Tuesday, February 26, 2013

ALFA NA OMEGA YA MAQUIS


ALFA  NA  OMEGA  YA  MAQUIS

March , 2013

MAQUIS du ZAIRE ni bendi ambayo ‘iliyowatesa’ Watanzania kwa kuwaporomoshea burudani za  muziki wa dansi maridhawa katika kumbi mbalimbali hapa nchini.

Kwa wale waliokuwa vijana kati ya miaka ya 1970 na 1990, kamwe hawawezi kuisahau bendi hiyo ambayo iliingia hapa nchini kwa kishindo kikubwa ikitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Zaire) wakati huo.

Mwaka 1981 niliwahi kufanya mahojiano maalumu na mmoja wa viongozi wa bendi hiyo, Chimbwiza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye alinipa wasifu wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire.

Wasifu huo niliuandika na kuchapishwa katika gazeti la serikali la Nchi Yetu la kila mwezi, ambalo lilikuwa likuzwa kwa senti 30, likitolewa na Idara ya habari (MAELEZO).
Hivyo basi  si vibaya nikarejea kuwapasha wale ambao hawaifahamu bendi hiyo na kwa waliosahau, niwakumbushe  kwa kuwapa wasifu wa bendi ya Maquis du Zaire tangia ilivyoanzishwa hadi kutoweka kwake  katika taswira ya muziki.

Historia ya bendi hiyo inaanzia mwaka 1960 kwa vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Zaire), walioungana na kuunda bendi yao wakaiita Super Theo.

Bendi hiyo ilitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki  wa Kamina  na vitongoji vinavyouzunguka mji huo, baadaye wakaibadilisha jina kuwa  Super Gabby.

Katika kile kilichoelezwa na uongozi wa Super Gabby kuwa ni kuleta mageuzi katika muziki, bendi hiyo mwaka 1972, ilibadili jina tena na kuitwa Maquis du Zaire.

Bendi hiyo ya Maquis du Zaire iliingia hapa Tanzania mwaka huohuo wa 1972, kwa mwaliko wa mfanyabishara maarufu Mzee Batengas. Walianza kutumbuiza kwa mkataba katika ukumbi wa Mikumi Tours uliokuwa maeneo la Tazara,  Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Baada ya  kumaliza mkataba wao waliachana na Mzee Batengas,  wakaenda kupiga muziki katika Klabu ya Hunters kwa  kipindi kifupi. Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima aliyekuwa akimiliki wa  ukumbi wa Safari Resort  maeneo ya Kimara.

Mnamo mwaka 1977 Maquis du Zaire waliamua kuongeza nguvu kwa  kuimarisha kikosi chao. Hivyo uongozi huo ulimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee Paul’ kwenda Congo kutafuta wanamuziki wengine wapya.

‘Mzee Paul’ alibahatika kuwachukuwa akina Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Nkashama Kanku Kelly, Ilunga  Banza ‘Mchafu’, Mutombo Sozy na  mnenguaji  mahiri,  Ngalula  Tshiandanda. Wakati huo walikuwa wakipiga na kucheza katika mtindo wa ‘Chakula Kapombe’ ambao kwa watanzania ulikuwa mpya na ukapendwa mno na mashabiki.

Kufika kwa wanamuziki hao yaelezwa kuwa  kulileta mabadiliko makubwa sana katika muziki husuan tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ambaye ndiye aliyeleta mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.

Maquis du Zaire ilikuwa  na wanamuziki wenye ubunifu kwa ajili ya kuboresha bendi yao. Waliazisha mtindo mwingine wa ‘Kamanyola’ mtindo uliowapagaisha  wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es  Salaam. Wakati huo ‘rapa’ wa bendi hiyo, Mwema Mudjanga
 ‘Mzee Chekecha’ alikuwa akiwahamasisha wapenzi wake kwa kutamka  “cheza Kamanyola… Kamanyola bila jasho… cheza ukijidai…”

‘Mwenye bahati habahatishi’ usemi huo ulijodhhirisha mwaka wa 1977 mwishoni, ambapo bendi ya   Maquis du Zaire ilipoangukiwa na bahati nyingine tena. Walisaini  mkataba mwingine na  Mzee Makao aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah,  maeneo ya Ubungo.Baada ya kumaliza mkataba na mfanayabiashara Hugo Kisima

 ilimaliza mkataba na kuondoka kwa Hugo Kisima. Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya  Sanifu na Ogelea piga mbizi, haikuchukua kipindi kirefu ukumbi huo ukabadilishwa jina na kuitwa White House. Ikumbukwe kwamba  wakati huohuo Maquis pia ilikuwa ikipiga  muziki kwenye ukumbi wa Mpakani, maeneo ya Mwenge. Ukumbi wa  Mpakani  baadaye ulibadilishwa jina kuwa   Silent Inn.  Kisha kuishia kuwa Kanisa.

Mwishoni mwaka 1978 waliamua kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka Congo ambao ni akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na  Khatibu Iteyi Iteyi.


Maquis du Zaire ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.

Chini  ya uongozi huo miaka ya 1980 mafanikio makubwa yalionekana. Mojawapo ni lile la kuanzisha Orchestra Maquis Company (OMACO). Kampuni hiyo ilikuwa ikimiliki shamba la matunda, wakilima kwa kutumia matreka yao maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mazao yao walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko  Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

OMACO pia  ilimiliki mradi mwingine wa viwanja  tisa na nyumba kadhaa maeneo ya Sinza na pia waliwahi kuingia mkataba wa kuitangaza kampuni ya magari makubwa ya SCANIA.

Vijana wa wakati huo watakumbuka jinsi ukumbi wa White House ulivyokuwa ukifurika watu kila siku za Jumamosi, kuwashuhudia vijana wa Maquis du Zaire waliokuwa watanashati na nidhamu ya hali ya juu wakiwa jukwaani wakifanya vitu vyao.

Enzi hizo ilikuwa ukiingia katika ukumbi wa White House, mbele yako macho lazima yakutane na mbao zilizo nakshiwa kwa kuandikwa  majina ya wanamuziki wote na kukomelewa juu ya mwembe uliokuwa katikati ya ukumbi huo.

Maquis du Zaire ambayo ilikuwa ikipiga muziki mara moja kwa wiki, ilikuwa ikifika usiku wa manane, wanasisitisha muziki na kusikika kipaza sauti kikiuliza kama wapenzi wao kama wamekuja na miswaki?  Wapenzi walikuwa wakijibu ndiyooooo… Wanaelezwa dawa ya meno ipo hapo. Muziki ulikuwa unapigwa hadi alfajiri.

Bendi hiyo ikiwa hapa nchini ilikuwa ikipiga na kucheza katika  mitindo  mbalimbali kwa nyakati tofauti. Mitindo hiyo ilikuwa ya Chakula Kapombe, Kamanyola, Bishe Bishe, Zembwela, Chekecha na Ogelea Piga mbizi.

Mwema Mudjanga ‘ Mzee Chekecha’ ndiye aliyekuwa akinogesha zaidi mitindo hiyo. Alikuwa kivutio kikubwa ukumbini licha ya kazi yake ya  kupuliza tarumbeta, alikuwa ‘rapa’ aliyeweza kuwainua vitini wapenzi kwenda kucheza, akitumia  vibwagizo vya ‘Chekeee….  Chekechaaa’  ‘Tusangalaa’, ‘aima imaa’,  ‘Bishe bishee’, ‘cheza Kamanyolaa’, ‘cheza kwa maringo’, ‘ Cheza  ukijidai’ ‘  Sanifuu Saa... Sanifu, Ongeleaa piga mbizi … na mengine mengi.

Maquis du Zaire wakati huo  ilikuwa imesheheni wanamuziki zaidi ya 40 wenye vipaji vinavyopishana. Kwa idadi hiyo, laiti kama wangelikuwa na tamaa, wangeliweza kupiga muziki katika kumbi tatu tofauti kwa wakati mmoja.

Nina uhakika kwamba msomaji wangu unashauku ya  kujua au kukumbushwa kikosi kamili kilichokuwa kinatengeneza Maquis du Zaire wakati huo. Nikianza na safu ya waimbaji walikuwepo akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, mapacha Kassalo Kyanga na  Kyanga Songa.
Wengine walikuwa  Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mbomboka, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Tshimanga Kalala Assosa, Kabeya Badu, Masiya Radi ‘Dikuba kuba’,  Issa Nundu na Tabia Mwanjelwa, Rahma Shaari na Anna Mwaole.

Wapiga gita  la solo alikuwepo  Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye kwa umahiri wake wa kulicharanza gita hilo, wapenzi walimpachika cheo cha juu kabisa jeshini cha   ‘Field Marshal’.
Wengine katika gitaa hilo  waalikuwa akina Ilunga Lubaba, Dekula Kahanga ‘Vumbi’ na Mbwana Suleiman ‘Mbwana Cox’.

Gitaa la rhythm walikuwepo Mulenga Kalonji ‘Vata’, Omari Makuka na Steven Kaingilila Mauffi. Bila kuwashau akina Mbambu Kazadi, Mondo Mondonde na  Nawayi Kabwila.

Gitaa  zito la besi lilikuwa likiungurumishwa na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’ ambaye alijizolea umaarufu mkubwa kwa kulicharaza gita hilo  akiwa kajitwisha kwenye upara kichwani kwake. Wengine walikuwa Ibrahimu na Mujos wa Bayeke.

Kama nilivyokujuza hapo awali kwamba bendi hiyo ilikuwa imejaza mseto wa vipaji mbalimbali. Kwa upande wa wapuliza Saxophone ‘mdomo ya bata’ walikuwepo akina Mafumu Bilali ‘Bombenga/‘Super Sax’,  Khatibu Iteyi Iteyi,  Alex Kanyimbo,  Kalamazoo, Akulyake Suleimani ‘King Mallu’, Roy Mukuna ‘Mukuna wa Mukuna’, Chibangu Katayi , Comson Mkomwa na  Majengo Selemani.

Wapuliza tarumbeta walikuwepo akina Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ Nkashama Kanku Kelly,  Mioma wa Mwamba ‘Mzee Tito’, Kayembe Ndalabuu ‘Trumbloo’  Mpoyo Kalenga, Berry Kankonde,  Kaumba Kalemba,  Ngoi Mubenga, Ilunga Ngoi ‘Bizos’, Morgan Machege na Ngenda Kalonga.
Vijana hao kwa pamoja walikuwa wakitoa burudani maridadi  wakiwa wamejitwisha tarumbeta zao vichwani wakilishambulia jukwaa, huku wakicheza kwa staili za aina yake ukumbini.

Madoido na mbwembwe hizo, ziliwavutia  wapenzi wengi na kupenda kuhamishia viti vyao wakisogea  sehemu iliyokuwa karibu, ili kushuhudia vijana hao wakifanya maajabu ya kuchezea vyombo hivyo.

Mbonyezaji  wa Kinada alikuwa Mbuya Makonga ‘Adios’ huku Mutombo Sozzy  akizicharaza drums akisaidiana na  Matei Joseph.  Tumba zilikuwa zikigongwa na Siddy Morris ‘Super Konga’ na Pulukulu Wabandoki Motto.

Walikuwepo na wanenguaji  mahiri  ambao walikuwa wakitoa burudani za pekee wakati huo akina ‘Washa Washa’, Dulla ‘Panga Panga’, Wandema Rashidi, Anna Mganga, Kinacho, Mwajuma, Frida Shirima,  Zuwena na  Ngalula Tshiandanda, wakiongozwa na Nkulu Wabangoi.

Ikiwa White House bendi hiyo ilitoka na vibao vingi vikiwemo vya Double double, Clara, Kyembe, Maiga, Mpenzi Luta, Mwana yoka ya Babote, Ngalula, Nasononeka, Nimepigwa ngwala, Promotion, Ngalula, Karubandika na Noelle Bonane wimbo ambao ulikuwa ukipigwa mahsusi nyakati za Krimasi na mwaka mpya.

Zingine zilikuwa Dora mtoto wa Dodoma, Balimwacha, Malokelee, Promotion, Seya, Sophia, Sumu ya mapenzi, Sababu ya nini, Zowa, Uba, Safari ya Mbeya, Wakati nikiwa mdogo na nyingine nyingi zisizo idadi.
Kuna msemo usemao “Cha kuazima hakistiri maungo”  msemo huo uliisibu bendi ya  Maquis du Zaire baada ya kiungia katika maelewano ‘hafifu’ na mwenye ukumbi, hadi kulazimika kuondoka wakiacha ukumbi huo ukibadilishwa kuwa Gereji hadi leo.

Baadaye bendi hiyo ikabadilishwa jina na kuwa Maquis Original wakipiga katika kumbi za Wapiwapi’s pale maduka mawili, Chang’ombe na CCM Kata ya 14 Temeke, kabla ya kuhamia ukumbi mpya kwa wakati huo wa Lang’ata pale  Kinondoni.

Maquis Original ilileta wanamuziki  wengine toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo muda mfupi kabla ya mpiga gitaa la solo, Dekula Kahanga ‘Vumbi’ kuondoka kwenda Stockholm nchini Sweden.

Wanamuziki hao walikuwa Kivugutu Motona Chatcho (Solo), na waimbaji Freditto Butamu na Luhembwe Mwahitwa ‘Bobo Sukari’.

Walitikisa ukumbi wa Lang’ata  kwa nyimbo zao kali za Mangolibo, Mayanga,  Kisebengo, Makumbele, zikisindikizwa na wimbo wa Ngalula ambao mwimbaji Thsimanga Kalala Assosa alikuwa akitoa kibwagizo wakati wa chorus akiita “ Vumbiii Vumbiii  Vumbiii. Nyimbo zote zilipigwa na kutamba kwa mitindo ya  ‘Washawasha’ na ‘Sendema’.

Maquis Original ikiwa Lang’ata, kuna shabiki mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Magoma moto’  ambaye  alikuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa Maquis, kwa kuonyesha uhodari wa kucheza ‘Sendema’  akiwa kajitwisha chupa ya Bia juu ya kichwa chake.

Ikumbukwe kwamba idadi kubwa mno miongoni mwa wanamuziki wanaotajwa humu, wameshatangulia mbele za haki.
Wengine ni wagonjwa akina Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mmbombo wa Mmboka na Mutombo Lufungula ‘Audax’

 Mungu aziweke roho zao pahala pema peponi waliotangulia na awape tahfifu wanaoumwa, Amen.




MWIMBAJI WA MAQUIS DU ZAIRE KASONGO MPINDA 'CLAYTON' NA MPIGA GITA LA KATI MULENGA KAONJI 'VATA'
MPIGA GITA LA SOLO CHIMBWIZA MBANGU NGUZA 'VICKING' AKIWA NA KASONGO MPIDA 'CLAYTON' NYUMA.
 MUTOMBO LUGUNGULA 'AUDAX'(kushoto) NA KASONGO MPINDA
 KASONGO MPINDA (katikati) NA MAPACHA KYANGA SONGA NA KASALO KYANGA.
 NKASHAMA KANKU KELYY AKIPULIZA TARUMBETA.
 CHINYAMA CHIYAZA AKIYARUDI KATIKA STAILI YA CHAKULA KAPOMBE.
 ILUNGA BANZA ' MCHAFU' (kushot) NA DEKULA KAHANGA WAKIYACHARAZA MAGITA.
 BAADHI YA WANAMUZIKI WA MAQUIS DU ZAIRE TOKA KUSHOTO, SULEIMA MBWANA 'COX', MBUYA MAKONGA 'ADIOS', MUJOS WA BAYEKE, KSTEVEN KAINGILILA MAUFFI, DEKELA KAHANGA 'VUMBI' ISSA NUNDU MUKUMBULE LOLEMBO 'PARASHI' NA ROY MUKUNA.
 MPIGA TUMBA WA MAQUIS DU ZAIRE SIDY MORRIS AKIZIDUNDATUMBA KWA STAILI YA AINA YAKE.

No comments: