Wednesday, February 27, 2013

MBILIA BELL ALIKATAA KUOLEWA NA WAZIRI.


           MBILIA  BELL
ALIKATAA KUOLEWA NA WAZIRI


 Na: Kiyungi  Moshy.

MBILIA BELL ni mwanamuziki alinyeonyesha ujasiri kwa kukataa kuolewa na Waziri katika serikali ya nchi ya Gabon huko Afrika  ya  Kati, aliyempa sharti la kuacha muziki ili amuoe.
 Bell ni mama aliyejaaliwa kuwa sura, umbo lililojengeka lenye  mvuto, sauti nzuri ya uimbaji na hata uchezaji wake katika jukwaa.

Ni mwanamuziki  mwenye sifa adimu ambazo pengine yawezekana zisisifikiwe na mwanamke mwingine.
Sifa  nyingine kubwa aliyonayo mwama mama huyo ni kwa aliolewa na mwanamuziki nguli Tabu Ley na ndoa yao ya kifahari iliyofungwa ndani ya ndege wakiwa hewani.

Jina lake halisi ni Marikirala Mboyo, ambaye kama walivyo watoto wengine wa kiafrika wafikiapo umri wa miaka  minane, hukaa na wazazi, Babu au nyanya zao na kulazimishwa kusikiliza hadithi pia  kuimba nyimbo za asili inayowazunguuka.

M’bilia alikuwa mmoja wa hao baada ya kuvutiwa na sauti ya babu yake ambaye alikuwa bingwa wa kuimba, wakati Bibi yake alikuwa mchezaji wa ngoma asiyeshindwa kijijini humo.

Marikirala M’bilia alizaliwa mwaka 1959 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na alianza kuimba akiwa na umri wa miaka 17 akiwa na mkongwe Abeti Massekini mwaka 1976.

Akiielezea historia yake Bell anasema alianza kupenda muziki baada ya kuangalia katika televisheni na kumuona mwanamuziki nyota toka nchi ya Togo, Bela Bello, ailiyekuwa akifanya onyesho katika mji wa Kinshasa  huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Anasema alivutiwa na kipaji cha mwanamuziki huyo na kutamani siku moja aje kuwa kama Bello. Ansema siku aliyosikia kwamba amefariki, alilia kwa  siku kadhaa.

Baada ya siku saba kupita, akiangalia televisheni, alimuona mwanamuziki mwingine AbÈti Massekini. Baadaye akaamua kumuandikia barua Abeti ya kuomba kujiunga na bendi yake. Alishangazwa kuona  Abeti alipomualika kujianga naye. Hapo  ndipo historia katika muziki wake ilipoanzaia. Alijifunza kuimba akiwa karibu na Abeti kwa kipindi cha miaka minne.

M’bilia baada ya kujiamini amefuzu, aliondoka kwa AbÈti  na kwenda kuungana na Sam Mangwana, ambaye aliwasiliana naye  baada ya kumuona katika televisheni akifanya vitu vyake.  Lakini huko nako hukukaa sana kwani baada ya miaka miwili aliondoka na kujiunga na gwiji la muziki Afrika Tabu Ley Rochereau mwaka 1981.

Bell alipatwa na mshituko siku aliyokutana na kiongozi wa bendi ya Afrisa International Tabu Ley, akiwa na uso wa furaha katika mahojiano kwa njia ya televisheni.

Ley alimwambia kwamba hana mabilioni ya kumpatia lakini kama wakifanya kazi pamoja hatajuta kamwe.

M’bilia alitumia mwanya huo akajiunga na bendi ya Afrisa Internationale na ukizingatia sauti yake nyororo, uchezaji wake kupitia maungo yake yaliyojengeka kipekee, kwa kipindi kifupi M’bilia akawa gumzo katika jiji la Kinshasa. Juhudi zake hizo zilipelekea bendi hiyo kuongeza mapato kwa mauzo ya rekodi zao. 

Yaelezwa kwamba M’bilia Bell na Tabu Ley Rochereau walifunga ndoa kabambe ya kifahari wakiwa ndani ya ndege hewani. Katika maisha yao ya  ndoa walifanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike aitwaye Melodie Tabu, ambaye anasoma katika jiji la Paris na kufanya muziki na Baba yake.

M’bilia Bell anamuelezea Binti yake huyo kwamba anaongea kwa ufasaha lugha ya kiingereza, na kwamba ni mwimbaji mzuri aliyefuata nyayo za  wazazi wake na tayari amemshirikisha katika kuimba kwenye album yake mpya ya Belissimo.

Mwaka 1982 Bell alitoka na kibao  chake kiitwacho Mpeve  ya Longo, kikisimulia kisa cha mwanamke aliyetelekezwa na mumewe na kuachiwa watoto awalee peke yake. Kibao ambacho kiligusa hisia na kuwa simulizi kila kona za miji ya nchi hiyo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (zamani Zaire).

M’bilia aliipenda nchi ya Kenya, alipokuwa katika jiji la Nairobi alilazimika kujifunza lugha ya Kiswahili na kuweza kuimba nyimbo kadhaa kwa lugha hiyo.

Nyimbo zilizompatia chati M’bilia zalikuwa za  Nakei Nairobi, Boya ye,  Yamba ngay, Amour sans frantiere na   Biu Mondo.
Mbilia aliimba nyimbo nyingine zaidi za  Beyanga, Befosami, Faux Pas,Cadence Mudanda, Motema na Napika. Nyimbo za Kuteleza si kuanguka,  Faux  Pas, Iyolela, Bafosami na  Frontiere,. Zingine zilikuwa zaPhenomene, Manzil manzil, Mbanda na Nga, Nadina, Mayaval, Eswii yo Wapi, Biu Mondo, Nelson Mandela,Wende na Wende  na nyingine zasizokuwa na idadi zilimjengea heshima Mbilia Bell.

Karibia nyimbo zote alizoimba mwana mama huyo Bell akishirikiana na Rochereau hazichuji wala kukinai kuziangalia runingani au kuzisikiliza redioni, hadi leo.

Mbilia Bell aliwahi kuja hapa Tanzania akifuatana na mumewe  Tabu Ley Rochereau  na kundi zima la  Afrisa Internationale Bell alifanya kufuru katika maonyesho yao yote waloyoandaliwa hapa nchini.
Akiwa katika jiji la Dar es Salaam Bell aliweza kulitawala jukwaa mwanzo mwisho akitumia kuyachezesha  maungo yake sanjari na uzuri wake, akawa kivutio kikubwa.

Tabu Ley baadaye alimuongeza mwimbaji mwingine wa kike ‘Faya Tess’ ambaye jina lake halisi ni Kishila Ngoyi,  akiwa na nia ya  kuijenga vyema bendi yake. Lakini ujio wa Faya Tess ulimfanya  M’bilia  kuamua kuiacha Afrisa Internationale na kuondoka  kwenda jiji la Paris ambako alikutana na mwanamuziki wa sokous, mpiga gita Ringo ‘Star’ Bamundele mwaka 1983.

Sababu kubwa za kuondoka kwake ni kile kilichoelezwa kuwa wivu wa kimapenzi baina ya wana ndoa hao ulioingilliwa na Faya Tess.


Mbilia Bell aliwahi kuishi nchini Gabon,  ambayo inapakana na nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alikataa kuolewa na Waziri mmoja katika serikali ya nchi hiyo aliyempa sharti la kuacha muziki ili amuoe.

Anafurahia mafanikio yake na kujivunia kuwa yeye ni mmoja wa kati ya wanafunzi wa Rochereau  Tabu Ley ambaye alikuwa akimpa kipaumbele na kuwa mwanafunzi bora katika shule yake.

Marikirala Mboyo  M’bilia anasema haikuwa kazi rahisi kukubalika kuwa mwanamuziki mwanamke wa kimataifa katika maisha yake yote ya kazi za muziki. Watu wengi  hawakuwa wakimuamini na kuichukulia kazi yake kwamba haitakuwa endelevu.

Bell alikaririwa akisema kama wao wanawake wanawaamini waume zao na wala hawawalazimishi kuacha kazi zao, iweje wanaume wamfikirie yeye kila anapotikisa maungo yake kwamba huwa anawavutia?
Alitoa wito kwa wanawake wenzake kuungana na kufanya wanaume wawaone kwamba wao hawajirahisishi kama wanavyofikiria.

Marikirala Mboyo ‘M’bilia’ akiwa na muda wa ziada huutumia kufanya shghuli za kijamii zakiwa zile za kuwatembelea watoto wa mitaani, kurekebisha vituo vya watoto hao na kugawa msaada wa vyakula na nguo.

Mwana mama huyo kwa kawaida huamka kila siku saa 12:00 asuhuhi na kufanya maombi baadaye  huenda kwenye mazoenzi ya viungo. Anatoa siri ya kutochakaa mapema ni kuishi ukiwa na afya njema, wala si kwa kula nyama na kunywa pombe.

Ratiba yake ya asubuhi ni glasi moja ya maziwa isiyokuwa na mafuta, na glasi nyingine maji huwa ndiyo kifungua kinywa chake. Baada ya hapo hutumia muda mwingi katika kuandika nyimbo zake na kuangalia sinema katika televisheni.

Mbilia anasisitiza kwamba kazi ya muziki ni ya siku nzima na ni gumu sana hawezi kupata muda wa kutafuta kazi nyingine kwa kuwa hafikirii kuwa tajiri ila ameridhika na hali aliyonayo.

Bell ana mpango wa kuwahamsisha wanamuziki wa kike wa Afrika kuungana na wanamuziki wengine kulilia amani.

Mwisho.

No comments: