Sunday, November 1, 2015

NENE TCHAKOU MUUNGURUMISHA WA SOLO



NENE TCHAKOU MUUNGURUMISHA WA SOLO

Nene Tchakou ni jina ambalo halijazoweleka sana kwa wapenzi wengi wa muziki wa dansi. Ni mkung’utaji wa gitaa la solo aliyepitia katika bendi nyingi huko jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jina lake halisi ni Nene Mbedi, kwa sasa ni mtu mzima wa umri wa miaka 57 hivi sasa. 

Alizaliwa Februari 1957, katika eneo lililojulikana kama Banana huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Vipaji vingi vya wanamuziki huibukia wakati wakiwa  Kanisani  wakiimba au kupiga ala ya muziki na wengine hutokea kwenye Madrasa wakiimba Kaswida. Lakini kwa Nene Tchakou kwake ilikuwa tofauti kabisa.

Mbendi Tchakou  alianza kujihusisha na maswala ya muziki akicharaza gita kwenye kundi lililokuwa linaundwa na watoto wa Askari jijini Kinshasa.

Nuru njema ya mafanikio katika muziki ilianza kung’aa mwaka 1973 akiwa na bendi ya Bella Negrita. Mafanikio hayo yalipelekea kuanza safari ndefu ya kuzunguka kwenye bendi kadha wa kadha.

Weledi wake katika muziki alifanywa mithiri ya kito cha thamani kwa kuwa kila alikotuwa, alikubalika vilivyo.

Safari yake ya mwaka ya 1981, ilimfikisha katika kundi lililokuwa maarufu la ‘Langa Langa Stars mahali alikopewa jina la ‘Tchakou,’ likiwa na maana ya Parrot kwa lugha ya Kilingala. Kwa Kiswahili ni ndege ajulikanaye kama Kasuku.

Tchakou hakuwa mtu wa kukata tamaa wakati akitafuta mfanikio zaidi. Aliendeza safari  mwaka 1983 alipojiunga katika bendi ya Grand Zaiko, ikiwa chini ya uongozi wa Pepe Manwaku.

Alitoa mchango mkubwa mno katika bendi hiyo hususani katika e kibao cha ‘Mbongo’. Baadaye akaamua kupiga muziki akijitegemea na kufanikiwa kufyatua wimbo wa ‘Niger’ mwaka 1987.

Ni kawaida kwa wanamuziki toka nchi za Afrika ya Kati pindi wanapokaribia mafanikio, hukimbilia kwenda nje ya nchi yao. Nene naye alifanya kwenda katika jiji Paris nchini Ufaransa mwaka 1988.

Alipokuwa katika jiji hilo aliandika historia kwa kutoa mchango mkubwa kwa nguli wa muziki barani Afrika, Kofi Olomide na kutoa albamu ya ‘Papa Bonheur’.

Alipenda sana kushiriki na wanamuziki wakubwa hivyo baada ya muda alijiunga na kundi la Soukous Stars linaloongozwa na Lokassa ya Mbongo. 

Hapo walianza matayarisho ya albamu iliyokuja kutamba vilivyo ya ‘Lagos Knight’.

Utaratibu wa kushirikiana na wanamuziki wakubwa aliuendeleza ambapo kwa mara nyingine alishirikiana na mwanamuziki Lala Nomotoki (kutoka Togo) Shi Loving (Kutoka Nigeria), Papa Wemba (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, walitoa albamu ya ‘For idole.’

Ili atengeneze muziki mzuri Nene akashirikiana na mwimbaji mahiri Aurlus Mabele kutoka Congo Brazzavile, kwa pamoja wakaandaa albamu ya ‘Dossirr X’.

Nene Tchakou alitengeneza albamu yake ya kwanza akiwashirikisha Madame (Bongo), Patience Dabani (Kutoka Gabon), 3615 Code Niawu (Kutoka DRC.

Mwaka mmoja baadaye akiwa katika Jiji la California nchini Marekani, alirekodi albamu moja iliyotoka mwaka 2001.

Alimshirikisha mwimbaji wa Soukous Stars Shimmita mapema mwaka 2002, kuanzisha kundi la Afro Muzika.

Mwaka 2003 Nene Tchakou alijiunga na Lembo ya ‘Rowa Records’ kama msanii mkaazi. Huko ndiko alikotengeneza na kufyatua CD ya ‘Cesse Le Fou’ Pendin.

Tchakou vilevile anajishirikisha na kupiga muziki wa kiasili akishirikiana na wanamuziki wengine wa Kiafrika chini ya uongozi wa Injinia na Produza Rick Scott.

Nene Tchakou ameongeza idadi ya wanamuziki kwa Kiafrika wanaoishi nchini Marekani, na kwa idadi yao hadi sasa wamepatikana wanamuziki watatu.

Wanamuziki hao ni pamoja na Sam Mangwana, Diblo Dibala na  yeye Nene Tchakou.

Amesema bado wanahitaji wanamuziki wengi ili waendelee kuutangaza muziki wa Kiafrika Ulimwenguni kote.

Mwisho.





No comments: