Wednesday, December 24, 2014

BOZI BOZIANA ‘MZEE BENZI’ ASIYECHUJA KIMUZIKI



BOZI BOZIANA ‘MZEE BENZI’ ASIYECHUJA KIMUZIKI.

Bozi Boziana  ‘mzee Benzi’ kama anavyojulikana na wengi ni mwanamuziki ni kiongozi wa kundi  Anti Choc toka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Licha ya umri wake kuwa mkubwa, awapo jukwaani huwezi kuamini macho yako unapomuona akiimba na kucheza sambamba na wanenguaji wa bendi hiyo.

Muziki wa nguli huyo huwa hauchuji kama ilivyo kwa wanamuziki wengine.

Bozi amejizolea sifa lukuki kwa kuweza kuongoza kundi hilo ambalo ni miongoni mwa bendi zinazokubalika huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Sifa nyingine kubwa ya mwanamuziki huyo ni kwamba pamoja na utunzi na uimbaji Bozi pia ni mkung’utaji mzuri wa gita, aliyepitia katika bendi nyingi kupiga muziki katika mtindo wa soukous.

Imani iliyojengeka kwa baadhi ya wadau wa muziki ni kwamba mwanamuziki bora ni yule anayekubalika kupiga muziki katika bendi yeyote atakayokwenda.

Kama ni hivyo basi miongoni mwa hao ni Bozi Boziana ambaye aliwahi kupitia bendi nyingi zikiwamo za Bamboula de Papa Noel,  na Zaiko Langa Langa. Zingine zilikuwa za Isifi Lokole, Yoka Lokole, Langa Langa Stars na Choc Stars

Baada ya kupata uzoefu wa muda mrefu katika muziki, alihamasika kuunda bendi yake, akaweza kuanzisha bendi ya Orchestra Anti-Choc.

Wasifu wa mwanamuziki huyo unaeleza kuwa jina lake kamili anaitwa Mbenzu Ngamboni Boskill.
Alizaliwa  mwaka 1952 huko Jamhuri ya Kidemkokrasia ya Kongo.

Alianza muziki wa Afro-Pop katika  bendi ya Air Marine. Mafanikio yake katika muziki  alianza kuyaona ilipotimu mwaka 1974, alipojiunga na bendi ya Zaiko Langa Langa.

Hapo Zaiko alishirikiana na waimbaji  wengine mahiri wakati huo, wakiongozwa na mkongwe  Papa Wemba na mwezake Evoloko Jocker.

Kabla mwaka  haujatimia, waimbaji Papa Wemba na Evoloko waliondoka katika bendi hiyo ya Zaiko Langa Langa.

Kuondoka kwao kulikuwa ni changamoto kwa Bozi Boziana ambaye naye aliamua kuwafuata na wakanzisha bendi mpya ikaitwa Isifi Lokole

Kukosekana kwa uongozi madhubuti kulisababisha kutokukubaliana katika masuala mbalimbali ya msingi, miongoni yakiwemo ya kimaslahi.

Mtafaruku huo uliwafanya wanamuziki akina Papa Wemba, Boziana, Mavuela Somo na wengine kuondoka bendi ya Isifi Lokole’  wakaunda bendi nyingine mpya iliyopewa jina la Yoka Lokole.

Bozi baada ya kuona kaachwa mithiri ya mkiwa, mwaka 1977 naye akaondoka Yoka Lokole licha ya bendi hiyo kuwa maarufu kwa kipindi kifupi.

Kwa miezi michache  Boziana alishirikiana na mwanamuziki Efonge Gina, ambaye naye alikuwa katika bendi ya Zaiko Langa Langa.

Walirekodi nyimbo kadhaa kama vile Selemani iliyotungwa na Bozi na  Libanko Ya Ngai utunzi wake Gina.

Produza maarufu Kiamuangana Mateta ‘Verckys’ ambaye ni mkongwe wa muziki nchini huo mwaka 1981, aliibadilisha  bendi ya Soukous Super group  na kuita  Langa Langa Stars.

Bendi hiyo alikuwa imejaza wanamuziki waliokuwa na vipaji tofauti akina Evoloko Jocker, Dindo Yogo na  wnengine wengi.  Bozi Biziana alialikwa kujiunga vijana hao naye akaubali na kuicha  Zaiko Langa kwa mara ya pili.

Boziana alidumu kwa miaka michache hapo Langa Langa Stars kabla ya kuondoka kwenda kujiunga na bendi kubwa nchini humo  Choc Stars aliyokuwa chini Ben Nyamabo ambako alipiga hadi mwezi Novemba 1985.

Akiwa na bendi hiyo ya Choc Stars alirekodi baadhi ya nyimbo ambazo zilikuja kuwa maarufu za Sandu Kotti, Alena, Mbuta-Mutu na Retrouvailles a Paris.


Bendi ya Choc Stars ilikuwa na wanamuziki wengi wenye vipaji lukuki akina Fifi Mofude, Djo Nolo, Koffi Alibaba, Wally Ngonda, Rigo Star, mpiga gita la besi Ngouma Lokito.

Boziana aliwahi kushinda zawadi ya Kora All-African kwa album yake kuwa bora toka nchi za Afrika ya Kati.

Kwa wapenzi wa muziki hapa nchini watamkumbuka Bozi jinsi alivyoteka wapenzi katika maonesho kadhaa aliyoyafanya hapa nchini kwa ushirikiano walioonshea kati ya Bozi Boziana, Deesse Mukangi na Joly Detta walivyokuwa wakilishambulia jukwaa kwka staili ya ‘Nzawisa’ katika nyimbo za Tembe na Tembe, Palpitation na zingine nyingi zilifanya watu kuviacha viti vyao kwenda kuwatuza.

Bozi Boziana ana sauti nzuri, yakupendeza akimba huku akipokezana na timu yake ya wanadada wawili, Joly pamoja na Deesse.

Sifa nyingine za mwanamuziki huyu mzee Benzi ni kwamba muziki wake hauna mwingiliano kati ya sauti ,gitaa na synthesizer katika nyimbo zake zote. Mfano katika wimbo wa ‘Ngoyartong020’ tune tatu za mwanzo Boziboziana amemshirkisha Jolly Detta na Deesse,  na sehemu ya pili ya wimbo huo aliongeza nguvu kwa kumuongeza waimbaji na wanenguaji  Scola Miel maarufu kwa jina ‘Nzawissa’ na Betty.

Bozi alifyatua vibao vingi vilivyompa sifa nyingi ukiwemo wa La reine de Sabah, Lelo Makambo Lobi Makambo Evelyne na Fleur de Lys ambazo alimshirikisha mwimbaji wa kike Joly Delta.
Boziana aliachia wimbo mwingine akimshirikisha Deesse na Ba Bokilo.

Bozi Boziana na bendi yake bado anaendeleza muziki akiwa na bendi yake na watanzania watakumbuka kwa mara ya mwisho alikuja hapa nchini kwa mwaliko wa African Stars Entertainment Tanzania (ASET) iliyo chini ya uongozi wa Mkurugenzi Asha Baraka.

Mwisho.

No comments: