Tuesday, February 26, 2013

BIOGRAPHY YA 'IRON LADY' ASHA BARAKA


KUTANA NA MAWNAMKE JASIRI   ASHA BARAKA.

Na: Kiyungi Moshy.
January 20, 2013

Asha Baraka ni mwanamke wa mfano wa kuingwa kwa ujasiri mkubwa, asiyesita kujaribu na hatimaye kufanikiwa.
Mama huyu ana vipaji lukuki ambavyo kwa kauli yake anasema vingine bado hajavionyesha.

Baadhi ya vipaji vyake hivyo vilianza kujitokeza akiwa katika shule ya Sekondari ya Tabora Girls alipokuwa katika mchezo mpira wa Pete na kikapu, iliyomfikisha kuchaguliwa timu ya shule.
Kwa uhodari wake katika michezo hiyo Asha baadaye alichaguliwa kuwa mmoja kati ya wanafunzi waliounda timu ya UMISETA mkoani Tabora.

Akiieleza historia ya maisha yake,  Asha amesema alizaliwa katika kijiji cha Mwandiga, kilichopo katika Wilaya Kigoma Vijijini , Mkoani Kigoma.
Masomo yake ya msingi aliyapata katika shule mbili tofauti. Darasa la kwanza hadi la tatu alisoma katika Shule ya msingi Kipampa iliyopo Ujiji, mjini Kigoma.
Baba yake Mzee Ramadhani Baraka alikuwa Daktari hivyo alihamishwa kwenda kufanya kazi katika hospitali nyingine ya Nguruka, mkoani humo.
Asha alilazimika kuandamana na wazazi wake kwenda Nguruka, akiwemo mama yake mzazi, maliyemtaja kwa jina maarufu la Mama Ali Baraka.
Alisoma katika shule ya msingi Nguruka darasa la nne hadi alipofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Asha Baraka alikuwa ‘Kichwa’ kweli kweli darasani, alifaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kwenda kusoma katika Sekondari ya vipaji maalumu ya Tabora  Girls,  iliyopo mkoani  Tabora.
Akiwa shuleni hapo alicheza mpira wa pete na kikapu hatimaye alichaguliwa kuwakilisha mkoa wa Tabora,  akiwa katika timu ya mpira wa Pete.
Licha ya kucheza mchezo wa Pete na kikapu,  Asha Baraka alikuwa mwanariadha mashuhuri akikimbia mbio za mita 100,  na kuwa kati ya mwanamichezo bora shuleni hapo.

Alipomaliza masomo ya Sekondari mwanzoni mwa miaka ya 1980, aliajirawa katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) la jijini Dar es Salaam katika Idara ya mauzo na masoko.
Asha Baraka ni mama mwenye familiya ya mume na watoto wawili wa kiume.  Anawataja kwa majina kuwa ni Mope mwenye umri wa miaka 18, ambaye ansema  amefuata nyayo zake za uhezaji wa mpira wa  kikapu Alichaguliwa katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18. Mwingine ni  Imani mwenye umri wa miaka 14, ambaye  ni mwanafunzi katika shule ya  Sekondari ya Bearden Paul, iliyopo  Wilaya ya Bagamoyo.
Asha licha ya majukumu yake ya kazi,  pia alikuwa  akijishughulisha kibiashara kwa kuongoza kundi la vijana waisopungua 45, katika bendi ya African Stars ‘ Twanga Pepeta’

Nikukumbushe kwamba  enzi za miaka ya nyuma kulikuwa na mipango mzuri ambapo mashirika mengi ya umma yalikuwa na timu za mpira wa miguu,wavu,  kikapu, pete hadi bendi za muziki wa dansi.
Shirika la Bima la Taifa lilikuwa mojawapo ambalo lilikuwa natimu ya mpira wa pete halakadharika ilikuwa na bendi ya Bima Lee Orchestra.
Alicheza mpira wa pete na kikapu  katika  timu ya Bima  pia lichaguliwa  katika timu ya wilaya hadi ya mkoa wa Dar es Salaam.
Kipaji kigine cha mwana mama huyo ni kile cha kuchaguliwa katika timu ya ya taifa ya riadha, akikimbia mbio za mita 100, kabla ya kuchujwa wakiwa kambini jijini Arusha.
“ Siwezi kumshau Juma Ikangaa ambaye aliniletea viatu mahsusi kwa ajili ya kukimbilia (Sparks) toa Japan. Kabla ya hapo, nilikuwa ninakimbia nikiwa na viatu vya raba” anasema Asha Baraka.

Anatolea mfano wa mwanariadha wa zamani ambaye aliyepata mafanikio makubwa licha ya kutokuwa na zana, Mwinga Mwanjala. Mwanjala alishinda mashindano ya kitaifa ikikimbia bila viatu ‘Pekupeku’
Asha anatanabaisha kwamba hata kuchaguliwa kwake kukimbiza mwenge wa Olympic haukufanyika kwa upendeleo, anasema yeye ni  mwanariadha wa  siku nyingi mwenye rekodi kitaifa.
 Kama nilivyokueleza hapo awali kuwa Asha ana vipaji vingi mno, alionyesha maajabu baada ya kuendesha gari akiwa na umri mdogo wa miaka 14, wakati huo alikuwa kidato cha pili hapo Tabora Girls.

Anaeleza kwamba hata alipoanza kazi  Shirika la  Bima, watu wengi wakiwemo wafanyakazi wenzake, walikuwa wakimshangaa kumuona binti mdogo  wakati huo  akiendesha ‘mkoko’ kuja kazini.
Mama Asha kupitia uzoefu wake wa muda mrefu wa kuendesha magari, aliwahi kupatwa na shauku ya kushindana katika mbio za magari hapa Tanzania. Asha alikosa gari maalumu la mashindano hayo, licha ya kufanya mazoezi makali kupitia maeneo mbalimbali hadi Chalinze.
“ Nilikuwa napenda sana  kuendesha magari, nilifanya mazoezi ya kushindana nikapitia maeneo mengi hadi Chalinze. Anajisifu Asha Baraka.
Analisema kwamba Pamoja na kukosa gari, alijichomeka katika  katika gari la wasindikizaji na kuweza kuzunguka toka mwanzo wa safari hadi mwisho wa mashindano hayo.

Ujasiri wa mama Asha ulionekana mwaka 2010, baada ya kuacha kazi yake nzuri katika Shirika la  Bima la Taifa (NIC) na kuamua kujikita katika Biashara na Siasa.

Shirika la Bima la Taifa mwaka 2000, liliwataka waajiriwa wote  kuomba kazi upya. Japo yeye alikuwa nje ya mji kikazi wakati huo, lakini aliporejea hakutaka kuendelea na kazi,  hivyo akaamua kutoandika barua ya maombi ya  kazi hatimaye akacha kazi rasmi 2010.

Asha  baada ya kuacha kazi Shirika la Bima la Taifa (NIC) aliamua kujikita katika Biashara na Siasa.
Kwa upande Siasa,  Asha Baraka hivi sasa  ni mjume wa National Executive Committee (NEC) kupitia wilaya mpya ya Uvinza, iliyopo mkoani Kigoma.
Anajuvunia kuwa karibu na wanamuziki wake wa African Stars, wana ‘Twanga Pepeta’  kwa kuwa anapata muda wa kuzungumza na   kuelewa matatizo yanayoikabiri bendi sanjari kujua  mafanikio.
Historia inaeleza kwamba  kabla ya kuwa  kampuni African Stars Entertainment Tanzania (ASET), kulikuwa na bendi ya  African Stars iliyoanza mnamo tarehe 01 July 1994, katika Hoteli ya  Bahari Beach jijini Dar es Salaam.
Baadaye bendi za M.K.Group, M.K. Beat na M.K. Sound  zikaanzishwa na Alli Baraka, aliyekuwa mfanyakazi wa  Shirika la Ndege la Zambia (Zambia Airways) baadaye akawachia  uongozi Msilwa Baraka, aliyekuwa kwa  Mwenyekiti na  Asha Baraka akawa Mkurugenzi Mtendaji.
Kampuni ya African Stars Entertaiment Tanzania (ASET) iliyoasisiwa mwaka 2000 na  yeye kuwa  Mkurugenzi wa Kampuni hiyo.
Anasema ASET ni mithiri ya Chuo ambacho kinatengeneza vipaji kwa vijana  kisha kuwaruhusu kwenda  popote wanapohitajika pasipo mashrti.
“Tuna   Academy ya kuendeleza vipaji vya vijana, inayoitwa Twanga Pepeta   Acade Asha ni Mkurugenzi wa kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET) ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 2000 jijini Dar es Salaam.
my. Vijana hao hupewa nafasi ya kupiga muziki siku za Jumamosi pale Mango Garden, kabla ya African Stars  wana ‘Twanga Pepeta’  kupanda jukwaani” Anasema mkurugenzi huyo wa ASET.
Akiyaelezea mafanikio katika kampuni yake ya ASET,  Asha anasema ni makubwa sana licha ya kwa kuwa wana Academy na pia ina wanamuziki wa kuingia na kutoka wapatao 45. Vilevile wamekwisha tunukiwa tuzo kibao zikiwemo za BBC, BASATA, ile Mascut  huko Arabuni ambako kulifanyika  festival. ASET imekuwa mstari wa mbele kuisaidia jamii katika matatizo mbalimbali ya kijamii.
Mojawapo ni lile la Asha kuandaa onyesho maalumu la muziki ambalo pesa zilizopatika hapo,  alizikabidhi kwa mwanamuziki mkongwe Maalim Gurumo ambaye hali yake ya kiafya bado ni tete.
Mwaka  2000 wakati wa shindano la Tanzania Musical Awards, The African Stars Band ilifanikiwa kuwa bendi bora ya mwaka kwa mwaka 2000/2002 na wimbo wa Kisa cha Mpemba ukawa ndiyo mwibo bora namba mbili.
 Asha Baraka alimalizia kwa kuwataka wanasanii wa tasnia zote kuzingatia  upendo na nidhamu ambayo kwake yeye anaona kuwa ndiyo nguzo kuu kwa mafanikio ya msanii.

Mwisho.

Mwanadishi wa makala hii anapatikana kwa:
0713331200, 0784331200, 0767331200 na 0773331200
m_kiyungi@yahoo.co.uk

No comments: