Wednesday, January 23, 2013

TABORA JAZZ ILIVYOTIKISA MJI WA TABORA






TABORA JAZZ   ‘Wana Segere Matata’ ni bendi pekee ya muziki wa dansi  inayojulikana huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kauli hiyo nzito ilitolewa na mkongwe wa muziki wa dansi toka Jamhuri  na Kidemokrasia ya Congo, Tabu Ley  Rochereau.

Akiwa ziarani hapa Tanzania, Tabu Ley aliwahi kufanya mkutano na waandishi wa habari katika hoteli Kilimanjaro. Moja kati ya  maswali aliyoulizwa ni kutaka kufahamu ni bendi gani hapa Tanzania wanayoijua huko kwao DRC. Tabu Ley pasipo kupepesa macho, alikiri kwa kujibu kwamba  ni Tabora Jazz pekee ndiyo inayojulikana huko.

Tabora Jazz ni bendi kongwe iliyoanzishwa mwaka 1954, ambao katika historia ya Tanzania ndiyo mwaka ambao chama cha TANU kilianzishwa.

Bendi hiyo ilikuwa  ikiongozwa na waanzilishi akina  Hamis Ali Songo na Mlekwa Selemani, ikiwa na makazi yake mjini Tabora ikipiga na kutoa burudani murua za muziki wa dansi katika kumbi za  Lumumba kwenye kona ya mitaa ya Usagara na Rufita ambako ndiko yalikuwa makao makuu yake. Pia walikuwa wakipiga katika Baa za Bizeta, Maua na nje ya mji wakialikwa.

Miaka ya nyuma Tabora Jazz ilikuwa na upinzani mkubwa na bendi ya Western Jazz ya jijini Dar es Salaam. Upinzani huo ulijiri baada ya Bendi ya Western Jazz kukwapua kwa nyakati tofauti nguli wawili toka Tabora Jazz., kwa ambao walihamisha ‘melody’ yao kuipeleka huko.

Wanamuziki hao walikuwa  akina Wema Abdallah na Rashidi Hanzuruni ambao walikuwa mahiri kwa kulicharaza gitaa la solo,ambao walihamisha ‘melody’ kuzipeleka Western Jazz.


Nyimbo nyingi za bendi hiyo zilipigwa mno katika  kituo cha Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kusikika  sehemu kubwa Afrika ya Mashariki na Kati.

Huko nchini Rwanda kulikuwepo redio Rwanda iliyokuwa na kipindi cha muziki nyakati za jioni kikiendeshwa na mtangazaji Kabendera Shinani, ambaye alikuwa akizipiga nyimbo za Tabora Jazz kila mara. Redio hiyo ilikuwa ikisikika hapa nchini maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kagera (Ziwa Magharibi) wakati huo.

‘Wana Segere matata’ waliwika sana miongoni mwa bendi kubwa hapa nchini zikiwemo Morogoro Jazz, Cuban Marimba, Western Jazz, NUTA Jazz, Dar. Jazz, Kilwa Jazz, Urafiki Jazz, Jamhuri Jazz na nyingine nyingi.

Mji wa Tabora wakati huo ulikuwa na ushindani mkubwa katika muziki kati ya Tabora Jazz na bendi zingine zilizokuwepo wakati huo za Kiko Kids iliyokuwa ikiongozwa na Salimu Zahoro na Nyanyembe Jazz iliyoibuka na kibao chake cha ‘Rangi ya Chungwa’ wimbo ambao hadi sasa bado unarindima kwenye vituo vingi vya redio na kumbi nyingi  za burudani hapa nchini.
Pia mji wa Tabora enzi hizo kulikuwa na umkumbi mkubwa wa Disco uliokuwa ukijulikana kwa jina la ‘Mwana Isungu’ uliokuwa ikiteka kundi kubwa la  vijana wa mji huo kwa kuporomosha muziki maridhawa, zikiwemo nyimbo za Tabora Jazz na Nyanyembe Jazz.

Kama nilivyokudokeza hapo awali kwamba bendi hiyo ilianzaishwa kabla ya  Tanganyika kupata Uhuru, hivyo iliendeleza mfumo wa kikoloni. Mfano mmoja ni kwamba katika miaka ya 1960 ilikuwa ni marufuku kwa mpenzi au shabiki kuingia ukumbini kucheza muziki pasipo ‘kunyonga’ Tai shingoni, licha ya pesa zake. Hii ilikuwa ni moja ya njia ya kuzingatia utanashati na nidhamu  kwa ujumla.

Bendi hiyo ilipiga katika mitindo ya  Segere matata, Segua Segua, na Mambo Milekana, ikiwazingua wapenzi wa muziki mjini humo.
Miaka hiyo Tabora Jazz alitoka na nyimbo zao ngingi zikiwemo za Usijifanye mwewe, Mariam mpenzi, Zabibu No.2, Anna, Regina, Mambo Mileka, Tucheza Segere, Dada Mwantumu, Serafina,Tamaa yako, Alhamdulilah, Nashukuru sana, na Dada Asha.

Zingine ni pamoja na Zabibu, Halima, Dada Helena, Lucie, Farida na Dada Mwantumu.
Kufuatia ushindani mkubwa uliokuwepo mjini humo  kati yake na Nyanyembe Jazz na Kiko Kids, Tabora Jazz ilifumua vibao ingine vikali  vya Chakula kwa Jirani, Mapenzi hayana mganga, Mambo Mileka, Ujana una mwisho. Salima, Dada Remmy, Tucheze Segere na  Rukia wajidanganya.

‘Segere matata’ wakati huo ilikuwa na mashabiki waliokubuhu. Kwa wakazi wa Tabora mjini hawawezi kumsahau shabiki mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Mzee Segua’ ambaye alikuwa hakosi onyesho lolote la bendi hiyo akicheza ‘Segua Segua, mtindo aliokuwa aikiumudu hadi kufikia kupachikwa jina la ‘Mzee Segua’

Alikuwa ni Mzee mwenye vituko ukumbini, akiwa na mfanyakazi katika Ofisi moja ya serikali mjini humo  kama dereva. ‘Mzee Segua kwa mapenzi yaliyopitiliza mbele ya tabora Jazz, alidiriki kukakataa uhamisho kwenda Wilaya ya Urambo, akitoa sharti ili aende huko basi Bendi hiyo nayo ihamishiwe Urambo. Yaelezwa kwamba baadaye alifukuzwa kazi.


Kikosi kamili cha wanamuziki waliokuwa wakiunda kikosi kamili cha bendi hiyo kilikuwa cha akina  Athumani Tembo kwa upande wa gitaa la Soloakisaidiana na  Shem Ibrahim Karenga aliyekuwa akipiga gitaa la solo, akitunga na kuimba.  Salumu Luzira  alikuwa akiliungurumisha gitaa zito besi na  ugeweza kulilingalinisha na alivyokuwa akipiga Suleiman Mwanyiro ama Lofombo wa  Empire Bakuba.

Wengine katika safu hiyo walikuwa  Kassim Kaluwona, aliyekuwa akilicharaza gitaa la rhythm akisaidiana na  Issa Ramadhani ‘Baba Isaya’  Waimbaji walikuwa ni akina Ramadhani Hamis Nguligwa, Ismail Mwangoko, na Msafiri  Haruob, ambaye baadaye alijiunga na Mwenge Jazz ya Jijini Dar es Salaam.

Kuna msemo wa waswahili usemao kwamba ‘ Vizuri huigwa na Vitamu huonjwa’  Msemo huo ulijidhihirisha wazi kwa Bendi kubwa toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya Soukos Stars, ambayo iliiba nyimbo za Dada Asha wa Tabora Jazz na Vigeregere wa Western Jazz.


Kwa umahiri mkubwa wa bendi hiyo ya  Soukous Stars ilitoka na mseto wa nyimbo nyingi zikiwemo za Dada Asha na Vigeregere  katika album moja ya ‘ Nairobi by Night’

Shem Karenga alijaribu kufuatilia  haki miliki yake pasipo mafanikio kwa kuwa nchi yetu ilikuwa bado haijatunga sheria ya haki miliki.

Tabora Jazz iliposambaratika mwaka 1980, sanjari na Bendi za Nyanyembe Jazz na Kiko Kids, nazo zilienda mrama na baadaye kuondoka katika taswira ya muziki hapa nchini.
Kutoweka kwa Bendi hizo kuliwaacha wapenzi wa muziki wa dansi wa mji huo ambao waliupachika jina la ‘Mboka’ wakijawa na simanzi tele, licha ya kuanzishwa kwa bendi nyingine ya Tabora Jazz ‘Sensema Malunde’ ambayo imeibuka miaka ya karibuni ikiwapa burudani.


Picha zinafyatia....

No comments: