Thursday, October 8, 2015

UNAMKUMBUKA FRANKLIN BOUKAKA?



UNAMKUMBUKA FRANKLIN BOUKAKA?


Ule usemi usemao kuwa “Maji hufuata mkondo” unajionesha wazi kwa mwanamuziki Frankin Boukaka aliyerithi  mikoba ya baba yake.

Alikuwa ni mtoto wa Aubin Boukaka aliyekuwa mwanamuziki wa kundi la ‘The Gaiety’ wakati mkewe Yvonne Ntsatouabaka alikuwa  mshereheshaji (MC) maarufu  kwenye misiba na pia alikuwa mwanamuziki muimbaji.

Mara baada ya kuzaliwa Oktoba 10, 1940, alipewa jina la François Boukaka baadae akajulikana kama Franklin.

Alikuwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanane wavulana watatu na wasichana watano.

Franklin Boukaka alijongezea umaarufu zaidi nchini mwake pale alipojiunga na wenzie waliotaka kuipindua serikali ya Kongo Brazzaville wakati huo ikiwa chini ya uongozi wa rais Marien Ngouabi.

Elimu yake alipata katika shule mbalimbali nchini kwake Kongo Brazzaville. Franklin  alianza kujishighulisha na mambo ya muziki 1955 katika kundi lililojiita Sexy Jazz.

Kundi hilo lilikuwa likiongozwa na Miguel Samba, baadae akaanzisha kundi la Negro Band.

Hatimae katika safari yake ya muziki akaungana na wakali wengine kama  Edo Clary Lutula, Jeannot Bombenga, Tabu Ley ,Mutshipile "Casino", André Kambite " Damoiseau ",  Papa Bouanga, Charles Kibongue katika lile kundi maarufu la African Jazz, sauti ya Franklin imo katika nyimbo kama  Mwana mawa , Catalina cha cha na Marie José zilizotungwa na Tabu Ley.

Mwaka 1959 kundi la African Jazz lilimeguka baada ya wanamuziki wengine walipohamia katika jiji la Brussels nchini Ubelgiji wakifuatana na wanasiasa wa Kongo kwenye mazungumzo ya awali ya uhuru wa Kongo.

Wanamuziki waliobaki akiwemo Jeannot Bombenga,  ila Tabu Ley wakajiunga na kuanzisha kundi jingine lililotingisha nchi lililoitwa Vox Africa.

Waimbaji wakati huo wakiwa ni akina Franklin Boukaka na Jeannot Bombenga.

Baada ya hapo Franklin akaaliacha kundi hilo na kurudi kwao Brazzaville ambako  mwaka 1962, akawa mmoja wa wanamuziki wa bendi ya Cercul Jazz. 

Bendi hiyo ilianza miaka ya 1950, ikiwa chini ya Chama cha vijana kilichokuwa kikipata ufadhili wa serikali ya Ufaransa. 

Chama hicho kiliitwa Cercule Culturel de Bacongo. 
Hatimae Boukaka alikuja kuwa kiongozi wa chama hicho na kikawa na umaarufu wa mkubwa. Wimbo wa bendi hiyo ‘Pont Sur le Congo’ (Daraja juu ya Mto Congo), ulikuwa una hamasisha kuunganika kwa Kongo Leopoldville (Kinshasa) na  Kongo Brazzaville baada ya nchi hizo kupata uhuru.

Kufikia hatua hiyo wimbo huo ukapata umaarufu kuliko nyimbo zote za bendi hiyo.

Baadae Franklin akiwa na gitaa lake kavu akaanzisha kikundi ambacho kilikuwa na wapiga marimba wawili akaweza kufanya ziara kadhaa hata nje ya nchi yake na kundi hilo.

Mwaka 1970 Boukaka  aliweza kurekodi nyimbo 12 zilizopangwa vyombo na Manu Dibango. Nyimbo za Nakoki na Le Bucheron ndipo zilipopatikana. 

Baada ya hapo Franklin alijiunga na wenziwe waliotaka kuipindua serikali ya Kongo Brazzaville, wakati huo ikiwa chini ya uongozi wa rais Marien Ngouabi.

Jaribio hilo lililofanyika tarehe 22 February 1972 lilishindwa na siku chache baadae kifo cha Boukaka kilitangazwa.

Mungu ailaze roho yake pahala pema pepeni, Amina.

Mwisho.

No comments: