Tuesday, February 26, 2013

HISTORY of DEKULA KAHANGA 'VUMBI'

 DEKULA KAHANGA 'VUMBI'  AKICHARAZA NYUZI ZA GITA LA SOLO HUKO SWEDEN.


 DEKULA KAHANGA AKIPIGA GITA KATIKA UKUMBI WA WHITE HOUSE UBUNGO DAR ES SALAAM, TANZANIA.
 DEKULA KAHANA AKIWA KATIKA PICHA YA 'POZI' NA GITA LAKE.
 'MAMBO YA ULAYA' VUMBI AKIWA NA FARASI.

DEKULA  KAHANGA ‘VUMBI’  ALIZIBA PENGO LA NGUZA

Na Kiyungi Moshy
January 28, 2013

KATI YA WANAMUZIKI  WAAFRIKA waliopata mafanikio makubwa kwa kuchacharika, jina la Dekula Kahanga haliwezi kukosa. Ni mwanamuziki wa dansi, aliyefanikiwa kuanzisha bendi yake katika jiji la Stockholm nchini Sweden baada ya ‘kuitosa’ Maquis Original.
Dekula ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Vumbi’,  anasisitiza kwamba mafanikio yoyote katika maisha ni lazima mtu kuwa na malengo, na dhamira ya dhati, hatimaye kufanya maamuzi magumu.
Kabla ya kwenda nchini Sweden, ‘Vumbi’ alikuwa mpigaji wa gita la solo katika bendi ya Maquis Original, iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Lang’ata  Kindondoni jijini Dar es Salaam, miaka ya 1990.
Akiwa katika mapumziko mafupi nyumbani kwake Mikocheni kwa Warioba  jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Dekula alitamka baadhi ya maamuzi magumu aliyoyafanya mojawapo ni lile la kondoka katika bendi hiyo ya Maquis Original, na kutokomea kwenda Sweden bila kujua atakuwa mgeni wa nani huko ughaibuni.
Vumbi anaeleza kwamba hivi sasa hajutii maamuzi yake kwakuwa amepata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kumiliki bendi yake iitwayo Dekula Band. Amesema bendi hiyo hupiga muziki kwa mkataba mara mbili kwa mwezi katika ukumbi wa Lala Vin, mjini Stockholm nchini Sweden.

Dekula Band ina  wanamuziki mahiri toka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo akina Luhembwe Mwanahita ‘Bobo Sukari’ ambaye ni mwimbaji na kucheza Show, Sammy  Kasule, huyo ni injinia pia huimba, kupiga gita la besi, drums na kinanda. Wengine amewataja kuwa ni Joe Gerald Nnaddibanga, ambaye huimba, kupiga konga na kucheza show, Christina Frank, na Marceline Kouakoua.
Mwenye Dekula Kahanga, hulicharaza gila la solo na rhythm pamoja na Arne Winald ambaye ni mbonyezaji wa kinanda. Safu hiyo kwa pamoja huufanya muziki wao kukubalika kimataifa hadi kupelekea kupata mialiko lukuki ndani na nje ya Sweden zikiwemo nchi za Ulaya, Asia, Marekani, Japan,  Falme za kiarabu na Afrika.
“ Hakuna kitu muhimu kama kuwa na mahusiano  mema na baadhi ya watu toka nchi mbalimbali ninazotembelea. Nimefikia kuweza kuongea  kwa ufasaha lugha tano tofauti za Kiswahili, Kiingereza,  Kifaransa, Lingala na Kiswidish” Anajigamba Dekula ‘Vumbi’.
Historia ya Dekula Kahanga anailezea kwamba  alizaliwa mwezi Aprili 02, 1962 katika kijiji cha Lumera, Wilaya ya Kivu  Kusini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ni baba wa familia akiwa na mke na watoto watatu. Dekula ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kadhaa wa Mzee Aloyce Obeid Dekula,  aliyekuwa mfanyakazi katika serikali ya Zaire iliyokuwa ikiongozwa na rais Mobutu Seseseko.

Alipata  elimu ya Sekondari katika shule mbili tofauti za Bukavu na Uvira huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alihitimu kidato cha nne  mwaka 1979. Mwaka uliofuatia wa 1980, safari yake katika muziki ilianza kwa kujiunga na bendi za Bavy National, na Grand Mike jazz, ambako alikutana na wanamuziki akina Kyanga Songa na Issa Nundu.
Akiwa huko kwao wilaya ya Kivu, ‘Vumbi’ alikuwa msikilizaji mzuri wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo ilikuwa ikisikika wakati huo na alizitamani sana nyimbo zilizokuwa zikiporomoshwa na bendi za Morogoro Jazz, Jamhuri Jazz, Tabora Jazz, Nyamnyembe Jazz,  NUTA Jazz,  Mlimani Park, Maquis du Zaire na Orchestra Safari Sound.
Kamwe hatomsahau  John Luanda katika historia ya maisha yake, kwa kuwa huyo ndiye aliyekuwa chanzo cha yeye kuingia hapa Tanzania. Luanda alikuwa akimiliki bendi ya Chamwino Jazz,  aliwachukua toka Kongo akiwa na wenzake  akina Bwami Fanfan, Sisco Lunanga na Baposta kwa madhumuni ya kujiunga katika bendi yake ya Chamwino. Bendi hiyo wakati huo  ilikuwa ikipiga muziki maeneo ya Tandale huko Manzese,  jijini Dar es Salaam.
“Mwenye bahati habahatishi” ndivyo anavyosema mkung’utaji mahiri wa gita la solo Dekula Kahanga ‘Vumbi’,  kwamba mwaka 1980 alikutana na mwanamuziki  Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Viking’ katika ofisi za ubalozi wa Kongo hapa nchini.
Nguza wakati huo alikuwa mpiga gita la solo pia alikuwa ni mmoja kati ya  wanahisa wa Orchestra   Maquis Comapy  (OMACO) na  mmoja kati ya viongozi wa bendi ya Orchestra Maquis du Zaire. Katika maongezi yao, Chimbwiza  Nguza alimpa mwaliko yeye na wenzake kwenda kuburudisha kwenye ukumbi wa White House, uliokuwa maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Dekula alikubali mwaliko huo na Weekend moja walifika na kupewa nafasi ya kuburudisha kwa muda mfupi.
Walipopanda jukwaani waliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi wa muziki waliokuwa wamefurika ukumbini humo pamoja na wanamuziki wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire.
Dekula Kahanga baadaye aliitwa na uongozi wa bendi ya Maquis du Zaire akina Chibangu Katai ‘Mzee Paul’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’ wakimtaka aandike barua ya kuomba kujiunga na bendi yao kwa mkataba usio na mshahara. Alitakiwa na bendi hiyo ili kuziba nafasi ya Nguza ambaye alikuwa tayari ameanza mgomo baridi. Vumbi alikubali na akajiunga na Maquis du Zaire.

Vumbi anaikumbuka siku mmoja wakipiga muziki katika ukumbi wa  Temeke Stereo,  alimuona Nguza  akiwa amejibanza pembeni mwa ukuta ukumbini humo huku akisikiliza midundo inavyounguruma..
“Nilipomuona,  nikaingiwa na hofu kubwa nikijihisi kama ninamvunjia heshima Nguza. Nikaomba  nimpishe ili ashike nafasi yake” Anasema kwa kujiamini Dekula Kahanga.
Lakini  viongozi wake akiwemo Chibangu Katai ‘Mzee Paul’ na  Ilunga Lubaba, walimwamuru aendelee kushika ‘mpini’.
Kwa amri hiyo, ilikuwa kama Fisi aliyeachiwa  Bucha kuilinda. Aliweza kuzicharaza kwa umahiri mkubwa nyimbo zote alizokuwa zikipigwa Field Marshal  Nguza zikiwemo za Makumbele, Ngalula Seya Malokelee, Karubandika, Mage, Dora mtoto wa Dodoma, Clara, Mwana yoka ya Babote, Nimepigwa ngwala na nyingine nyingi pasipo kutofautisha kati yake na Nguza.
Aliachiwa  kulivurumisha gita hadi  mwisho wa onyesho hata mpiga solo Ilunga Lubaba hakutaka kuligusa siku hiyo. Baada ya hapo kwa adabu zote alikwenda kumsalimia na Nguza pale alipo naye hakusita kumpa hogera kwa kazi  nzuri.
 “Mungu mkubwa,  siku hiyo Nyota yangu iling’ara kiasi kwamba hata mimi mwenyewe sikuweza kuamini nilichokuwa nikikifanya jukwaani hapo” Anasema  Dekula Kahanga ‘Vumbi’ huku akitabasamu.

Taharuki kati ya uongozi wa  Maquis du Zaire  na Nguza ‘Vicking’ ziliendelea hatimaye aliondoka rasmi bendi hiyo, hadi kwenda kuanzisha bendi yake ya Orchestra Sambulumaa akiwa na mwanamuziki wengine akiwemo mwanaye Papii Kocha. Bendi hiyo ilikufa baada ya Nguza na mwanaye huyo kuhukumiwa kutumikia kifungo  cha maisha gerezani.

Miaka ya 1989 na 1990 Dekula alikuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa Maquis Original,  jina lililozaliwa toka Maquis du Zaire baada ya kuhamia katika ukumbi Lang’ata Kinondoni. Mtunzi na mwimbaji Maquis Original Tshimanga Kalala Assosa,  alikuwa akipaza sauti ya kumpandisha mori kwa kumuita mara kwa mara Vumbiii,Vumbiii,Vumbiii kama kibwagizo wakati wa chorus kwenye  wimbo wa Ngalula.

Vumbi wakati huo alikuwa na umri ambao unamruhusu kuhangaika kutafuta maisha yenye maslahi mazuri. Hivyo maamuzi magumu yakaanzia hapo Lang’ata baada ya kuamua kuicha bendi ya Maquis Original, iliyompa jina na kuchepukia katika jiji la Stockholm nchini Sweden.
 
Akiwa Stockholm, Vumbi alianza kuchacharika mitaani  akitafuta bendi ya kupiga,  hatimaye akakutana na mwanamuzi toka Uganda,  aitwaye  Sammy Kasule. Mwaka 1993 wakaamua kuanzisha bendi yao ikiitwa  Makonde Group.
Mwaka 1999, Dekula Kahanga alifyatua Album iitwayo Bolingo Ekesemi iliyosheheni nyimbo za ‘Dunia kuna mambo’ na ‘mpenzi Asha’

Dekula Kahanga anajivunia kwamba yeye ni  mwanamuziki wa kwanza toka Afrika huko Sweden, kufyatua album.  Alitoa album iitwayo ‘DEKULA Sultan Qaboos’ yenye nyimbo za Sultan Qaboos, Mon Amour, Babylon, Mayanga, Rozina, Mambo leo na Nostalgie  nyimbo hizo  anasema zinazopigwa mno katika vituo vingi vya redio Duniani.
Ili kupata unafuu wa maisha nchini Sweden,  Dekula alilazimika kuomba uraia wa nchi hiyo hivyo ilifuata taratibu zote. Alichukua maamuzi magumu mengine ya kuukana uraia wa nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili kupata uraia wa nchi hiyo.
Hivi sasa yeye na wanamuziki wenzake wa bendi hiyo ni  raia halali wa nchi ya Sweden na wanaweza kusafiri kwenda nchi za Marekani Ulaya Asia na kwingineko pasipo kuomba VISA.

Dekula ametoa mwito kwa wanamuziki chipukizi kujifunza kupiga ala za muziki ili wafikie viwango vya kuwa  wanamuziki. Pia amewaasa kuacha kulewa sifa ndondogo pia kuepuka anasa zisizo na tija.
“Nawapenda sana Watanzania, walinipokea,  wakanilea, wakanithamini na wakanipenda. Ninatarajia kutoa zawadi endelevu  kwa Watanzania siku za usoni kuanzisha bendi ya vijana, itakayokuwa ikitumia ala za muziki wa kisasa” anamaliza Dekula Kahanga Vumbi.

Mwisho.



No comments: