Monday, June 20, 2016

ALLI JAMWAKA ALIYEIKANYAGA ARDHI YA MAREKANI WA KUPIGA TUMBA



ALLI JAMWAKA ALIYEIKANYAGA ARDHI YA MAREKANI WA KUPIGA TUMBA

Miaka ya 1980 hadi 1990 walikuwepo wadunda tumba wengi waliosifika katika bendi za muziki hapa nchini.
Katika bendi ya Maquis du Zaire alikuwepo Pulukulu Wabandoki Motto, aliyekuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi na mashabiki wa bendi hiyo. Halikadhalika bendi ya MK Group alikuwa mpiga tumba maarufu Sidy Morris ambaye wakati wa uhai wake alikuwa akionesha madoido ya wakati akilizidunda tumba kwenye ukumbi uliokuwepo katika hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam hadi wakampachika jina bandia la ‘Tanzania One’,
Miaka ya 2000 alijitokeza mpiga tumba aliyekuwa katika bendi ya African Stars, MCD ambaye aliweza kuwachezesha wanenguaji akipiga tumba huku akipuliza filimbi.
Katika makala haya yanamzungumzia mpiga tumba Ally Omary Jamwaka, aliyejizoela sifa nyingi kwa uhodari wake wa kupiga tumba.
Wasifu wa Jamwaka unaeleza kuwa  alizaliwa katika kijiji cha Malui Machi 01, 1953. Alijiunga na shule ya msingi ya kijijini kwake kuanzia mwaka 1960 hadi alipomaliza elimu ya darasa la saba.
Mwaka 1969 akaingia katika jiji la Dar es Salaam akaanza kutafuta maisha. Alli Jamwaka alikuwa na ndoto za kuwa msanii. Hiyo yawezeka alivutiwa na jinsi kaka yake Shaaban Omary Jamwaka alikuwa mpiga drums ambaye aliyetangulia kufika katika jiji hilo.
Kaka yake huyo ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa kumtia hamasa ya kuwa msanii.
Jamwaka amekuwa kwenye talanta hiyo tangia miaka ya 1970 mara baada ya kujiunga na kikundi cha sanaa kilichokuwa na maskani maeneo ya Buguruni, jijini Dar es Salaam, kikiwa chini ya Mzee Mindu.
Akiwa na kikundi hicho ndipo alipokutana na rafiki yake aliyeitwa Adam Bakari, huyu baadae sana alikuja kupewa jina la ‘Sauti ya Zege’.
Kwa pamoja wakajadiliana jinsi ya kujikwamua kimaisha wakaamua kutengeneza kundi lao waliloliita The Hippies.
Kundi hilo lilikuwa ni la muziki wa vijana lililokuwa na kazi ya kwenda kwenye kwenye kumbi za madansi kunakopiga bendi kubwa, na kuomba 'ujiko' ili waoneshe makali yao.
Mtindo ulikuwa wa kawaida kwa vijana waliokuwa wakichipukia katika muziki, ulikuwa umeenea nchi nzima wakati huo. Bendi ndogo zilikuwa zikifuatilia zinakopiga bendi kubwa nao kuomba nafasi kidogo.
Walivyokuwa wakiruhusiwa kupiga nyimbo kadhaa walikuwa wakitumia vyombo  vya bendi kubwa. Mtindo huo uliwapa uzoefu vijana hao. Walionekana kuwani wazuri walipatiwa hata kupata ajira papo hapo.
Bendi ya The Hippies ilikuwa imeweka makao makuu yake mtaa wa Somali maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam. Walikuwa wakipiga muziki wa kukopi bendi za ndani na nje zilizotamba wakati huo, hasa zile za Ulaya na Marekani. Jamwaka wakati huo alikuwa tayari akipiga tumba na drums.
Miaka ya 1970 Mashirika ya Umma yalianzisha vikudi mbalimbali vya sanaa zikiwemo bendi. Alli Jamwaka  alijiunga mwaka 1971 katika bendi ya Biashara Jazz.
Biashara Jazz wakati huo ilikuwa bado mpya kabisa baada ya kubadili jina kutoka STC Jazz. Bendi hiyo ilikuwa chini ya mmiliki ya Board of Internal Trade (BIT) ambayo chini yake kulikuwa na mashirika ya umma kama RTC, DABCO, HOSCO, GEFCO na kadhalika.
Katika bendi hiyo aliwakuta akina wanamuziki wengine akina Raphael Sabuni, Belino, Muddy, na kaka yake Shaaban Omary Jamwaka ambaye alikuwa mpiga drum wa bendi hiyo wakati huo.
Ally Jamwaka alipiga muziki katika bendi  hiyo chini ya uongozi wa Juma Ubao ‘King Makusa’ hadi mwaka 1977 alipoamua kujiunga katika bendi ya Tanzania Stars.
Bendi hiyo ilikuwa na makao yake katika ukumbi maarufu miaka hiyo iliyoitwa Margot ambayo ilikuwa katikati ya Jiji pembeni mwa barabara ya Samora jijini humo.
Ukumbi huo ulikuwa maarufu mno kwakuwa muziki ulikuwa ukipigwa kila siku mpaka usiku wa manane.
Wateja wakubwa Margot walikuwa ni  mabaharia walikuwa wakisha tia nanga meli zao katika bandari ya Dar es Salaam, usiku walikuwa wakijazana Margot ambako kulikuwa ni mahala penye starehe za kila aina.
Kufika kwake bendi hiyo alipishana na wanamuziki maarufu ambao wote ni marehemu, Haruna Lwali mpiga tumba na Joseph Bartholomew Mulenga ‘King Spoiler’ aliyekuwa akipiga gitaa, waliohamia bendi ya Orchestra Santa Fe, iliyokuwa ikipiga muziki katika ukumbi jirani wa Gateways.
Baadhi ya wanamuziki waliokuweko katika bendi ya Tanzania Stars wakati huo walikuwa Joseph Emmanuel aliyekuwa akiimba na kupiga gitaa, Hussein Sadiki na Yahaya Bushiri. Bendi hiyo ilikuwa inapiga muziki ya kukopi kutoka nchi mbalimbali duniani, kuwaburudisha wateja wao  hasusani mabaharia kutoka kila kona ya dunia.
Wakati huo ilikuwa ukiingia katika ukumbi wa Margot ungeweza kusikia nyimbo za Kichina, Kihindi, Kigiriki na ngine toka mataifa mbalimbali duniani.

Baada ya ukumbi huo kuchukuliwa na Chama Cha Ushirika, bendi pia ikachukuliwa, na ndipo ilipozaliwa ile bendi maarufu ya Washirika Tanzania Stars. ‘Wantunjatanjata’
Alli Jamwaka alichukuliwa akajiunga  kupiga muziki katika bendi hiyo mpya ya Tanzania Stars mpaka mwaka 1979.
Uongozi wa bendi ya Orchestra Mlimani Park ulimfukuza kazi mpiga tumba wake aliyekuwa akiitwa Haruna Lwali, na hapo Abel Balthazar aliyekuwa mmoja kati ya viongozi wa bendi hiyo, alimfuata Jamwaka ili ajiunga katika bendi ya Orchestra Mlimani Park Orchestra.

Mlimani Park  ilikuwa chini ya Chama cha Usafirishaji na hasa wa Taxi (TTTS).
Bendi ya Orchestra Mlimani Park Bendi ilipewa huduma nzuri sana hadi  kufikia kuwa moja ya bendi kubwa nchini. Nyimbo zake za wakati ule bado zinaheshimika katika nyanja za muziki hata leo.
Ukumbi wa Msasani Beach Club ulikuwa mmoja wa mali za TTTS, na bendi ya Mlimani Park ndio iliyojenga ukumbi huo kwa kutumia mapato ya kila Jumatano kuelekezwa kwenye ujenzi wa ukumbi huo. Baada ya ukumbi huo kukamilika wanamuziki wakiwa na imani ambayo baadae ilikuja kuonekana potofu, waliamua kutumia fedha yao ya kila Jumatano kuanza kujenga ukumbi wa bendi yao uliokuwa Mpakani, maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam.
Lakini taharuki iliyojiri wakati huo, ujenzi ulifika mahala ukadorora na kufa kabisa.
Mwaka 1982 mali za TTTS kama vile bendi na ukumbi wa Mpakani ukahamishiwa Shirika la Maendelo la Jiji la Dar es Salaam (DDC).
Awali kulikuweko na wazo kuwa bendi hiyo ihamishwe kuwa chini ya Shirika la Ndege Tanzania (ATC) maana wakati huo Shirika hilo lilikuwa na klub yao moja nzuri.
 Lakini ikaonekana DDC walikuwa na kumbi nyingi zikiwemo za DDC Kariakoo, DDC Magomeni Kondoa na  DDC Keko. Ilielezwa kwamba bendi Mlimani Park Orchestra ingefanya kazi kwa ufanisi zaidi huko.
Kwa mantiki hiyo bendi pamoja na  wanamuziki wakauzwa kwa Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC).

Walipiga muziki katika bendi hiyo hadi mwaka 1985, ambapo awamu ya kwanza ya kundi kubwa la wanamuziki lilipoondoka DDC Mlimani Park Orchestra na kujiunga na kundi lililoanzishwa la International Safari Sound.
Bendi hiyo ikapewa majina ya Orchestra Safari Sound (OSS),
iliyokuwa na mtindo wa ‘Ndekule’.
Baadhi ya wanamuziki walikuweko ni pamoja na Abel Barthazar, Muhidin Maalim Gurumo, Ally Makunguru, Mustafa Jonh Ngosha, Kassim Rashid ‘Kizunga’ pamoja na mwimbaji mahiri Skassy Kasambula.
Katika awamu ya pili ya wimbi la wanamuziki wa Orchestra Mlimani Park walichomoka kwenda Orchestra Safari Sound, Ally Jamwaka pia alikuweko.
Wakati waimbaji mashuhuri akina Fresh Jumbe, Cosmas Chidumule, Hamis Juma ‘Maalimu Kinyasi’ na mcharangaji drums Chipembele Said ‘Bobchipe Chipembele’, wakasindikizana na Michael Bilali ambaye alirejeshwa Orchestra Mlimani Park kwa nguvu ya wapenzi na mashabiji wa bendi hiyo  waliochanga fedha na kulipa fedha alizokuwa kachukua toka uongozi wa Orchestra Safari Sound.
Alli Jamwaka amewahi kufanya ziara nyingi ndani nan je ya nchi. Ziara ambayo iliweka historia katika maisha yake ni ile alipopata fulsa miaka michache ya nyuma kwenda Marekani kupiga muziki akifuatana na wanamuziki wengine akiwemo Hassan Rehani Bichuka.
Mwisho.

No comments: