Monday, April 14, 2014

JABARI LA MUZIKI MARIJANI RAJABU


 JABARI LA MUZIKI  MARIJANI RAJABU
APRILI 15,2014.

MARIJANI RAJABU KWELI HATUNAYE TENA HAPA DUNIANI LAKINI KAMWE WADAU NA WAPENZI WA MUZIKI WA DANSI HAPA NCHINI HAWATAMSAHAU.
ALIKUWA MMOJA MIONGONI MWA WANAMUZIKI WALIOTOA MCHANGO MKUBWA WA MAENDELEO YA NCHI KUPITIA TUNGO ZA NYIMBO ZAKE MARIDHAWA  ZILIZOKUWA ZIKIENDANA NA WAKATI.
MARIJANI MWEZI MACHI 23, 2014, ALITIMIZA MIAKA 18 TOKA KIFO CHAKE. NGULI HUYO ALIFARIKI MACHI 23, 1995 NA KUZIKWA SIKU ILIYOFUATIA YA MACHI 24, 2013 KATIKA MAKABURI YA KISUTU JIJINI DAR ES SALAAM.

MARIJANI ALIZALIWA TAREHE MARCHI 03, 1955 KARIAKOO, JIJINI DAR ES SALAAM. KWA MAPENZI YAKE MUNGU, AKAMCHUKUA AKIWA NA UMRI MDOGO WA MIAKA 40 TU.
ALIKUWA AKITUNGA NA KUIMBA NYIMBO ZILIZOKUWA ZIMEJAA MAUDHUI MEMA KWA JAMII, IKIZINGATIWA KWAMBA TAKRIBAN NYIMBO ZAKE ZOTE ZILIKUWA NI VISA VYA KWELI.
NGULI HUYO ALIKUWA NI MITHIRI YA ‘MTAMBO’ WA KUREKEBISHA TABIA YA MTU YEYOTE ALIYEFANYA MAMBO KINYUME CHA MAADILI PASIPO KUJALI CHEO, URAFIKI, UDUGU HATA UKARIBU.
UBORA WA MASHAIRI KATIKA NYIMBO HIZO, NI KATI YA SABABU ZA KUENDELEA KUPENDWA NA WAPENZI WA MUZIKI HAPA NCHINI HADI KUFIKIA KUITWA ‘JABARI LA MUZIKI’
KILA KUMBI ZA STAREHE UTAKAZOINGIA HAPA NCHINI, NYIMBO ZAKE HAZIKOSI KUSIKIKA ZIKIRINDIMA. HALI KADHALIKA BENDI ZETU ZA MUZIKI WA DANSI ZILIZOSALIA NAZO HAZIWEZI KUMALIZA ONESHO PASIPO KUPIGA ANGALAU WIMBO MMOJA WA NGULI HUYO.  
WASIFU WA MARIJAN RAJABU UNAELEZA KWAMBA MAMA YAKE ALIKUWA MAMA WA NYUMBANI WAKATI BABA YAKE ALIKUWA NA SHUGHULI ZA UCHAPISHAJI.

MAISHA YAKE YA UTOTO YALIKUWA YA KAWAIDA ILA ALIKUWA AKIPENDA SANA UIMBAJI WA TABU LEY, MWIMBAJI TOKA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO NA MWIMBAJI TOKA NCHINI GUINEA, SORRY KANDIA. PIA ALIKUWA AKICHEZA MPIRA WA MIGUU.
ALILELEWA KATIKA MISINGI YA DINI YA KIISLAM KWA HIVYO ALIHUDHURIA MAFUNZO YA DINI UTOTONI KAMA INAVYOTAKIWA.

ALIPOKARIBIA  UMRI WA MIAKA 18, NURU YAKE YA KATIKA MUZIKI ILIANZA KUNG’ARA, BAADAYE ALIJIUNGA NA BENDI YA STC JAZZ, IKIWA CHINI YA MPIGA GITAA MAARUFU WAKATI HUO RAPHAEL SABUNI. KABLA YA HAPO,  BENDI HIYO ILIKUWA UNAJULIKANA KAMA THE JETS.
AKIWA KATIKA BENDI HIYO MARIJANI ALIWEZA KUTOKA NJE YA TANZANIA KWA MARA YA KWANZA AMBAPO ALIKWENDA NAIROBI NCHINI KENYA.
KATIKA SAFARI HIYO ALIAMBATANA NA BENDI KWA MADHUMUNI YA KWENDA KUREKODI NYIMBO ZILIZOTOKA KATIKA NEMBO  YA PHILLIPS.
AKIWA NA BENDI HIYO YA STC, UONGOZI WA SHULE YA SEKONDARI YAKE YA TAMBAZA ULILETA MALALAMIKO KWA UONGOZI WA STC ILIYOKUWA IKIMILIKI BENDI HIYO JAMBO AMPALO STC IKALAZIMIKA KUMUENGUA.

MWAKA 1972 MARIJANI ALIHAMIA BENDI YA SAFARI TRIPPERS, ILYOKUWA INAUNDWA NA VIJANA WENZAKE NA HAIKUWA IKIMILIKIWA NA CHOMBO CHA UMMA.

JAMBO PEKEE MARIJANI ALIONEKANA KWAMBA ALIKUWA ‘AMEBANWA’ HUKO STC KATIKA FURSA YA KUNG’ARA KATIKA UIMBAJI, UBORA WAKATI HUO ALIFINGUKA HASWA NA KUWEZA KUINYANYUA SAFARI TRIPPERS KUWA MOJA YA BENDI MAARUFU HAPA NCHINI.

ALIWAKUTA VIJANA WENZAKE AKINA DAVID MUSSA ALIYEKUWA AKIPIGA GITA LA SOLO NA KUIMBA. DAVI HIVI SASA NI MLOKOLE AMEACHANA NA MAMBO YA MUZIKI ANAISHI KARIBU NA KLABU YA TTC CHANG’OMBE.
WENGINE WALIKUWA ALLI RAJABU (MWIMBAJI), CHRISTIAN KAZINDUKI ALIYEKUWA AKILIUNGURUMISHA GITA ZITO LA BESI, JOSEPH BERNARD KWA UPANDE  WA SAXOPHONE NA JEFF AMBAO HADI SASA WANAPIGA KATIKA BENDI YA MLIMANI PARK WALIOJIUNGA NAYO MWAKA 1978.

WALIWEZA KUTOA VIBAO VILIVYOPENDWA MFULULIZO PIA WALIZUNGUKA NCHI NZIMA. VIBAO KAMA ROSA NENDA SHULE, MATILDA, BABA NYERERE MLEZI, MKUKI MOYONI, KUMEKUCHA AMBAO ULIPENDWA NA RADIO TANZANIA DAR ES SALAAM (RTD) NA KUFANYWA KUWA KIAMSHO CHA KIPINDI CHA KUMEKUCHAKILICHOKUWA KIKIRUSHWA KILA CHA ALFAJIRI.

SAFARI  TRIPPERS ILIKUWA KATIKA USHINDANI NA BENDI NYINGINE ZA VIJANA NA HASA AFRO 70, ILIWEZA KUUZA ZAIDI YA NAKALA 10,000 ZA SANTURI NA HIVYO KUWEZESHA BENDI KUNUNUA VYOMBO VYAKE VIZURI AINA YA RANGERS VILIVYOKUWA MAARUFU WAKATI HUO, IKIWA NA MAKAO YAKE MAKUU ENEO LA CHANG’OMBE UHINDINI, TEMEKE JIJINI DAR ES SALAAM.

‘JABALI LA MUZIKI’ MARIJANI ALIHUSUDU KWA KIASI KIKUBWA UIMBAJI WA ALIYEKUWA KIONGOZI WA EMPIRE BAKUBA KABASELE YAMPANYA ‘ PEPE KALE’ HATA BAADHI YA NYIMBO ZAKE ZILIKUWA AKIZIGHANI, ZIKISHABIHIANA NA LADHA YA UIMBAJI WA PEPE KALE.

‘LAKUVUNDA HALINA UBANI’ MSEMO HUU ULIJIONESHA WAZI PALE MAELEWANO MABAYA KATI YA WANAHISA WANNE WA BENDI HIYO, YALIYOPELEKEA KUSAMBARATIKA LICHA YA BENDI HIYO AMBAYO ILIKUWA IKO JUU KIMUZIKI WAKATI HUO MWAKA 1978.

MARIJANI AKIAMBATANA NA WENZAKE KAZINDUKI ‘PACHA’  WAKE KATIKA KUIMBA HATA KUSHABIHIANA MAJINA, ALLY RAJABU, BENARD  NA JEFF WAKAJIUNGA NA BENDI MPYA YA DAR INTERNATIONAL ILIYOKUWA ILIYOONGOZWA NA MPIGAJI GITA LA SOLO ABEL BARTAZAR ALIYEAMBATANA NA GWIJI MWINGINE MUHIDINI GURUMO.
WAKIUNGANA NA WANAMUZIKI WENGINE, MAHIRI WALISHIKAMANA KUUNDA KIKOSI ‘MOTO’ AMBACHO  BAADA YA KUPAKUA ‘VIBAO’ VYAKE VYA KWANZA UKIWEMO WA ‘MARGARET’ WALITIKISA ANGA YA MUZIKI HAPA NCHINI.
KATIKA BENDI HIYO YA DAR INTERNATIONAL WALIKUTA WANAMUZIKI WAZURI NAO WAKAONGEZA  NGUVU NA KUIFANYA BENDI HIYO KUPATA UMAARUFU WA HALI YA JUU KWA VIBAO VYAKE KAMA ZUWENA NA MWANAMEKA, AMBAVYO VILITAMBA KATIKA VIPINDI KADHAA VYA SALAMU VYA RADIO TANZANIA DAR ES SALAAM (RTD) WAKATI HUO.

HALI YA WAKATI ULE, BENDI ILIREKODI VIBAO VYAO  RADIO TANZANIA DAR ES SALAAM (RTD) NA KUAMBULIA SHILINGI 2,500 TU.

YAELEZWA KWAMBA NYIMBO ZAO TISA ZILIUZWA KWA KAMPUNI YA POLYGRAM BILA YA RIDHAA YAO.

KATI YA MWAKA 1979 NA 1986 BENDI ILIPIGA MUZIKI KARIBU KILA WILAYA  HAPA NCHINI KWA MINAJIRI YA KUTOA ELIMU SANJARI NA KUWABURUDISHA WANANCHI WAKIPIGA KATIKA MTINDO WAO WA SUPER BOMBOKA.

MARA NYINGI ILIPOKUWA HAPA DAR ES SALAAM, KAMA ILIVYOKUWA SAFARI TRIPPERS, MAKAO YAKE MAKUU YALIKUWA KATIKA HOTELI YA PRINCESS MNAZI MMOJA, SUPER BOMBOKA LILISAKATWA KILA WIKI, KATIKA UKUMBI WA SUPER FANAKA BUGURUNI.

‘MBIO ZA  SAKAFUNI HUISHI  UKINGONI’ UCHAKAVU WA VYOMBO HATIMAE MWAKA HUO 1986, UKAMALIZA MBIO NDEFU ZA BENDI HII.

MARIJANI RAJABU ‘JABARI LA MUZIKI’ ALIKUWA MMOJA KATI YA WANAMUZIKI 57 WALIOUNDA KUNDI LA WASANII LIKIJULIKANA KAMA TANZANIA ALL STARS, MWAKA 1987.

KUNDI HILO LILITIA FORA MKWA WIMBO WAKE WA ‘FAGIO LA CHUMA’  WIMBO HUO ULIKUWA NI KUITIKIA KAULIMBIU YA RAIS WA AWAMU YA PILI ALI HASSAN MWINYI, JUU YA UWAJIBIKAJI.

KUNDI HILO LILIREKODI VIBAO VINGINE VINNE AMBAVYO SI RAHISI KWA BENDI ZILIZOPO SASA KUFIKIA UBORA WAKE KIMUZIKI.

KUNA WAKATI DAR INTERNATIONAL ILISIMAMA KIMUZIKI, MARIJANI ALISHIRIKI KUPIGA MUZIKI KATIKA BENDI YA JESHI LA WANANCHI TANZANIA (JWTZ) YA MWENGE JAZZ AMBAKO ALIPIGA MUZIKI  KWA MUDA MFUPI.

MARIJANI ALIPIGA HODI KATIKA JIJI LA ARUSHA NA KUJIUNGA NA BENDI YA KURUGENZI JAZZ AMBAKO HUKO ALIDUMU MWAKA MMOJA PEKEE NA KUREJEA DAR ES SALAAM.

MFANYABIAHARA MMOJA WA JIJINI DAR ES SAAM ALIYEJULIKANA KWA JINA ROGER MALILA,ALIMCHUKUWA MARIJANI KWA AJILI YA KUANZISHA BENDI YA ORCHESTRA BENE BENE. BENDI HIYO WAKATI HUO ILITAMBA NA MTINDO WAKE WA ‘MAHEPE’ MWANZONI MWA MIAKA YA 1990.

MARIJANI KWA MARA NYINGINE TENA BAHATI HAIUKUWA UPANDE WAKE, KWANI BENDI HIYO HAIKUDUMU KWA KIPINDI KIREFU KUFUATIA UKOSEFU WA VYOMBO VYA MUZIKI. HATIMAYE MAMBO YAKAENDA KOMBO TOFAUTI NA WALIVYOTARAJIA.

BAADA KUHANGAIKA KWA MUDA MREFU  HUKU NA KULE MARIJANI ‘JABARI LA MUZIKI’ ALIAMUA KUTHUBUTU KWA KUANZISHA KUNDI LAKE LA MUZIKI LIKIITWA AFRICULTURE.
LAKINI NAYO HAIKUDUMU NAYO IKAFA ‘KIFO CHA MENDE.’

MAISHA YA MWANADAMU NI KITENDAWILI KILICHOJAA MAJARIBU MENGI.
INAELEZWA KWAMBA KUFIKIA MWAKA 1992, HALI YA MAISHA YA MARIJANI ILIKUWA NGUMU KUPITA KIASI. ALIFIKIA KUENDESHA MAISHA YAKE KWA KUUZA KANDA ZA NYIMBO ZAKE. ALIJENGA KIBANDA NJE YA NYUMBA YAKE, MAENEO YA KARIAKOO, JIJINI DAR ES SALAAM.

PAMOJA NA NYIMBO NYINGI, ZA KUIMBIA CHAMA TAWALA NA SERIKALI, NA HATA TUNGO YAKE MWANAMEKA KUTUMIWA KATIKA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE, MARIJANI RAJABU HADI SEPTEMBA 09, 2012  NDIPO RAIS DK. JAKAYA KIKWETE ALIPOMTUNUKIA TUZO YA HESHIMA YA MUUNGANO KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 51 YA UHURU  IKULU JIJINI DAR ES SALAAM.

WASANII WENGINE WALIOTUNUKIWA SIKU HIYO NI PAMOJA NA KIONGOZI WA ZAMANI WA MSONDO NGOMA, MUHIDINI GURUMO, MWIMBAJI WA MKONGWE  WA TAARABU, FATUMA BINT BARAKA, MSANII WA MAIGIZO YA FILAMU, FUNDI SAID ‘MZEE KIPARA’ NA MWANARIADHA MKONGWE JOHN STEVEN AKWARI.

HAPANA SHAKA UTAKUWA UNAZIKUMBUKA NYIMBO ZA NGULI HUYU ALIZOTUNGA NA ZINGINE KUSHIRIKI KIKAMILIFU KUIMBA KAMA VILE MASUDI, HABARI YAKO, SAUTI YAKO NYORORO, BABA ANNA, KITINDA MIMBA, SALAMA NAKUITA, NAMSAKA MBAYA WANGU, ZUWENA NA NDOA YA MATESO.

MARIJANI RAJABU HAKUISHIA HAPO KWANI ALITOKA NA NYIMBO ZANGINE ZA TABU NI HALI YA DUNIA, NDOA YA MATESO, NAMSAKA MBAYA WANGU, MAMA WATOTO, TAMAA MBELE NA BABA WATOTO AMBAZO ZILIGUSA HISIA ZA  WAPENZI WA MUZIKI NA WALE WAKAWAIDA WALIOKUWA WAKISIKILIZA REDIO.
NYIMBO WA ‘UKE WENZA UNA MAMBO’, ULIOFYATUA, NDOA NYINGI ZA MITARA ZILIJIREKEBISHA KITABIA.
WIMBO WA GEORGINA ULIKUWA WIMBO ULIOTIA FORA MIONGIONI MWA NYIMBO BORA HAPA NCHINI.

MTUNZI WA WIMBO HUO WA GEORGINA ALIKUWA WANAMUZIKI MKUNG’UTAJI GITA LA RHYTHM MAHIRI NCHINI JUMANNE UVURUGE, UKAIMBWA KWA UMAHIRI MKUBWA KWA SAUTI YENYE HISIA KALI NA MARIJANI RAJABU.

MARIJANI ALITHUBUTU KUKEMEA TABIA MBOVU YA NDUGU YAKE WA KARIBU KUPITIA WIMBO WA ‘CHAKUBANGA’.  WIMBO HUO ULIKUWA NI KISA CHA KWELI AMBACHO NDUGU YAKE HUYO BAADA YA KUTOKA ULAYA, AKAJIITA JOHN SMITH BADALA YA JINA LAKE HALISI LA CHAKUBANGA.

KUPATA LADHA HALISI YA WIMBO HUO, SEHEMU FUPI YA GHANI ZAKE KATIKA KIBAO CHA CHAKUBANGA NI KAMA IFUATAVYO:

“LEO KIJANA NINASEMA EEH! HAYO MAMBO YAKO UNAYOFANYA EEH, MWISHO WAKE BWANA, MAMBO YATAKUWA MABAYA, WALA USIDANGAYIKE NA CHEO ULICHOPATA, KUDHARAU WAZAZI KUHADAIKA NA DUNIA, MWANA VIBAYA EEH, VIBAYA MWANA VIBAYAA.

“FIKIRI KWANZA ULIKOTOKAA, USIJIFANYE HUNA BABA WALA MAMA WALIO KULEA, KWA TAABU NYINGI NA MASHAKA , WAKAKUSOMESHA UKAHITIMU MAFUNZO, MBONA UNAWANYANYASA NA MATUSI KUWATUKANAAA, MWANA VIBAYAA, VIBAYA MWANA VIBAYAA. MAMBO YA AJABU ULIYOFANYA EEH, ULIPOCHAGULIWA KWENDA NG’AMBOO ULIPORUDU BWANA, NA JINA UMEBADILISHA, JINA LAKO CHAKUBANGA, UNAJIITA JOHN SMITH, NA MWENDO UMEBADILI BEGA MOJA UMELISHUSHA…”
NYIMBO ZA  NGULI HUYU ZITAENDELEA KUSIKIKA VIZAZI NA VIZAZI KWAKUWA ZIMEBEBA UJUMBE MZITO KWA JAMII YEYOTE ILE.

JE, TUNAMUENZIJE MARIJANI RAJABU? USHAURI  WANGU KWA VIJANA WA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA KUFUATA NA KUYAENDELEZA YOTE MAZURI YA WATANGULIZI WAO KAMA AKINA MARIJANI, GURUMO, MBARAKA MWINSHEHE NA WENGINE WENGI.

MUNGU AIWEKE ROHO YAKE PAHALA PEMA PEPONI, AMINA.

MWISHO.


No comments: