo fani yake ya muziki ilipoanza rasmi.
Gerard Akueson ndiye akawa meneja wake mkuu tangia mwaka 1972. Abeti na Akueson wakaanzisha mahusiano ya kimapenzi na ilipotimu mwaka1989, wakakufunga ndoa jijini Paris nchini Ufaransa.

Walibahatika kupata watoto wanne, wa kike 3 na mvulana mmoja.

Mumewa huyo alimshauri waongozane kwa kuhamia kwenye nchi za Afrika ya Magharibi, ambako walitumaini kupata mafaanikio zaidi.

Wikiwa hukowalijikuta akiwa na Mashabiki wengi sana kwenye nchi za Benin, Conte D’ivoire, Togo, Niger, Nigeria, Guinea na Ghana.

Baada ya miaka kadhaa akiwa kwenye nchi hizo, Abeti Masikini aliaamua kurudi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Aliporejea mapokezi hayakuwa mazuri kwa kuwa watu wengi walikua hawamfahamu kabisa.

Kilicho mponza zaidi ni kwa kipindi chote hicho, alikua hajaweka hata na album japo moja sokoni.
Licha ya kutofahamika kwake, aliamua kufanya onesho kubwa katikati ya jiji la Kinshasa kwenye ukumbi wa CINE Palldium ambako aliambulia watu 12 pekee ndio walio jitokeza kumuangalia.
Tukio hilo halikumdhoofisha moyo Abeti, aliendelea kufanya kazi kwa bidii ili malengo yake yakamilike.

Baada ya kufanya mazoezi makubwa ya kuboresha sauti yake, mwaka 1973 alitoka na album yake ya kwanza ‘Pierre Cardin’ ikiwa na nyimbo kadhaa zikiwemo Mutoto wangu, Bibile, Aziza, Miwela na Safariet Papy yaka.

Album hiyo haikupokelewa vilivyo na wakazi wa jiji la Kinsahasa. Machoni mwao walimchukulia Abeti kama mgeni.

Walimlaumu kwa tabia yake ya kupenda kuimba baadhi ya nyimbo zake kwa lugha ya Kiswahili.
Nguli huyo Abeti Masekini akapatwa na wazo la kuunda kundi lake akalipa jina la ‘Les Redoutables’.

Kundi hilo lilikuwa na wanenguaji wake machachari walio julikana kama ‘Les Tigresses’, ambalo lilifanya watu wengi waanze kuvutiwa naye.

Maonesho yake katika jiji la Kinshasa yakawa gumzo mitaani. Kazi lizokuwa akizifanya meneja wake, zikazaa matunda mema.

Alifanikiwa kupata mkataba uliompeleka kwenda kufanya onesho katika ukumbimaarufu wa Olympia uliopo katika jiji la Paris, ncini Ufaransa.

Mwaka1973 akiwa njiani kuelekea Paris kwenye onesho hilo, alitua katika jiji la Dalkar nchini Senegal. Huko alifanya onesho ambalo pia rais wa nchi hiyo wakati huo Leopald Seadar Senghor alihudhuria.

Pesa zilizopatikana katika onesho hilo alizotoa kama msaada wake kwa watu walioathiriwa kwa ukame wa ardhi.

Alipotuwa katika jiji la Paris Februari 02, 1973 aliporomosha onesho kabambe lilowavutia hasa mashabiki wakizungu kwenye ukumbi wa Olympia.

Abeti Maseki alifanikiwa kufanya onesho jingine Juni 06, 1974  kwenye ukumbi wa Carnegie, uliopo katika jiji ma New York nchini Marekani.

Umaarufu wake ulizidi kuja juu zaidi hususani pale alipopewa fursa ya kutumbuiza kwa pamoja katika jukwaa moja na nguli wa muziki duniani.

Jukwaa hilo lilipambwa na wanamuziki akina James Brown, Miriam Makeba, Tabu Ley na Franco Luambo Makiadi, kabla ya pambano la masumbwi la kihistoria kati ya Mohammed Alli ‘Clay’ na George Foreman jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Albam yake ya pili alifyatua mwaka 1975 ikiwa na jina la ‘La Voix Du Zaire’.

Nyimbo zilizokuwa zimesheheni katika albam hiyo ni Likayabo,Yamba yamba, Kiliki, Bamba, Nalikupenda na Ngoyaye.

Mwaka huo huo Abeti alipokea mualiko kutoka kwa  ‘Bruno Coquatrix’  ambae ndie aliyekuwa mmiliki wa ukumbi wa Olympia ya jijini Paris.

Akaenda kwa mara nyingine tena kufanya maonesho kwa Siku mbili mfululizo.

Ndipo hapo akapachikwa jina bandia la ‘Tiger mwenye kucha za dhahabu’
Mwaka uliofuatia wa 1976, ulikuwa mbaya ki maslahi kwa Abeti Masekini.

Alimpata mpinzani wa uhakika katika muziki aliyejulikana kwa majina ya Mpongo Love, aliyekuja juu kuliko yeye.

Mpongo akaongoza Hit Parade kwenye radio ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( Zaire) wakati huo.

Wimbo wake ‘Pas Possible’ ulimafanya kuwa ni mwenye kupendwa mno na mashabiki.

Pamoja na yote mwaka 1977 wanamuziki hao Abeti na Mpongo, walifanya kitu ambacho hakikutarajiwa na wengi.

Walifanya onesho kubwa la pamoja kwenye ukumbi wa ‘Cine Palldium’ katika jiji la Kinshasa na kuacha simulizi kubwa.

Kila mmoja wao kaimba kiaina yake, wakaweka  misingi mizuri ya kupendana kwa wanamuziki wa kike wa kizazi kijacho.

Historia ya Abeti Masekini itaendelea kukumbukwa daima kwa kuwa yeye ni darasa tosha,
Wanamuziki wengi maarufu wamepitia kwenye bendi yae wakiwamo  akina Mbilia Bel, aliyenengua toka 1976  hadi1981, Lokua Kanza aliyekuwa mpiga gitaa mwaka 1980- hadi 1981, Abby Surya aliyekuwa mnenguaji mwaka 1984 hadi 1986 na  Malage De Lugendo aliyekuwa mwimbaji.
Wengine walikuwa wanenguaji Joëlle Esso, Tshala Muana mwaka 1978 hadi 1979, Yondo Sister mwaka 1986 na Lambio Lambio ‘Komba Bellow’ kwan upande wa kinanda.
Abeti Masekini ni mmoja kati ya wanamuziki wa kike barani Afrika waliofanikiwa kujiwekea jina Kimataifa.
Alidhihirisha uwezo wa kipaji chake na kufahamika nchini mwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,  ambayo muziki umetawalia na  Wanaume.
Abeti pia alikuwa mstari wa mbele kupigania haki ya Wanawake.
Kwa miujiza ya mungu, Abeti alifariki dunia Septemba 09, 1994 akiwa katika jiji la Paris nchini Ufaransa.Tarehe hiyo inafanana na ile aliyozaliwa ya Novemba 09, 1954.

Ni mwaka wa 21 tangu atutoke mwana muziki huyo, mungu ailaze pahala pema peponi, Amina.

Mwisho.



No comments: