Thursday, January 3, 2013

KANKU KELLY, ALIYEFUKUZWA SHULE KWA SABABU YA KUPENDA MUZIKI
NKASHAMA KANKU KELLY ni mpigaji mashuhuri trampeti mwenye historia ya ndefu katika muziki.
Ni mwanamuziki aliyewahi kushikana mikono na viongozi wakubwa wanaoheshimika  duniani kote, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Nelson Mandela.
Kanku ambaye alifukuzwa shule kwa ajili ya muziki, jina lake halisi ni Nkashama Luis Polycarp, alizaliwa Januari 20, 1958, katika mji wa Kananga Mkoa wa Kasai, Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kanku ambaye aliingia nchini Tanzania akiwa kinda ‘Under Twenty’ alikuwa kivutio kikubwa kwenye safu ya wapulizaji wa trumpet katika bendi iliyokuwa tishio miaka ya 1970 hadi 1990 ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa White House,Ubungo jijini Dar es Salaam.

Baba yake mzee Chasuma Leonard alikuwa Daktari wa binadamu na mama yake Chibwabwa Kayipu, alikuwa mfanyabiashara katika mji huo wa Kananga.

Kelly alipata elimu ya msingi katika shule ya Kamilabi ambayo miongoni mwa masomo yaliyokuwa yakifundishwa somo la muziki lilikuwemo. Baadaye aliendelea na masomo ya juu  katika shule ya Sekondari ya Lyceede Kelekele, ambako aliishia kidato cha tano kwa kufukuzwa shule baada ya kufumwa na mwalimu akiandika  wimbo wa Nyboma Mwandido darasani mwaka 1973.

Akiwa shule ya msingi walifundishwa somo la muziki na yeye alikuwa akifanya vizuri sana na kuwa mmoja kati ya wanafunzi bora wa somo hilo.

Akifafanaua juu ya kufukuzwa shule, Kelly anasema “Nilikuwa anapenda muziki kupita kiasi, nikiwa darasani mwalimu alinikuta nikiandika wimbo wa ‘Amba’ uliotungwa na Nyboma Mwandido ndipo nikafukuzwa shule”

Kanku anasema baada ya kufukuzwa shule mwaka 1974, alihitajika kujiunga na jeshi la nchi hiyo katika kitengo cha muziki wa Brass band, lakini akakataa akiwa na dhamira kubwa kuwa mwanamuziki masuhuri.
Anajuza kuwa jamaa zake aliokuwa nao darasani asilimia tisini  walipelekwa jeshini kupiga muziki wa Brass band.

Katika kujitafutia maisha mwaka 1975  Nkashama Kelly aliamua kwenda mji wa Katanga uliopo jimbo la Shaba, huko alijiunga katika bendi ya Safari Nkoi iliyokuwa na wanamuziki mahiri akina Ndala Kasheba na Baziano Bwetii.

Nyota yake  ilianza kutoa nuru njema, kwani mwezi Febrauri 1977 baadhi ya wanamuziki Kongo walifuatwa na Chibangu Katai ‘mzee Pual’ kuja Tanzania kujiunga na bendi ya Maquis du Zaire.

Anamtaja Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Mutombo Sozzy (drums), Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’(besi gita)  Ngalula Chandanda (stage shoo) pamoja na yeye Kanku ndiyo kwa pamoja  walichukuliwa kuja Tanzania waka huo.

 Alipofika Maquis du Zaire jijini Dar es Salaam, aliungana na wapulizaji wa trumpet wengine akina Mwema Mudjanga ‘mzee Chekecha’, Mino wa Mwamba ‘mzee Tito, Mpoyo Kalenga, Kaumba Kalemba  na Ngenda Kalonga.
Safu hiyo ilikuwa burudani tosha katika ukumbi wa White House wakati huo kwa jinsi walivyokuwa wakimudu kulimiliki jukwaa kwa uchezaji wao.
Kanku Kelly anatamka kwamba mwaka 1978 ilikuwa kama ‘bahati ya mtende kuotea Jangwani’ anasema hatakuja kuisahau siku ile  aliyopelekwa kukutana na Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam.

Anakumbuka alishikana mikono na rais wa Tanzania wakati huo, Mwalimu Nyerere na  alimuuliza “unatoka Kongo ya Lumumba”? Akiwa na hofu isiyokuwa na sababu, Kelly alijibu ‘ndiyo’

Maisha ni kutafuta. Ndivyo alivyosema Kanku kwamba mwanzoni wa mwaka 1981 alichomoka na kwenda kujiunga na bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS). Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara maarufu Hugo Kisima.
Katika kipindi  cha mwaka mmoja wa 1981 aliondoka Orchestra Safari Sound(OSS) kwenda kujiunga katika bendi ya mzee Makassy ambako huko nako hakudumu kipindi kirefu na alirudi tena OSS.

Mwaka 1982 Kanku alichupa hadi Nairobi nchini Kenya, na akajiunga na bendi ya Orchestra Virunga iliyokuwa ikiongozwa na mwanamuziki mkongwe Samba Mapangala, ambako alidumu na bendi hiyo kwa takriban miaka miwili.

Akiwa huko Kenya mwaka 1984 Nkashama Kanku Kelly akiwa na wanamuziki wenzake, waliamua  kuanzisha bendi yao ya Orchestra Vundumuna ikiwa na wanamuziki nguli akina Sammy Kasule (kuimba), Nsilu wa Bansilu ‘Manicho’(gita), Tabu Ngongo(sax), na  Tabu Fratal (gita/drums).
Wengine walikuwa akina Munamba Jean(keyboard)na Botanga Mofrank Bijing, ambaye alikuwa kiongozi wa bendi na mpiga keyboard.
Anamtaja Mofank kuwa ndiye aliyekuwa chanzo cha bendi hiyo kupata mikataba wa kupiga muziki nchini Japan kwa  kupitia nafasi yake ya kuoa mwanamke wa nchi hiyo.

Kanku Kelly ni Baba wa familiya. Alifunga ndoa ya kiserikali mwaka 1987 na  Bi. Mwajuma Kibwana ambaye ni mtanzania, katika jiji la Nairobi huko Kenya.

Katika maisha yao ya ndoa wamefanikiwa kupata mabinti wawili Agnes Chichi Kelly (26), anayesoma katika Chuo Kikuu nchini Malaysia na mdogo wake Lucy Kelly (20) ambaye anamuelezea kwamba amefuata nyayo zake  katika muziki.

Baada ya kuachiwa huru mzee Nelson   Mandela  toka gerezani, mwaka 1990 alifanya ziara ya kuizunguka dunia. Katika ziara yake hiyo alifika nchini Japan ambako bendi yao ya Vundumuna ilialikwa kutoa burudani katika sherehe za mapokezi ya shujaa huyo kwenye uwanja uliokuwa umefurika kumpokea.

Anasema mzee Mandela alivutiwa na wanamuziki wa Vundumuna ambao ni weusi. Mandela alipanda kwenye jukwaa lao kuja kuwashika mikono huku akiwauliza wanatoka nchi gani.

 Alipomfika yeye, akamuuliza swali lilelile kama aliloulizwa na Mwalimu Nyerere kuwa natoka Zaire ya Lumumba? “ Sitoshau maishani mwangu  siku hiyo” anasema Kanku.

Vundumuna ilifanya safari zaidi ya mara kumi kati ya miaka ya 1987 na 1991 kisha wakatengenezewa vikwazo vya hati yakufanya kazi hapo Japan (working permit), na walirudi nyumbani na ndiyo ikawa mwisho wa bendi hiyo.

Kanku Kelly akiwa bado kijana kwa wakati huo alikuwa ni mwenye ujasiri usiyetaka kushindwa kitu. Mei 15, 1992 aliingiwa na ujasiri wa kusimama kama yeye na  kuazisha bendi yake ya  The Kilimanjaro Connection.

Alifanikiwa kuwapata wanamziki mahiri na makini akina Asia Darwesh ‘super mama’ aliyekuwa mbonyezaji wa kinanda, Mafumu Bilari ‘Bombenga’ kwenye  Saxophone,  Andy Swebe kwa upande wa gita zito la besi, Burahan Muba, aliyekuwa mpiga gita la solo na Shomari Abdalah akizicharaza drums.

The Kilimanajaro Connection Band imekuwa ikipata mikataba ya kupiga muziki katika nchi mbalimbali za Singapore, Malaysia, Thailand na Oman.
 Ni usimamizi makini wa Kanku Kelly umeifikisha bendi hiyo kupata mafanikio makubwa pia bendi hiyo imekubalika sana nchini Malaysia.

Mwanamuziki huyo Kanku Kelly Nkashama ameviomba vyombo vya habari hususani vya utangazaji kuzicheza na kuzipiga nyimbo zao za zamani katika redio na Luninga ambazo kwake yeye anaziona kama ni ‘Lulu’ inayotoweka.

Anasema si vyema kubeza vya zamani ambavyo ndivyo vilivyotufikisha hapa tulipo.  Anawaasa vijana wanaopenda muziki kujifunza kutumia ala katika nyimbo zao. Kanku akafika mbali zaidi kwa kusema kwamba hakuna mafanikio bila kuvuja jasho.

Kanku Kelly ni raia halali wa Tanzania aliyefanikiwa kupata uraia  mapema Aprili 27, 2011. Matarajio yake ya baadaye ni kuwa ProdAuza mkubwa aiyekamilika kwa vyombo vya kufanyia kazi hiyo.
Ametoa shukrani nyingi za dhati  kwa watanzania wote waliomlea toka alipokuja hapa nchini, akiwa bado kinda wa miaka 19 hadi leo ana zaidi ya nusu karne.
PICHA ZAIDI.

No comments: