Wednesday, December 24, 2014

MAJENGO ALIANZA KUPIGA MUZIKI TANGU MIAKA YA 1950

 MAJENGO ALIANZA MUZIKI MIAKA YA 1950


Majengo Bakari ni mwanamuziki aliyeuthibitisha usemi usemao kuwa “Ujuzi hauzeeki”. Alianza kupiga muziki  tangu miaka ya 1950, lakini hadi sasa anaendelea na fani hiyo.

Majengo anapiga muziki katika bendi ya Shikamoo Jazz 'Wana Chelachela Beat'.

Hilo ni kundi la muziki wa dansi lililoanzishwa mwaka 1993 kwa kujumuisha baadhi ya Wakongwe wa miondoko hiyo kutoka katika bendi nyingine kadhaa.

Wakongwe hao hufanya ‘vitu’ vyao kwa kupiga nyimbo za zamani ambazo zilitamba katika bendi zao.

Salum Zahor ni kiongozi wa bendi hiyo akiwa na nguli wenzake akina John Simon, Ally Adinani, Athuman Manicho, Kassim Mapili na wengine ambao wameshatangulia mbele za haki, akina Mohammed Tungwa, Ally Rashid, Kassim Mponda na Mariam Nylon.

Mbali ya hao, kuna mwanamuziki ambaye makala hii inamuongelea ambaye ni nguli katika upulizaji wa Saxophone ‘mdomo la Bata’ aliyepitia bendi kadha wa kadha za muziki wa dansi, Majengo Bakari.

Majengo akiwa ni mmoja wa waasisi wa Shikamoo Jazz, amechangia mafanikio makubwa ndani ya bendi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuiongezea mashabiki na kuvuta mapromota nje ya nchi.

Aliwahi kumtaja mzungu aitwaye Ronnie Graham aliyekuwa anafanyakazi katika shirika la HelpAge Tanzania, kuwa ndiye chanzo cha Shikamoo Jazz.

Ronnie akiwa HelpAge alikuwa na kamati iliyokuwa na wajumbe akina John Kitime, Mariam Hamdani na marehemu Godigodi.

Kamati hiyo  ndiyo iliyowezesha uletwaji wa vyombo vya muziki kutoka Uingereza.

Baada ya hapo Godigodi na Kitime ndio walienda nyumbani kwa Mzee Salum Zahoro huko Buguruni kumuomba akusanye wakongwe wenzake watengeneze kundi litakalokuwa chini ya Helpage.

Hii ikiwa ni njia mojawapo ya Shirika hilo kuwezesha Wazee kujitegemea.

Majengo amesema kwamba tangu ajiunge na bendi hiyo ameshasafiri nayo kwenda nchi kadhaa, zikiwamo Kenya na Uingereza.

Shikamoo Jazz awali ilikuwa na  maskani yake katika jingo la Tanzania Region, maeneo ya Faya jijini Dar es Salaam.

Baada ya kipindi Ronnie aliamua kujiengua katika bendi hiyo kutokana na vituko vilivyofanywa na mmoja wa wazee hao bendi ilipokwenda nchini Uingereza.

Kutokana na waanzilishi wengine kuwa wameshafariki, ni wanamuziki wanne tu wanaoiendesha Shikamoo Jazz Band sasa, ambao ni Salum Zahor, John Simon, Ally Adinani na yeye mwenyewe.

Wasifu wa mwanamuziki huyu unaeleza kuwa alizaliwa mwaka 1943, Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika shule ya Mchikichini kwa miaka miwili ya 1949 na 50.
Mwaka 1955 ilipoanzishwa shule ya Magomeni Mzimuni, alilazimika kuanza tena darasa la kwanza hadi la nane mwaka 1962.

Akizungumzia historia yake kimuziki, Majengo anasema kuwa, mwaka 1954 ndipo alipoanza kujiingiza kwenye fani hiyo kwa kujiunga na bendi ya Dar es Salaam Jazz, akiwa mkung'utaji Tumba.

Kabla ya hapo, Majengo amesema kuwa, alikuwa akipiga ngoma kwenye vibendi vya watoto na kutumbuiza katika sherehe mbalimbali za kichama, kwenye ofisi za TANU.

Baadhi ya wanamuziki waliompokea Dar es Salaam Jazz, ni pamoja na Edward Salvu na Grey Sindo waliokuwa mahiri kwa upulizaji Sax, ambao kwa nyakati tofauti walichangia kumnoa kwenye chombo hicho.

Ilipofika mwaka 1963, marehemu King Michael Enock aliingia Dar Jazz na kumuongezea ujuzi wa kupuliza Sax kwa kiwango kikubwa.

Mwaka 1968 aliondoka Dar Jazz akiwa keshashiriki kupiga Saxophone kwenye vibao vingi, kikiwamo kile maarufu, 'Mtoto Acha Kupiga Mayowe', akajiunga na bendi ya Wakongoman watupu iliyoitwa King Afrika.

Mwaka 1969 alijiunga na bendi nyingine ambayo nayo ilikuwa ya Wakongoman, iliyoitwa 60 Zaire.

Mwaka 1970 aliamua kujiunga katika bendi ya  Nova Success iliyokuwa ikiongozwa na Papa Micky toka Zaire wakati huo. Alishiriki kupuliza saxophone katika nyimbo kadhaa mojawapo ni Chlorida.

Aliachana na Nova Success mwaka 1974, bendi hiyo ilipopata safari ya Swaziland ambapo yeye alishindwa kwenda kutokana na ajira aliyokuwa nayo katika kiwanda cha BATA Shoes, jijini Dar es Salaam.

Alifanyakazi kazi kwenye kiwanda cha BATA tangu mwaka 1963. Mwaka 1975 aliingia katika bendi ya Maquis du Zaire 'Wana Kamanyola' iliyokuwa chini ya mpulizaji Saxophone hodari, Chinyama Chiaza. Huko alishiriki kurekodi vibao vingi vya bendi hiyo, huku mwenyewe akijisifu kazi aliyoifanya katika wimbo 'Nimepigwa Ngwala'.

Mwaka 1986 Majengo aliamua kusimama kufanyakazi kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifua. Baada ya kupata nafuu alikwenda kumsaidia mwanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango 'King Kiki' aliyekuwa kaanzisha bendi yake ya Orchestra Double O.

Chinyama alipobaini hilo, alimfuata na kumsihi kurejea Maquis du Zaire.

Hakuwa mbishi alikubali na siku aliyorejea kazini alikuta bendi iko chini ya Tshimanga Kalala Assosa ambaye wakati huo walikuwa hawajuwani.

"Nilisalimiana naye kama kawaida lakini nilipotaka kupanda jukwaani kupiga muziki, alinizuia akiniamuru ‘nimsujudie’ kumuomba kwa vile yeye ndiye Kiongozi. “Baada ya majibizano makali nilisusa na kusimama kupigia bendi hiyo…," amesema Majengo.
Amesema kuwa alipokuwa kasimama kuitumikia Maquis, siku moja alitembelea onesho la pamoja na Orchestra Safari Sound (OSS) 'Wana Power Iranda' na mmiliki wake alikuwa mfanyabiashara Huggo Kisima.
Kwa bahati njema Hugo alikuwemo ukumbini humo na alipomuona akamvuta kwake, na Septemba 1986 alianza kazi rasmi na wanamuziki katika bendi hiyo ya OSS.

Kiongozi wa bendi wakat huo alikuwa Muhidin Gurumo aliyekuwa na safu nzuri ya wanamuziki wakiwemo akina Skassy Kasambulla, Mobali Jumbe na Abdallah Kimeza, aliyekuwa akipuliza Saxophone.

Alishiriki kikamilifu  kurekodi vibao vingi akiwa na OSS. Baadhiya vibao hivyo vilikuwa vya 'POP' na 'Mbu'.

Mwaka 1990 alirudi tena Maquis na kushiriki nao hadi mwaka 1993 alipoachia ngazi rasmi na kuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo Jazz.
Tofauti na wanamuziki wengi wenye tabia ya kuvitupia lawama kwa vyombo vya habari kuhusiana na kudidimia kwa dansi, Majengo anaweka wazi kuwa, ubinafsi wa wanamuziki wenyewe ndio chanzo.
Majengo anasema kuwa, kila mmoja kwenye muziki wa dansi anajijali yeye mwenyewe na wanamuziki wake tu na kwamba ushirikiano uliopo ni wa mdomoni si wa vitendo.
Kwa kawaida kazi yeyote ile ni muhimu ilete faida. Kwa upande wa Majengo faida aliyonufaika nayo katika muziki anayo ielezea kuwa ni ngumu kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Yeye amefanikiwa kujenga nyumba maeneo ya Kigogo Luhanga, jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa familiya, Majengo Bakari anaonesha kutofurahishwa jinsi watoto wake kushindwa kurithi kazi yake ya muziki.
Majengo na mke na watoto watano, ambao ni Selemani, Kassim, Juma, Zubeda na Tunu.

Mwisho.

No comments: