Wednesday, December 24, 2014

LOVY LONGOMBA ALIYETOKEA KATIKA FAMILIYA YA WANAMUZIKI.



LOVY LONGOMBA ALIYETOKEA KATIKA FAMILIYA YA WANAMUZIKI.

 “Mwana wa Nyoka ni Nyoka…” usemi huu wa wahenga unajionesha wazi kwa baadhi ya familiya zilizo jaaliwa vipaji vikubwa.

Kuna familiya zilizojaaliwa kuwa za wacheza mpira wa miguu, nyavu, na michezo mingine.

Mifano halisi ni kwa wanadada wawili Wamarekani weusi, Serena na Vunus Williams, ambao ni mabingwa Kimataifa katika kucheza mpira wa Tennis. 

Hapa nchini familya ya Uvuruge ilikuwa na watoto waliokuwa na vipaji vya kutunga  nyimbo na kupiga muziki.  Ndugu hawa Jumanne, Stamili, Huluka na Maneno, walijijengea sifa tele katika muziki hapa nchini.

Familiya ya akina Kihwelu nayo ilikuwa na viaji vya kucheza mpira wa miguu, ambapo walikuwepo akina Mtwa, Jamhuri ‘Julo’  na ndugu zao wengine.
Kwa upande wa ngumi, familiya ya Matumla imerithisha kucheza mchezo wa ndondi takribani familiya nzima.

Katika makala hii ambayo itamzungumzia Familiya ya Longomba, toka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Vicky Longomba ndye aliye kuwa baba wa familiya ya watoto wengi waliojaaliwa vipaji vingi vya muziki.

Huyo Mzee Vicky Longomba  alikuwa mmoja kati ya wanamuziki waliokuwa waanzilishi wa bendi ya T.P.OK. Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Franco Luanzo Makiadi.

Pia ikumbukwe kwamba  Vicky ndiye  aliyekuwa  mwanzilishi wa bendi ya Lovy du Zaire, iliyotamba kwa muziki nchini Kongo mwaka 1971.

Kwa kuwa familiya hiyo ina wanamuziki wengi leo katika makala hii itamzungumzia mmoja wa watoto wake Lovy Longomba.

Wasifu wa mwanamuziki huyo unaelezea kwamba alianza muziki katika bendi ya Orchestra Macchi mwaka 1976, akiwa na mwimbaji mwenzake Dindo Yogo.

Aidha walikishirikiana na mpiga gita Nseka Huit, waliondoka katika bendi ya Macchi na wakaunda bendi yao ya  Etumba na Ngwaka wakiwa na waimbaji wengine akina Lofanga, Gaby Yau-Yau na Mukolo, aliyekuwa akiimba sauti ya kwanza.

Wanamuziki wengine waliokuwepo katika bendi hiyo ni pamoja na Huit Kilos, ambaye baadaye alikwenda kuwa nyota katika bendi ya Afrisa International ya Tabu Ley Rochereau.

Mwanamziki Ricardo aliondoka na kwenda katika bendi ya Lemvo in Makina Loca, iliyo na makao yake huko  Los Angeles, Marekani.

Inaelezwa kwamba Lovy Longomba alikuwa mtunzi na mwimbaji mahiri. Alikuwa kaka wa wanamuziki machachari Awilo Longomba.

Awilo kabla ya kuanza kutunga na kuimba, alikuwa mcharazaji hodari wa drums katika bendi mbalimbali nchini humo. 

Lovy naye pia alikuwa baba wa familiya yenye watoto wanamuziki akiwemo binti yake aliyerithi uimbaji, Elly Longomba na mapacha Christian na Lovy ambao wote ni nyota katika muziki  wa Hip-hop, wakimiliki Kampuni ya ‘Longambas’ huko Nairobi, nchini Kenya.

Baadaye  Agosti 1978, Lovy aliicha bendi ya Orchestra Macchi, na kuamua kuondoka  Kinshasa. Alitiga katika jiji la Nairobi nchini Kenya ambako alijiunga katika bendi ya  Les Kinois.
Kwa kuwa ‘Kiu’ chake hakikuwa kimekidhiwa, Lovy alidumu kwa miezi mitatu pekee,
akatimkia katika bendi ya Boma Liwanza.

“Maisha ni kutafuta” mbio za kutafuta maisha zikaendelea. Baada ya miezi sita Lovy alitimka na kuiacha Boma Liwanza, akajiunga na bendi ya Super Mazembe iliyokuwa ikiongozwa na  Mutonkole Longwa Didos.
Akiwa katika bendi hiyo alionesha uhodari wa kutumia sauti yake ilivyokuwa nyembemba na nyororo, ambayo ndiyo iliyopelekea kwa yeye kupachikwa jina bandia la ‘Ya Mama’. Sababu kubwa ni kwamba alikuwa na uwezo wa kuimba sauti ya juu ambayo alipashwa aimbe mwanamke.

Katika bendi hiyo alikutana na  wanamuziki wenzake mahiri akina Joseph Okello Songa, Kasongo wa Kanema, Musa Olokwiso Mandala na Fataki Lokassa ‘Masumbuko ya duniya’ aliyekuwa ametokea katika bendi ya Les Noirs.

Baadhi ya nyimbo alizoachia katika bendi Super Mazembe ni pamoja na ‘Lovy’, ‘Yo mabe’, ‘Ndeko’, ‘Nanga’, ‘Mokano’ na ‘Elena’.
Sauti yake nyororo mara nyingi husikika katika baadhi ya nyimbo za bendi hiyo, akibwagiza akitamka “Vuta sigara SM, maana yake Super Mazembe…”

Hata hivyo umahiri wa kutunga na kuimba katika bendi hiyo, ilisababisha kuhitajika takribani na kila bendi.
Kwa mara nyingine tena Lovy aliondoka Super Mazembe mwaka 1981 akaenda kuimba katika bendi ya Shika Shika, iliyokuwa ikiongoza na Jimmy Monimambo, kwa miaka miwili.

Ndoto zake za kumiliki bendi yake zilitimia baada ya yeye na wanamuziki wenzake alipounda bendi yake Super Lovy ikiwa na Nembo ya AIT.

Lakini kwa kile alichokieleza ni kuepuka mkanganyiko na mvutano aliamua kutumia jina Bana Likasi  wakati aliporekodi  katika  Kampuni ya Audio Productions Ltd.


Akiwa na bendi hiyo, Lovy alipachikwa jina bandia la ‘Ya Mama’  kwa kile kilichoelezwa  kwamba alikuwa anauwezo mkubwa wa kuimba sauti  nyembamba ambayo ingelistahili kuimbwa na mwanamke.
Mnamo mwaka 1988 Lovy aliingia Tanzania katika jiji la Dar es Salaam na akapigia katika bendi Orchestra Afriso Ngoma.
Maisha ya nguli huyo yalikatishwa ghafla katika ajali iliyopelekea kufariki dunia nchini Tanzania mwaka 1996.
Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi, amina.

Mwisho.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba:
0784331200, 0767331200 na 0713331200.



No comments: