Monday, June 20, 2016

KASSIM MPODA ‘De la Chance’ ATIMIZA MIAKA 14 KABURINI



KASSIM MPODA ‘De la Chance’ ATIMIZA MIAKA 14 KABURINI

Wapenzi na mashabiki wa  muziki wa dansi hususani katika jiji la Dar es Salaam, jina la Kassim Mponda ‘De la Chance’  lilikuwa maarufu mnamo miaka ya 1980 na 1990, akipiga katika bendi za Juwata na Mlimani Park.
Mwanamuziki huyo alikuwa mpiga gitaa mashuhuri hapa nchini, Juni mwaka huu 2016, imetimia miaka 14 tangu alipofariki mwezi Juni 2002 akiwa katika jiji la Dar es Salaam.
Wakati wa uhai wake alijizolea sifa lukuki kwa kulicharaza gitaa la besi na solo kwa nyakati tofauti.
Alionesha makali yake hususani alipokuwa katika bendi ya Juwata. Gitaa lake hilo lilisikika kwenye wimbo wa Sogea Karibu.
Katika wimbo huo Waziri Alli alibofya kinanda kwa umahiri mkubwa sana.
Wasifu wa Mponda unaleleza kuwa alikuwa wa kabila Kindengereko aliyezaliwa mwaka 1945, barabara ya Mwanza mjini Tabora. Mwaka huo una historia kubwa duniani kote kwani ulikuwa mwaka ambao Vita vikuu vya pili vya dunia vilipomalizika.
Majina yake halisi alikuwa akiitwa Kassim Mponda Mbwana. Baba yake mzazi Mbwana Mponda aliyekuwa na asili ya Kabila la Kindegereko toka mkoa wa Pwani.  Mzee Mponda alifika Tabora na kuwa mfanyabiashara ndogondogo.
Kassim Mponda alipata elimu ya msingi katika shule ya Town, iliyopo mjini humo, baadaye alijiendeleza mwenyewe kujifunza lugha ya Kiingereza.
Alifunzwa kupiga gitaa la besi akiwa nyumbani kwa Hassani Athumani, aliyekuwa mwanamuziki katika bendi za Tabora Jazz, Kiko Kidds, Nyanyembe Jazz na Milambo ‘ Wana Sona sona’ kwa nyakati tofauti.
Hassan Athumani ambaye hivi sasa ni mjasiliamali akitengeneza Samani za ndani nyumbani kwake Barabara ya Mwanza mjini humo, aliunda kikundi kidogo cha vijana waliokuwa wanapenda kufundishwa muziki.
Kikundi hicho kilikuwa kikipiga muziki ‘mkavu’, vyombo vya muziki vilivyokuwa vikitumika ni magitaa makavu na ngoma.
Baadhi ya vijana walioshiriki kwenye kikundi hicho ni pamoja na yeye Hassani Athumani, aliyekuwa akilicharaza gitaa la solo, Kassim Mponda akiliungurumisha gita zito la besi na ngoma zilidundwa na Mavumbi Alli. Kwa upande wa waimbaji walikuwapo Hassani Athumani, Bozeni na Moshi Alli. 
Baadaye Mponda alikwenda kujiunga na bendi ya Kiko Kidds, iliyokuwa ikiongozwa na Salim Zahoro, mjini Tabora. Wakati huo huo mwalimu wake Hassani Athumani alikwenda kujiunga katika bendi ya Tabora Jazz.
Baada ya miezi takribani mitatu, Kassim Mponda aliicha bendi hiyo na kuchepukia katika bendi ya Tabora Jazz, akamfuata mwalimu wake Hassani Athumani.
Akiwa katika bendi hiyo, Mponda alionesha makali yake vilivyo kwa kuliungurumisha gitaa la besi wakati huo.
Kati ya mwaka 1968 na 1966, aliondoka katika bendi ya Tabora Jazz, akaenda katika jiji la Dar es Salaam ambako huko alijiunga katika bendi ya Western Jazz hadi mwaka 1967, aliporejea tena Tabora.
Alipofika mjini humo alimkuta Hassan Athumani akiwa mbioni kuanzisha bendi mpya ya Nyanyembe Jazz. Aliungana naye kuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi hiyo.
Akiwa na Nyanyembe Jazz, Mponda ndipo alianza kupiga gitaa la solo hadi Juni 1967, alipoondoka kwenda Dodoma kujiunga katika bendi ya Central.
Alikuwa na sifa kubwa ya utafutaji maendeleo latika muziki hivyo baada ya miezi miwili alikwenda Dar es Salaam kujiunga katika bendi ya Polisi Jazz. ‘Wana Vangavanga’.
Akiwa katika bendi ya Polisi Jazz alikokutana na aliyekuwa kiongozi wa bendi hiyo Kassim Mapili. Licha ya kuwa kiongzi Mapili pia alikuwa ni mtunzi, mwimbaji na uwezo mkubwa wa kupiga gitaa.
Hukaa sana katika bendi hiyo baada ya kipindi kifupi Mponda aliondoka akaenda kujiunga katika bendi ya Vijana Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Hemed Maneti wakati huo.
Hata huko Viajana Jazz nako hakutumikia kwa kipindi kirefu kwani alitimka kwenda kujiunga katika bendi ya Safari Trippers, ambako katika wimbo wa Salama alikung’uta gitaa ‘kinoma’ likisindikiza sauti nyororo ya Marijani Rajabu wakati huo.
Baadaye akawa mmoja kati ya wanamuziki waloihama Safari Trippers, wakaenda kuanzisha bendi ya Dar International.
Bendi ya Juwata ‘Wana Msondo ngoma’ ilimyakuwa Kassim Mponda kuongeza nguvu katika bendi yao.
Wakati huo bendi ya Juwata ilikuwa ikipiga kwenye ukumbi za Kigongo Bar, maeneo ya Buguruni na Argentina maeneo ya Manzese jijini Dar es Salaam.
Mnamo miaka ya 1980 Kassim Mponda alijiunga katika bendi ya Orchestra Mlimani Park akitokea Msondo ngoma na baadaye alichukuliwa kwenda kupiga muziki katika bendi ya African Sound Orchestra (Afriso Ngoma).
Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na mtunzi na mwimbaji mahiri toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lovy Longomba.
Longamba aliwahi kukiri umahiri wa Kassim Mponda tangu akiwa katika jiji la Nairobi miaka ya 1980, alimuelezea kuwa ni mmoja wa wapiga solo wa Kitanzania anaowaheshimu sana pamoja na kwamba alikuwa hajawahi kukutana nae.
Sifa hizo ndizo ilielezwa kuwa yawezekana ndio zilimfanya Lovi amchukue kujiunga katika bendi ya Afriso.
Wakati huo Lovi Longomba alikuwa ni ,wanamuziki katika bendi ya Super Mazembe, iliyokuwa na makazi yake katika  jiji la Nairobi nchini Kenya.

Kwa upande wake Mponda hakuwa akitarajia sifa kubwa toka mwimbaji na mtunzi katika bendi ya Super Mazembe.
Akisimulia wasifu wa Mponda, Hassani Athuani alisema kuwa kuondoka kwa Mponda katika bendi ya Juwata, kulipelekea bendi hiyo kumchukua mwanamuziki chipukizi Abdu Ridhiwani Pangamawe kujaza nafasi yake.
Pangamawe aliingia katika bendi hiyo akiwa na vipaji vingi kikiwemo cha kulicharaza gitaa la solo na kubofya kinanda. Ikumbukwe kwamba hata wakati mbofya kinanda wa bendi hiyo Waziri Alli ‘Kissinger’ alipoondoka kwenda katika bendi ya Kilimanjaro ‘Wana Njenje’, Ridhiwani aliziba nafasi yake pasipo shaka.
Mponda aliyepachikwa jina la bandia la ‘De la Chance’, likiwa na maana ya ‘mtu mwenye bahati’.
Ndiye aliyepiga gitaa solo katika nyimbo nyingi ukiwemo wa wa Kiu ya Jibu, Ashibai, Sogea Karibu na vingine vingi akiwa na bendi ya Mlimani Park Orchestra.
Nyota ya Mponda ilianza kufifia baada ya kuondoka katika bendi ya Juwata hata alipokwenda kujiunga na bendi za  Mlimani Park, Bima Lee na hatimaye Afriso Ngoma.
Aidha gitaa lake linasikika vizuri katika wimbo wa ‘Dawa ya Pendo ni Pendo’ uliofyatuliwa na bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra.
Mponda alikuwa ni miongoni mwa wanamuziki waliochukuliwa na Shirika la Bima la Taifa kwenda kuongeza nguvu katika bendi ya Shirika hilo ya Bima Lee Orchestra. Bima Lee ilikuwa ikitumia mtindo wa ‘Magneto tingisha’
Baadhi ya wanamuziki alioungana nao wakati huo walikuwa ni Jerry Nashon ‘Dudumizi’, Shabani Dede, Joseph Bartholomew Mulenga ‘King Spoiler’, Maximilian Bushoke na wengine.
Katika wimbo wa ‘Busu pande tatu’ ulioghaniwa kwa umahiri mkubwa na Jerry Nashon, Mponda aliyelikung’uta gitaa la rhythm linalosikika, likitanguliwa na solo la Joseph Mulenga.
Aidha kwa kipindi kifupi aliwahi kupiga muziki katika bendi ya Shikamoo Jazz inayoongozwa na Salim Zahoro katika jiji la Dar es Salaam.
Sifa nyingine za Mponda aliyokuwa nayo ambayo wanamuziki wengine wameikosa ni utanashati wake. Alikuwa akionekana maridadi muda na popote utakapokutana naye.
‘De la Chance’ alikuwa akipendelea kuvaa kofia ya aina ya ‘Kapelo’, wakati akishika ‘mpini’ alikuwa akifuata miserebuko ya mashabaki utadhani anawaona rohoni.
Faida ya kuwa na mtoto mwenye hekima aliionja pale mwanae mmoja alipoamua kumnunulia vyombo va muziki vilivyomuwezesha kuanzisha bendi yake ya Afriswezi.
Bendi hiyo iliwahi kufanya ziara mkoani Lindi ambako mara walipowasili mjini humo, Mponda alipatwa na matatizo ya kuziba mkojo yaliyopelekea kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Lindi wakati huo.
Juhudi za kumtibu ziliedelea hata kupelekwa Kisiwani Mafia, mkoani Pwani kwa matibabu zaidi. Hata hivyo ilishindikana akarejeshwa jijini Dar es Salaam, ambako aliendelea kupatiwa tiba japo hazikumsaidia hatimaye mwaka 2002, akafariki.

Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi, Amina.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba 0784331200 na 0767331200.

No comments: