Monday, April 14, 2014

MZEE KASSIM MAPILI




MAPILI  GWIJI  ALlYETUMIA MAISHA YAKE YOTE  KATIKA MUZIKI.

Machi, 2013.

MZEE KASSIM  MAPILI  ni mwanamuziki mkongwe aliyeanza tasnia hiyo kabla ya nchi yetu ya Tanganyika, wakati huo haijapata Uhuru.
Mzee Mapili ni mwenye vipaji vingi vya kutunga, kuimba nyimbo za muziki wa dansi na kupiga gita. Pamoja na umri wake kumtupa, Mapili ni ‘mfua uji’ wakati wote  wala  haoneshi  dalili za ‘kuchoka’ kama Wazee wengine wenye umri kama wake.
Mwaka huu wa 2013, Mapili  ametimiza miaka 76 ya  kuzaliwa kwake, bado ni  mwenye nguvu, Afya njema  na kumbukumbu nyingi zilizojaa kichwani mwake.
Mzee Mapili amekula chumvi nyingi ingawaje ukikutana naye mitaani,  unaweza kumdhania kuwa  ni ‘Mzee kijana’  kwa jinsi anavyojichanganya katika maongezi na watu wa rika na jinsia tofauti
Mzee Kassim Mapili ameeleza kwamba amevuka mito, mabonde na kuparamia milima iliyoshindikana katika kuyatafuta maisha. Na amesisitaza kwamba hatokata tamaa kuendelea  kutafuta mafanikio hadi ifikapo kipindi atakapoishiwa nguvu.

.
Akisimulia historia ya maisha yake, Mzee Mapili amesema kwamba alizaliwa katika kijiji cha Lipuyu kilichopo Tarafa ya Lionya, Wilaya Nachingwea mkoani Lindi mwaka 1937.
Alipata elimu ya msingi sambamba na ya Koraan, akiwa kijijini kwake Lipuyu mkoani Lindi. Anasema akiwa madrasa alikuwa mahiri wa kughani  kaswida katika  Madrasa yake. Hata mapenzi yake ya kuimba nyimbo  aliyapata kupitia Madrasa hiyo.
Ni mwanamuziki mzoefu mwenye uwezo mkubwa wa kuimba na kupiga gita. Anasema  alianza kujifunza kupiga muziki wakati nchi yetu ikiwa bado inatawaliwa na Ukoloni wa Waigereza.
Jina la Kassim Mapili likaanza kusikika katika ulimwengu wa muziki mara tu alipojiunga katika bendi ya White Jazz iliyokuwepo mjini Lindi mwaka 1958.
Sifa zake za kupiga muziki zikazagaa sehemu mbalimbali hadi mikoa ya jirani. Hakuchuka muda mrefu katika bendi hiyo,  mwaka uliofuatia wa 1959  akahama na kujiunga na bendi ya Mtwara Jazz wakati huo.
Bendi ya Holulu ya mjini Mtwara, nayo ikaona ni bora inyakue ‘kifaa’ hicho. Mapili akashawishika na maslahi aliyo ahidiwa, ndipo alipoamua kujiunga katika bendi yao mwaka 1962.
Kwa kuwa nchi yetu ya Tanganyika wakati huo  ilikuwa tayari
imekwisha pata Uhuru, Chama TANU kiliazisha vikundi vya  Vijana kukitangaza chama hicho.
Hivyo mwaka 1963,  Mzee Mapili akaoneka anafaa kusaidia kufanya kazi hiyo, akachukuliwa kwenda katika bendi ya Jamhuri Jazz ambayo ilikuwa ya vijana wa TANU (TANU Youth League) ya Lindi.
Baada ya kufanya kazi nzuri hapo Lindi, akateuliwa kuwa muasisi wa bendi nyingine ya Vijana wa TANU (TANU Youth League) huko Tunduru,  mkoani Ruvuma mwaka 1964.
Katika kutafuta maslahi murua wakati huo, alilazimika  kwenda kujiunga na bendi ya Luck Star mwaka 1965,  iliyokuwa na makazi yake Kilwa Masoko mkoani Lindi.
‘Kizuri hupendwa popote’ Kassim hakukaa sana na Luck Star, mwaka huohuo alisakwa ‘kwa udi na uvumba’ na bendi ya Kilwa Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Ahmed Kipande, akajiunga nayo.
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilianzisha bendi mbili za muziki wa dansi za JKT ‘Kimbunga Stereo’ na JKT ‘Kimulimuli’. Kwa kuwa sifa za  Mzee Mapili zilikuwa zimezagaa kupitia wa muziki hapa nchini,  Jeshi hilo lilimchukuwa kwenda kuwa muasisi wa bendi ya JKT Mgulani, jijini Dar es Salaam mwaka 1965.
Ushindani wa bendi katika Majeshi, ukaaza. Jeshi la Polisi nalo likamhitaji ajiunge nalo. Alikubali kwenda kuasisi bendi yao ya Polisi Jazz  baada ya kupata ajira tarehe 15, Desemba 1965. Polisi Jazz  ilikuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Polisi Barracks, jijini Dar es Salaam.
 Akiwa ‘Afande’ Mzee Kassim Mapili aliteuliwa kuwa mwalimu wa bendi ya  Wanawake ikijulikana kama Woman Jazz Band Desemba 23,1965.
Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Umoja wa Vijana TANU (TANU Youth League) ambapo alisafiri na bendi hiyo kwenda nchini Kenya, kwenye sherehe za siku ya Kenyata.(Kenyata day) Kenyata alikuwa rais wa kwanza wa nchi ya Kenya.
Mzee Kassim Mapili alipata pigo kubwa Mei 1966, baada ya kuondokewa na baba yake mzazi Mzee Said Amri Makolela, aliyeuawa wakati akipambana  na Nyati porini. Anamshukuru mungu kwani mama yake mzazi Bi. Ajena Mussa Mtikita, bado yu hai.
Baada ya kuvunjika kwa bendi ya Woman Jazz  mwaka 1974, ndiyo ikwa mwanzo wa kuanzishwa kwa bendi ya Vijana Jazz  baada ya kuwakusanya vijana wa wakati huo akina Hemed Maneti,  Hassan Dalali, Manitu Mussa, Hamza Kalala ‘Komandoo’ Chakupele,  Abdallah Kwesa , Agrey Ndumbaro na wengine wengi.
Kassim Mapili alistaafu toka jeshi la Polisi  Mei 05, 1981 akiwa na cheo cha Sajenti. Mara baada ya kustaafu mwishoni mwa mwaka 1981, alijiunga na bendi ya Tanzania Stars Ushirika Jazz.
Kwa kipindi kirefu Mzee Mapili amekuwa  akiitwa kuhudhuria semina nyingi. Mwaka 1982,  alishiriki katika semina ya wanamuziki iliyofanyika mjini Bagamoyo. Katika semina hiyo ilipelekea kuundwa kwa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), naye akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho.
Kila panapofanyika jambo la manufaa katika muziki hapa nchini, Mzee Mapili amekuwa akishirikishwa kikamilifu. Amekuwa akitoa michango ya mawazo yenye busara katika tasnia ya muziki  kwa nyakati tofauti.
Busara zake zilipelekea mwaka 1986 kuchaguliwa kuwa mmoja wa washiriki katika uundwaji wa kundi la wanamuziki 57, lililoitwa Tanzania All Stars.
Mwaka huohuo alishiriki katika tamasha la utoaji  wa zawadi kwa Wasanii wakongwe, akiwemo Mzee Morris Nyunyusa, Mzee Makongoro, Mzee Mwinamira, Mbaraka Mwinshehe na wengine.
Kassim Mapili alikuwa muasisi katika shindano la nyimbo kumi bora za wanamuziki wa dansi (Top Ten Show) mwaka 1988, akiwa kama Mwenyekiti wa CHAMUDATA.
Mzee Mapili akiwa kama Baba, aliwakumbuka watoto wa mitaani wanaosumbuka katika kutafuta maisha. Alianzisha bendi ya watoto  wa umri wa miaka 16,  ambao baadaye walifanya onesho kamambe,  sambamba na siku ambayo watoto wa Afrika Kusini waliteswa huko Soweto.
Mapili mwaka 1993, alikuwa mstari wa mbele wa uanzishwaji wa bendi ya Wazee ya Shikamoo Jazz. Bendi hiyo bado ipo ikiongozwa na Mzee Salumu Zahoro.
Hekima na busara za Mzee  huyu,  zilipelekea mwaka 1974, kuteuliwa kuwa mlezi wa bendi ya Super Matimila.
‘Aliyena nacho huongezewa’ usemi huu ulijiri kwa Mzee Kassimu Mapili,  ambaye Nyota yake aliendelea kung’ara, aliteuliwa kuwa mkufunzi wa bendi ya Gold All Stars mwaka 1977.
Mzee Mapili hakuwa mchoyo wa kugawa ujuzi alionao, kwani alishiriki kikamilifu katika uundwaji upya wa bendi ya Super Volcano, akiwa na binti ya Mbaraka Mwinshehe, Taji.
Kama nilivyotangulia kukujuza kwamba  Mzee Mapili anaonekana si mtu wa kuchoka kiafya, siri yake alilidokeza hivi. “Nakula chakula vizuri,  ninafanya mazoezi ya viungo kila siku, Sigara, Pombe na starehe zisizokuwa za lazima, kwangu  ni  mwiko…”  Mzee Mapili anafafanua siri ya mafanikio ya afya yake kuwa imara hadi leo.
Pamoja na umri wake kuwa mkubwa, anasema bado  hajafikia wakati wa kuwa tegemezi kwa watoto wake. Anamiliki bendi ya Orchestra Mapili Jazz ambayo bado haijafahamika kwa kiasi kikubwa kwa baadhi ya washabiki wake.
“Bendi yangu huwa inawasisimua mno wapenzi wa muziki wa zamani kwa kuwapigia nyimbo za zamani kwa maombi yao maalum…”  anasema Mapili.
Kassim alienda mbali zaidi akijigamba kwamba wakati akipiga gita, huimba  kufanya ‘shoo’ mwenyewe  akiwakumbusha wazee wenzake mitindo yao ya  zamani ya Twist, Bumping, Charanga, Chacha na Pachanga.

“Nikianza kucheza Twist, juu… juu… chinii… chinii… juu… chiniii,  watu ukumbini huzizima na kunizunguka wakinipongeza wangine wakisema  “Wazee dawa…”  Mapili anatamka kwa kijiamini huku akionesha jinsi ya kucheza mtindo huo.
“Ninauheshimu sana muziki kwani ndiyo ulionilea hadi sasa. “Nimekulia na kuzeeka nikiwa katika muziki, sijawahi kufanya kazi nyigine tofauti na muziki katika maisha yangu yote. Hata nilipopata ajira katika Jeshi la Polisi, nilikuwa akifanya kazi ya muziki…” Anasema Mapili.
Kassim Mapili ni baba wa familiya ya mke na watoto watatu, aliowataja kwa majina ya Kuruthum, Said na Hassan. Kati yao hakuna hata mmoja aliyefuata nyao zake za muziki.
Mapili amekuwa mstari wa mbele katika shughuli takriban zote za kifamiliya za wasanii na wanamuziki wenzake hapa nchini. Huwa habagui kwamba ni Mtanzania ama vinginevyo. Mfano halisi wiki iliyopita  kabla ya kifo cha mwanamuziki Kabeya Budu wa bendi ya Le Capitale, Mapili alikuwa mstari wa mbele kwenda  kumjulia hali  akiwa hospitalini. Pia alishiriki kikamilifu katika mazishi ya mwanamuziki huyo Kabeya Badu, aliyefariki tarehe 06 Machi,  2013 katika hospitali ya Muhimbili kwa maradhi ya figo. Badu alikuwa raia wa  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC).

Mzee Kassim Mapili amemalizia kwa kuwasihi wanamuziki hususani vijana, kujifunza kupiga ala za muziki, ili wafikie malengo yao ya kuwa wanamuziki watakao kubalika kimataifa. Aidha amewataka kuzingatia heshima na upendo miongoni mwao.


Mwisho.


No comments: