Wednesday, August 7, 2013

KABEYA ‘NYOTA’ ILIYOZIMIKA GHAFLA.



KABEYA  ‘NYOTA’ ILIYOZIMIKA GHAFLA.

NA  MOSHY  KIYUNGI.

MARCH 2013.

KABEYA BADU ALIKUWA MWIMBAJI MAHIRI KATIKA BENDI YA LA CAPITALE, ALIYEWAACHA  WAPENZI NA MASHABIKI WA MUZIKI WA DANSI HAPA NCHINI, WAKIWA BADO WANAMHITAJI.

ALIAGA DUNIA TAREHE 06 MARCH, 2013 AKIWA KATIKA HOSPITALI WA MUHIMBILI ALIKOKUWA AMELAZWA KWA MARADHI YA FIGO, AKIWA AMEFIKISHA UMRI WA MIAKA 68.

MPAKA ALIPOFIKWA NA UMAUTI, ALIKUWA NI MWANAMUZIKI MWENYE VIPAJI VYA KUTUNGA NA KUIMBA KATIKA BENDI YA LA CAPITALE ‘WAZEE SUGU’ INAYOONGOZWA NA MKONGWE KIKUMBI MWANZA MPANGO ‘KING KIKI’.


MSIMBA WA KABEYA ULIWATIA SIMANZI NA MAJONZI MAKUBWA WAOMBOLEZAJI WALIOFIKA KATIKA HOSPITALI YA MUHIMBILI KUUAGA MWILI WAKE NA KATIKA MAZISHI YALIYOFANYIKA KATIKA MAKABURI YA KINONDONI MARCHI 07, 2013. UMATI WA WATU WALIBUBUJIKWA MACHOZI MARA WALIPOONA MWILI WAKE UKISHUSHWA KABURINI.

KABEYA BADU TOKA ALIPOANZA SAFARI YAKE KATIKA MUZIKI, KAMWE HAKUWA MTU MWENYE SONI. ALIKUWA TAYARI KUIACHA BENDI NA KWENDA NYINGINE WAKATI WOWOTE ULE, ILI MRADI MASLAHI YAWE MAZURI. BADU ALIPITIA BENDI NYINGI AKIWA HUKO KWAO JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO, NA HAPA TANZANIA, AMBAPO  ALIPIGIA KATIKA BENDI SI CHINI YA TANO TOFAUTI.

SI VYEMA KUMSIFIA MTU BAADA YA KUFA, LAKINI KWA KABEYA NINALAZIMIKA KUFANYA HIVYO KWA KUWA MWISHONI MWA MWAKA JANA 2012, NILIBAHATIKA KUPATA FURSA YA KUFANYA MAHOJIANO NAYE ILI KUJUA WASIFU WAKE.

NILIZUNGUMZA NA KABEYA BADU  KWA TAKRIBANI SAA MBILI MFULULIZO, AKINISIMULIA HISTORIA YA MAISHA YAKE KWA UJUMLA.

KABEYA ALIAZA KWA KUTAJA  MAJINA YAKE  AKISEMA ANAITWA KABEYA CHIBANGU BADU. ALIZALIWA JANUARI 22, 1945 KATIKA MJI WA  LIKASI, HUKO JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO.
ELIMU YA MSINGI ALIPATA KATIKA SHULE YA ECOLE  OFFICIALLE LAIQUE DE KOLWEZI NA KUMALIZA MWAKA 1959.

KABEYA ALISEMA MUZIKI ALIANZA TANGU AKIWA BADO MDOGO NA ALIPOPATA UMRI WA KWENDA KANISANI, ALIJIUNGA KATIKA KWAYA AKIIMBA NYIMBO INJILI.

AKIWA KANISANI HUMO, ALIJIFUNZA JINSI YA KUTENGENEZA ‘MELODY’ BAADAYE MWAKA 1963,  AKAJIAMINI KWAMBA ANAWEZA KUFANYA MUZIKI. ALIKWENDA KUJIUNGA NA BENDI YA MUZIKI WA DANSI YA  RICCO JAZZ, ILIYOKUWA KATIKA WILAYA YA KOLWEZI.

AKIWA KOLWEZI,  KABEYA ALIJIUNGA NA CHUO CHA UFUNDI AMBAKO ALICHUKUA MASOMO YA USEREMALA NA UASHI.
“TANGU  NIKIWA MDOGO, NILIPENDA SANA NYIMBO NA UIMBAJI WA TABU LEY ROCHEREAU NA KABASELE YAMPANYA ‘PEPE KALE’ NIKATAMANI SIKU MOJA NIFIKIE HADHI YAO…” ANASEMA KABEYA.

FAMILIYA YAKE ILIJITAHIDI KUMPA MOYO ILI AWEZE KUFANYA VIZURI KATIKA MUZIKI, HIVYO ILIMSHAURI KABEYA KUJIFUNZA LUGHA YA KIFARANSA AMBAYO INAZUNGUMZWA NCHINI MWAO.

KABEYA ALIKUBALIANA NA  USHAURI HUO NA ALINGIA KATIKA CHUO KILICHOKUWA KIKIMILIKIWA NA DHEHEBU LA DINI YA PROTESTANT HUKO KANANGA, JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO.

KIU CHA KABEYA KILIPOZWA PALE ALIPOPOKEA CHETI BAADA YA KUFUZU SOMO HILO LA KIFARANSA.
HARAKATI ZA KABEYA BADU ZA KUTAFUTA MAISHA ZILIMFIKISHA KUFANYA KAZI KATIKA GAZETI MOJA LA LEALITY CONGOLESE LA  MJINI KANANGA, KWENYE KITENGO CHA USAMBAZAJI MWAKA 1967.

“BAADA YA MIAKA MIWILI KUPITA, MMILIKI WA GAZETI HILO ALIKAMATWA BAADA YA GAZETI HILO KUANDIKA HABARI ZILIZO MUUDHI RAIS WA WAKATI HUO MOBUTU SESESEKO, HATIMA YAKE GAZETI LIKAFUNGIWA, TUKAKOSA KAZI….” ANAELEZA KABEYA BADU.

‘KUVUNJIKA KWA KOLEO SI MWISHO WA UJENZI’ MSEMO HUU ALIUFANYIA KAZI KABEYA AMBAYE MWAKA HUO HUO ALIANZA SAFARI YAKE YA MUZIKI KIKAMILIFU. AKAJIUNGA KATIKA BENDI YA LUPE  JAZZ, BAADAYE AKAENDA KATIKA BENDI NYINGINE YA AMIDE SUCCESS.

KABEYA HAKUISHIA HAPO KWANI ALIONDOKA TENA NA KWENDA KUJIUNGA NA BENDI YA SANTA FEE BAADAYE AKAJIUNGA KATIKA BENDI YA LUPINA NATIONALE, AMBAKO ALIKUTANA NA KASONGO MPINDA ‘CLAYTON’ HUKO KANANGA.

UTULIVU KATIKA BENDI KWAKE HAUKUWEPO KABISA,  KWANI ALIONDOKA TENA NA KWENDA KUJIUNGA KATIKA BENDI YA LUPE REVOLUTION, ILIYOKUWA YA VIJANA KAMA YEYE.
JINA NA SIFA ZA UIMBAJI WAKE ZIKAZAGAA NDIPO ALIPOCHUKULIWA NA  OMER BABA GASTON KATIKA BENDI YAKE YA  BABA NATIONALE  MWEZI SEPTEMBA 1968.

BAADAYE MWAKA 1970, KABEYA ALISHAWISHIKA KWENDA KUTAFUTA AJIRA KATIKA MJI WA KINSHASA. ALIBAHATIKA KUPATA AJIRA KATIKA BENDI AMBAYO BAADAYE AKAGUNDUA KWAMBA  ILIMPA AHADI ZA UONGO ZA MASLAHI, NAYE AKAACHANA NAYO.
KATI YA  MWAKA 1971 NA 1972 KABEYA BADU ALIPIGA MUZIKI KATIKA BENDI YA FESTIVAL DU ZAIRE KATIKA JIJI LA KINSHASA, JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO.

KABEYA ALIRUDI LIKASI MWAKA HUOHUO WA 1972 NA KUJIUNGA NA BENDI YA SAFARI NKOI BAADA YA KUITWA NA MWANAMUZIKI KIKUMBI MWANZA MPANGO ‘KING KIKI’. KATIKA BENDI HIYO PIA  ILIKUWA NA WANAMUZIKI WENGINE MAGWIJI NDALA KASHEBA NA BAZIANO BWETII.
KABEYA BADU NASEMA KWAMBA ALISOMA  DARASA MOJA NA KIKUMBI MWANZA MPANGO ‘KING KIKI’ KATIKA SHULE YA MSINGI YA SHULE YA  ECOLE  OFFICIALLE LAIQUE DE KOLWEZI, AMBAKO WALIMALIZA MASOMO YAO MWAKA 1959.
“TANGU TUKIWA VIJANA TULIKUWA TUKIELEWANA SANA NA KIKI, NDIYO SABABU NIMEKUWA NAYE SAMBAMBA TUKIENDA SEHEMU MBALIMBALI HADI LEO NINAYE…” ANSEMA KABEYA.
WALIPOKUWA KOLWEZI WAKIPIGA MUZIKI KATIKA BENDI YA SAFARI NKOI, WALIKUWA WAMEPANGA NYUMBA MOJA, WALICHANGIA BAJETI YA CHAKULA KWA PAMOJA KILA MWISHO WA MWEZI.

MWAKA 1973 UONGOZI WA  SAFARI NKOI ULIANZA KUWAFANYIA ‘MTIMANYONGO’ WANAMUZIKI WAKE AKIWEMO ‘KING KIKI’ LAKINI  KIKI  ALIGUNDUA MAPEMA HALI HIYO, AKAMSHAWISHI KABEYA MWAKA HUOHUO WA 1973, KUONDOKA NA KWENDA KUANZISHA BENDI YAO.

‘MWENYE BAHATI HABAHATISHI’ MSEMO HUO ULIJIONESHA DHAHIRI KWANI KABLA HAWAJAAZISHA BENDI YAO, AKAJITOKEZA  TAJIRI MMOJA ALIYEJULIKANA KWA JINA LA PARADIZO, AKIMTAKA KIKI KWENDA LUBUMBASHI KUANZISHA BENDI YAKE.
“KIKI HAKUNIACHA MWAKA 1974 TUKAENDA LUBUMBASHI KUUNDA BENDI YA TAJIRI HUYO YA BUKA BUKA MABELE. NI UKIRITIMBA WA TAJIRI YETU, ULISABABISHA BENDI HIYO KUFA BAADA YA MIEZI SITA…” ANAELEZEA MWANAMUZIKI HUYO.

KABEYA AKAONGEZA AKISEMA BAADA YA KUFA KWA BENDI YA BUKA BUKA MABELE, KIKI MWAKA 1974 MWISHONI ALIAMUA KWENDA MJI MKUU WA CONGO DRC WA KINSHASA LAKINI KABLA HAJAONDOKA, ALIWASHAWISHI YEYE NA WANAMUZIKI WENZAKE WAREJEE SAFARI NKOI.

WALIKUBALI USHAURI HOU NAO WAKAREJEA NA WAKAPOKELEWA  NA UONGOZI WA SAFARI NKOI KWA MARA NYINGINE TENA. KWA KIPINDI HICHO AKIWA SAFARI NKOI, KABEYA AKAWA NA MAWASILIANO YA KARIBU NA KIKI AKIMSHAWISHI KURUDI SAFARI NKOI KWA HALI YA UTULIVU KATIKA BENDI ILIKUWA NI IMEIMARIKA.

KING KIKI ALIREJEA LUBUMBASHI MWAKA 1976, AKITOKEA KINSHASA PASIPO KUMAFAMAMISHA  MTU YEYOTE.
KABEYA ANASEMA “ TULIKUWA TUNAPIGA MUZIKI KATIKA UKUMBI MMOJA WA RELE NIGHT CLUB   MJINI LUBUMBASHI,  GHAFLA KIKI AKAPANDA JUKWAANI NA KUSHIKA ‘MIC’ AKAANZA KUIMBA. SOTE TUKABUTWAIKA  TUKAONA KAMA VILE ‘SHETANI’ ALIYETUA KIMIUJIZA JUKWAANI”


MWAKA 1977  KIKUMBI MWANZA MPANGO ALIFUATWA NA  CHIBANGU KATAYI ‘ MZEE PAUL’ ALIYETOKEA MAQUIS DU ZAIRE ILIYOKUWA HAPA NCHINI. KIKI ALIMUULIZA MZEE PAUL  IWAPO WANAMUZIKI WALIOPO MAQUIS DU ZAIRE WANAKIDHI  VIWANGO? MZEE  PAUL ALIJIBU KWA WASIWASI NA KUPENDEKEZA BORA KUCHUKUA  WANAMUZIKI HUKO DRC. KIKI ALIPENDEKEZA WANAMUZIKI WA KUONDOKA NAYE KUJA TANZANIA  AKIWEMO  KANKU KELLY, MUTOMBO SOZY, ILUNGA BANZA ‘MCHAFU’ WAKIWA SAFARINI KUJA NCHINI WALIPITIA  MJI WA KAMINA AMBAKO WALIMPATA MNENGUAJI  MWANADADA NGALULA TSHIANDANDA  ALIYEKUWA AKINENGUA KATIKA BENDI YA SAKAYONSA YA MJINI HUMO.

KABEYA BADU ALIKUWA AKIWASILIANA  NA KING KIKI NA AKAMUAHIDI KWAMBA ATAJITAHIDI AJE TANZANIA.


AHADI YA KIKI KWA KABEYA IKATIMIA BAADA YA KUFIKA MAQUIS DU ZAIRE. SAFU YA UIMBAJI IKAONEKANA KUPWAYA. ALIPENDEKEZA KUONGEZWA KWA WANAMUZIKI ZAIDI ILI KUIMARISHA BENDI HIYO YA MAQUIS  DU ZAIRE.  CHIBANGU KATAYI ‘ MZEE PAUL’ KWA MARA NYINGINE TENA AKATUMWA KWENDA CONGO  KUWALETA WANAMUZIKI WALIOPENDEKEZWA NA KIKI.
“ TULICHUKULIWA MIMI  KABEYA BADU NA KALALA  MBWEBWE  TUKIWA NI  WATUNZI NA WAIMBAJI,  MONGA KIYOMBO  ALIYEKUWA NA UWEZO WA KUPIGA  GITA LA RHYTHM NA  SAXOPHONE. WENGINE WALIOCHUKULIWA NI KINA  NGOI MUBENGA KWA UPANDE WA TARUMBETA NA KHATIBU ITEYI ITEYI ALIYEKUWA MPULIZJI WA SAXOPHONE  TUKALETWA TANZANIA MWAKA 1978…” NATAMKA KABEYA.

KABEYA ANASEMA MARA ALIPOTUA MAQUIS DU ZAIRE, ALITUNGA NA KUIMBA NYIMBO NYINGI, BAADHI YAKE NI ‘NDOA YA KWANGU NA MAMA KAZI’, ‘PONDAMALI’, ‘KIBWE MUTOMBO’ NA ZINGINE ZA MUNTANDA MULI, LWEMBE NA MANENO, AMBAZO  HAZIKUWAHI KUREKODIWA.

KABEYA BADU ALIPIGA NA MAQUIS DU ZAIRE KWA MIAKA MIWILI BAADAYE MWAKA 1980, ALICHOROPOKA NA KWENDA AKIJUNGA NA KING KIKI KATIKA BENDI YA ORCHESTRA SAFARI SOUND (OSS) ILIYOKUWA IKIMILIKIWA NA MFANYABIASHARA MAARUFU HUGO KISIMA.
AKIWA NA OSS KABEYA ALITUNGA NA KUIMBA NYIMBO ZA NANI ATASHIKA JEMBE NA POLE NDUGU. ANAELEZA KUWA WIMBO WA ‘YUYU’ ULIPIGWA NA KUREKODIWA KATIKA KIPINDI CHA KLABU RAHA LEO SHOW KILICHOKUWA KIKIRUSHWA NA RADIO TANZANIA DAR ES SALAAM. (RTD)

BADU ALIKUWA AKIHITAJIKA SANA KATIKA BENDI HIZO MBILI PINZANI WAKATI HUO ZA MAQUIS NA OSS. HIVYO  AKAWA MITHIRI  YA ‘MUIGIZAJI’ KWA KUHAMAHAMA. ALIREJEA TENA MAQUIS  KWA KIPINDI KIFUPI KISHA MWAKA 1986 AKATAKIWA KUREJEA KWA MARA NYINGINE TENA KATIKA BENDI YA ORCHESTRA SAFARI SOUND.

ALIPOREJEA OSS TAYARI BENDI ILIKUWA CHINI YA UONGOZI WA NDALA KASHEBA NA HAICHUKUA MUDA MREFU AKATOKA NA WIMBO ULIOWAPAGAISHA WAPENZI WA OSS WA ZIADA. WIMBO HUO ALIUIMBA PEKE YAKE KWA HISIA KALI AKIMLILIA ZIADA, NA UKAMUONGEZEA SIFA KUBWA MIONGONI MWA WAIMBAJI WA MUZIKI WA DANSI HAPA NCHINI.
ZINGINE ZILIKUWA ZA ‘ KURUTHUMU’, ‘SIMBA WALA WATU WAMEVAMIA MJI’ MAMA MWITA,  KAYANDA NA NYINGINE NYINGI.
KABEYA BADU ANAMWELEZEA KIKUMBI MWANZA MPANGO ‘KING KIKI’ KUWA NDIYE ANAYEJUA UMUHIMU WAKE NA HAPA ANASEMA… “ KIKI NDIYE ALIYEKUWA AKIJUA UMUHIMU WANGU KATIKA MUZIKI TOKA MWANZO HADI AKANIPACHIKA  JINA LA ‘ CHANGA CHA MKONYOYO’ IKIWA NA MAANA YA SIRI ILIYOFICHIKA…” ALIPEWA JINA HILO BAADA YA KUFYATUA WIMBO WA CHANGA CHA MKONYOYO’ ANAOULEZEA KUWA  NI UJUMBE MZITO JAPOKUWA WIMBO HUO  HAUKUWAHI KUREKODIWA.

ALIONDOKA OSS  NA KWENDA KUJIUNGA KWA MARA NYINGINE TENA NA MAQUIS DU ZAIRE  MWAKA 1988, HAPO NAPO HAKADUMU AKACHUKULIWA NA KWENDA KUJIUNGA NA BENDI YA TANCUT ALMASI ILIYOKUWA IKIPIGA MUZIKI WAKE MJINI IRINGA.

‘MSAHAU KWAO MTUMWA’ KABEYA ALITAMANI KUREJEA KWAO CONGO, NDIPO MWAKA 1990 AKAAMUA KURUDI KWAO LIKASI KATIKA JIMBO LA KATANGA.
KAMA NILIVYOKUJUZA MWANZONI KWAMBA KABEYA ALIKUWA MTAFUTAJI WA  MASLAHI MURUA, HIVYO ALIREJEA TENA TANZANIA  MWISHONI MWA MWAKA 1998.  MWAKA ULIOFUATIA WA 1999, AKAPEWA KAZI YA KUANZISHA BENDI YA MAGOMA SOUND YA JIJINI DAR ES SALAAM.

MWAKA 2001 ALIJIUNGA KATIKA BENDI YA LA CAPITALE INAYOONGOZWA NA KIKUMBI MWANZA MAPANGO ‘KING KIKI’ AU ‘BWANA MUKUBWA’ HADI MAUTI YAKE YALIPOMFIKA JUMATANO ILIYOPITA YA TAREHE 06 MACHI, 2013.


KABEYA ALISEMA KWAMBA ANA  MATARAJIO MAKUBWA ANAYOTAMANI KUFIKIA.   “NINA MPANGO WA KUNUNUA VYOMBO VYANGU VYA MUZIKI, PIA NATARAJIA KUREKODI NYIMBO ZAGU ZOTE NILIZOTUNGA NA KUZIIMBA, NZIUZE  MIMI MWENYEWE…” ANASEMA KABEYA AKIWA MWINGI WA TABASAMU USONI.

NINASIKITIKA KWA KUSEMA KUWA KUMBE KAULI HIYO IKIFUATIWA NA TABASAMU HILO,   ILIKUWA LA NDIYO  MWISHO,  TUKIAGANA NAYE!

KABEYA BADU ALINISISITIZA KWAMBA  MARA TU MAKALA HII IKITOKA,  NIMUALIFU ILI  AWAHI KUNUNUA GAZETI HILI, LAKINI MPANGAJI WA YOTE NI MUNGU.

KIONGOZI WA BENDI YA LA CAPITALE, KIKUMBI MWANZA MPANGO KING  KIKI’  ALIMUELEZEA KUWA PENGO LA KABEYA KAMWE HALITAZIBIKA.  “ KABEYA  PENGO LAKE HALITAZIBIKA KAMWE  AMETUACHIA UKIWA USIO NA  KIFANI. ALIKUWA NI MTUNZI  NA MWIMBAJI MZURI SI HIVYO TU PIA ALIKUWA MSIKIVU, MTU WA KAZI TULISHAURIANA KUTENGENEZA ‘MELODY’NA KWA KWA USHIRIKIANO HUO TULIKUWA TUKICHOKOZANA NA KUTOA VIBAO ‘MATATA’ SANA. TUMEMPOTEZA KABEYA…” KWA MASIKITIKO NA MAJONZI ANASEMA KIKI.
KABEYA CHIBANGU  BADU, AMEACHA MJANE NA WATOTO WANANE KATI YAO WATANO NI WA KIKE.

WAPENZI NA WADAU WA MUZIKI WA DANSI HAPA NCHINI,  KAMWE HATAMSAHAU KABEYA BADU KWA JINSI ALIVYOKUWA  NA UWEZO WA KULISHAMBULIA JUKWA KWA KUCHEZA NA KUPAZA SUTI YAKE ILIYOKUWA NYORORO WAKATI AKIIMBA.

MUNGU AILAZE ROHO YAKE PAHALA PEMA PEPONI, AMINA.

MWANDISHI WA MAKALA HII ANAPATIKANA KWA NAMBA HIZI: 0784331200,  0767331200 na 0713331200.




No comments: