Thursday, January 3, 2013

MKONGWE SHEM KARENGA

MTAMMBUE MKONGWE SHEM  IBRAHIM  KARENGA.

 Shem Ibrahim Karenga akiwa katika picha na mpigaji wa gita la rythm , wa Soukous Stars, Lokassa ya Mbongo(kushoto) walipokutana jijini Dar es Salaam. 


Na Moshy Kiyungi.

SHEM IBRAHIM KARENGA ni mmoja kati ya wanamuziki wachache wenye uwezo wa kucharaza gita huku akiimba kwa wakati mmoja. Shem alitamba sana miaka ya 1970  akiwa na bendi ya Tabora Jazz wana Segere Matata.

Alizaliwa mwaka 1950 eneo la Bangwe mkoani Kigoma na kupata elimu yake katika shule ya msingi Kihezya kati ya mwaka 1957 na 1964.

Alianza kujifunza muziki akiwa mwanafunzi katika shule ya wamissionari na huko ndiko fani hiyo ilianza kuchipua hatimaye mwaka huo huo wa 1964  akajiunga na bendi ya Lake Tanganyika Jazz iliyokuwa na maskani yake mjini Kigoma.
Alipoingia Lake Tanganyika Jazz alijifunza Ala za muziki za drums, Kinanda na gita la rhythm, Solo. Besi gita pamoja akiimba.

Alidumu  katika bendi hiyo kwa kipindi cha miaka minane na mwaka 1972 Shem Kalenga aliitwa katika bendi ya Tabora Jazz ambako aliingia kwa kishindo na nyimbo zake alizozitunga akiwa na Lake Jazz na kuanza kuzipiga katika bendi yake mpya.

Nyimbo hizo zilikuwa Dada Asha na Remmy ambazo zilimpa umaarufu na kujulikana kwa haraka na kuwa simulizi katika kila pembe za mji  huo wa Tabora.

Shem alipata ushindani mkubwa baada ya kuwakuta wakali wengine wa kupiga gita akina Kassimu Kaluwona, Athuman Tembo pamoja na Salumu Luzila na  Issa Ramadhan ‘Baba Isaya’ lakini alijitutumua  na kuwa mmoja kati ya wapiga solo gita  bora la katika bendi hiyo.

Mwaka wa 1983 Shem Kalenga aliicha bendi hiyo kwa sababu zake mwenyewe na kuachana na mambo ya muziki kwa muda.Lakini baada ya kuondoka yeye bendi hiyo haikudumu tena na ikapotea katika ramani ya muziki.

Aliondoka Tabora  mwaka 1990  baada ya kuitwa na mfanyabiashara wa jijini Dar  es Salaam Baraka Msilwa ambaye alimuomba ajiunge katika bendi yake ya M.K. Beat iliyokuwa ikipiga katika mtindo wa ‘Tunkunyema’ Bendi hiyo ilikuwa ndugu na ile ya M.K. Group.

Ndani ya M.K.Beat Shem Kalenga  aliwakuta vijana machachari akina Maliki Star, Bwani  Fanfan, Sisco Lunanga na Fungo Shomari. Kwa mshikamano waliokuwa nao  waliweza kuiinua Bendi hiyo vilivyo na kuwa tishio kwa bendi zingine za jijini Dar es Salaam.

Bendi hiyo ilisambaratika mwaka 1995 na mwaka uliofuatia alianzisha bendi yake ya Tabora Jazz Star ambayo ina wanamuziki sita na huburudisha katika kumbi mbalimbali za jijini Dar  es Salaam hadi sasa. 

Anasema miaka ya hivi karibuni biashara huria ziliporuhusiwa, Studio nyingi binafsi zilifunguliwa lakini hazina manufaa kwao kufuatia kiwango cha pesa zinazotozwa na Studio hizo  kuwa kubwa mno kiasi cha wao kushindwa kumudu kulipia.

Kalenga anatoa wito kwa Serikali aidha kwa  wafadhili kuwaona kwa jicho la huruma wanamuziki hao wazamani kuwawezasha  kwa vile bado wanao uwezo mkubwa wa kupiga muziki na kutoa elimu kwa jamii pamoja burudani kwa wapenzi kama zamani.

Anajutia umaskini na ufinyu wa fikra uliowakumba wanamuziki wa dansi wa zamani umewafanya kushindwa kujitutumua na kwamba wanchosubiri ni kudra za mwenye mungu, serikali, wafadhili au yeyote atakayeguswa  kutaka kuwakwamua  wakongwe hao kwa kuwapatia vyombo vya muziki.

Shem Kalenga anakumbuka miaka ya nyuma jinsi Serikali ilivyokuwa ikiwasaidia kurekodi nyimbo zao bure katika Studio za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ambapo  gharama yao ilikuwa ni nauli ya kwenda Dar na kurejea  Tabora.

Anaendelea kuifagilia Studio RTD  enzi hizo ilivyokuwa ikichuja nyimbo zao  tofauti na sasa ambapo  Studio nyingi zinarekodi pasipo kuzichuja matokeo yake baadhi ya nyimbo zinazosikika katika vituo vya redio hazina maadili mema kwa jamii.
Mzee mzima Kalenga ambaye sifa zake zimezagaa kila kona Afrika ya Mashariki na Kati anawaasa vijana wa muziki wa kizazi kipya kujifunza kupiga Ala za muziki badala ya kutembea na CD mkononi. 

PICHA ZAIDI.
MTUNZI NA MWIMBAJI WA SOUKOUS STARS, MAYAULA MAYONI, AKIMPONGEZA SHEM KARENGA{kushoto} KWA UHODARI WA KULIKUNG'UTA SOLO,JIJINI DAR ES SALAAM.


No comments: