Monday, April 14, 2014

AHMED KIPANDE NA KILWA JAZZ



AHMED KIPANDE NA KILWA JAZZ.

AHMEDI  KIPANDE ni mwanamuziki nguli aliyeshiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa maendeleo na kupigani Uhuru wa Tanganyika akiwa na bendi yake ya Kilwa Jazz.

Kilwa Jazz ilishiriki kikamilifu siku Tanganyika inapata Uhuru Decemba 09, 1961 kwa kimba wimbo wa kusifia nchi yetu kupata Uhuru toka wa Wakoloni.

Chini ya uongozi wa Ahmedi Kipande,  Kilwa Jazz ilishiriki kikamilifu kutoa burudani wakati mikakati ya kufanya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye meneo ya makao makuu ya bendi hiyo jijini Dar es Salaam mwaka 1964.

Ahmedi Kipande na bendi yake waliteuliwa na serikali ya Tanganyika kwenda kushiriki sherehe za Uhuru wa nchi za Malawi na Uganda.

Historia ya mwanamuziki huyu iliyotolewa na mwanawe wa mwisho Kipande Ahmed, ameeleza kwamba jina kamili la  baba yake alikuwa ikiitwa Ahmed Mohammed Kipande,  aliyezaliwa mwaka 1937 huko Kilwa Kivinje mkoani Lindi.

Miaka michache baada ya kifo cha mama yake Ahmed Kipande alifuatana na Baba yake kuja Dar es Salaam na akaanza masomo katika shule ya Uhuru Wavulana ilikuwa maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam.

Katikati ya miaka ya 1950 Kipande alianza kupiga muziki akitumia ala iitwayo Violin, katika bendi ya Tanganyika Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Zimbe Kidosi. Bendi hiyo ilikuwa  na makao makuu yake katika mtaa wa New Street ambao hivi sasa unaitwa mtaa wa Lumumba.
Wanamuziki wa miaka hiyo walianzisha bendi wakizipa majina ya maeneo yale  wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika.
Ahmed Kipande aliyekuwa ametoka Kilwa Kivinje mkoani Lindi nae akishirikiana na mwanamuziki mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Shamte nao wakaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Kusini ya Kilwa Jazz mwaka 1958.

Kilwa Jazz ikaanza kujizolea umaarufu kwa kutunga na kuimba nyimbo mbali mbali zikiwemo za siasa, mapenzi na za uhamasishaji kupata Uhuru wa Tanganyika.
Aliunga na kuimba wimbo wa ‘TANU yajenga nchi’, nchi yetu’  ‘enyi Vijana tujenga yetu Doli na ‘It can be done, play your party’
Zingine zilikuwa za ‘Roza waniuwa uwa’, ‘Nipate lau nafasi’, ‘Nacheka cheka Kilwa leo’ na ule wa  Maneno hayafai’

Wimbo wa Nacheka cheka ulitungwa na Ahmed Kipande baada ya kukopi wimbo wa  Tabu Ley na John Bokelo wa ‘Mokolo nokokufa’ halikadhalika nyimbo za Nacheka cheka Kilwa leo na Maneno hayafai ambazo walizikopi na kupesti toka wimbo wa Course au Povouir wa T.P.OK. Jazz.

Mwaka 1973 Kilwa jazz ilialikwa na kutumbuiza kabla ya onyesho la gwiji la muziki wa dansi, Franco Makiandi na bendi ya T.P.OK. Jazz  iliyefanya onyesho kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Luambo Makiadi baada ya kuzisikiliza nyimbo hizo alimfuata Ahmed Kipande na kumpongeza kwa umahiri wake mkubwa wa ‘kokopi na kupesti’ pasipo kukosea.

Akimsifia baba yake Kipande Ahmed alisema kwamba mwaka 1961 siku Tanganyika inapewa Uhuru toka kwa Wakoloni, bendi ya Kilwa Jazz ilikuwa Uwanja wa taifa ikiporomosha muziki ambapo ilitoka na wimbo wa  kumshukuru mungu kwa kupata Uhuru.
Mtoto huyo wa marehemu Ahmed, aliimba mistari michache ya wimbo huo “ Ewe mola tunakuomba uibariki Tanganyika yetu na jirani  zetu, Uhuru tumepata lakini Nyoyo zina sikitika wenzetu wanateseka  Wakoloni wa mewashika…”
Bendi ya Kilwa Jazz ilikuwa na makao makuu yake katika kona ya mitaa ya Muhoro na Jangwani ambako siku moja ilipiga muziki nje ya Ofisi yao na kuwashangaza watu kuona bendi ikipiga muziki mchana. Lakini ilikuwa mipango kamambe ikipangwa maeneo hayo kwa viongozi wanamapinduzi siku chache kabla ya mapinduzi ya Zanzibar viongozi walikuwa wakipanga mikakati ya mapinduzi yaliyouondoa utawala wa Kisultani mwaka 1964 huko Zanzibar. Bendi ya Kilwa Jazz baadaye haikuelewa na jamii. Wengine wakafika mbali zaidi wakizusha maneno kwamba ni bendi ya serikali ‘eti’ ilikuwa ikialikwa kutoa burudani katika sherehe nyingi za kitaifa.
Kilwa jazz pia ilialikwa kutoa burudani katika sherehe za ndoa ya mmoja wa mawaziri wa serikali ya Tanganyika wakati huo, Oscar Kambona.

Ahmed  Kipande katika sherehe hiyo alionesha kipaji chake kwamba si cha kubahatisha. Alitunga wimbo wa papo kwa papo wa kuwasifia wanandoa hao Oscar Kambona na mkewe.
Yaelezwa kwamba Kambona aliinuka toka kwenye kiti cha maharusi na  kwenda kumkumbatika Kipande kisha akamtunza kwa pesa. 
Ni miaka 27 sasa tangu Ahmedi Mohammed Kipande afariki dunia  Aprili 27, 1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa kipindi kirefu. Alizikwa kwenye  makaburi ya Tandika Maguruwe, mkoani Dar es Salaam  Aprili 28,1987.

Mugu ailaze roho ya marehemu Ahmedi  Kipande  pahala pema peponi,  Amen.  


No comments: