Saturday, April 16, 2016

BELLA BELLA ILIYOTIKISA VIGOGO WA MUZIKI DRC



BELLA BELLA ILIYOTIKISA VIGOGO WA MUZIKI DRC.

Miaka ya nyuma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kulikuwa na ushindani mkubwa katika muziki. 

Walikuwapo wanamuziki wakubwa kama Franco Luambo Makaidi, Tabu Ley, Mpongo Love, Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’, na wengine wengi waliokuwa wakitamba katika muziki wa dansi.

Katika makala haya yanawaeelezea ndugu wawili Maxime Soki Vangu na Emile Dianzenza ambao kwa pamoja walaimua kuunda bendi yao ya Orchestra Bella Bella ililojulikana pia kwa majina ya Frères Soki & l’Orchestre Bella Bella iliyoanzishwa mwaka 1969.

Bendi hiyo ilileta chamgamoto kubwa kwa vigogo hao katika muziki, wakajikuta wakikwaa vikwazo vya kunyang’ayana wapenzi wa dansi toka kwa vijana hao.

Orchestra Bella Bella iliwajumuisha wanamuziki wengine akina Nyboma Mandido, Pepe Kalle, Shaba Kahamba na wengine wengi, waliofanya bendi hiyo kama jukwaa la kuanzia umaarufu.

Waliongozwa na ndugu hao Maxime Soki Vangu na Emile Dianzenza, wakiwa na wapiga magitaa Johnny Rodgers na Jean Bosco, Kahamba Uzalu maarufu kama Shaba Kahamba.

Wakati huo Emile Soki alikuwa na miaka 16 tu hivyo kuwa kipenzi cha vijana wenzie wakati huo.

Bendi hiyo ilirekodi vibao vilivyotikisa Afrika ya Mashariki na kati na kama vile “Baboti Bapekisi”, “Sylvie”, “Alexandrine”, “Mwasi ya moto”, “Luta”, “Lina”, Mandendeli”, “Mbuta”, “Bipale ya pembeni” na “Sofele”.

Kama wasemavyo waswahili kuwa “ngoma ikipigwa sana hupasuka” haya yalijiri baada ya ugomvi kutokea mwaka 1972, kati ya wanamuziki, uliopelekea bendi ipate mabadiliko makubwa.

Ile semi isemayo “hasira za mkizi…” zikajionesha kwa Emile, ailiyekuwa nguzo katika bendi ya Bella Bella, kuliacha kundi hilo na kwenda kuanzisha kundi la Bella Mambo.

Mtunzi na mwimbaji  Kabasele Yampanya ‘Pepe Kalle’ akajiunga na kundi hilo kwa miaka michache ili aweze kupata fedha za kununulia vyombo vyake mwenyewe.

Kujiunga kwa Pepe Kalle kukafanya Bella Bella iendelee kushikilia chati kwa kwa kufyatua vibao vya “Mbuta”, “Kamale”, “Kimbundi”, “Lipua Lipua” na “Sola”.
 
Kama wasemavyo waswahili kuwa “ Ngoma ya watoto haikeshi”, mwaka 1973 Emile Dianzenza aliicha bendi aliyoianzisha ya Bella Mambo na kurudi tena Orchesta Bella Bella kwa kaka yake Soki Vangu.

Alipotua kundini, wakatengeneza nembo ya kurekodia yenye majina ya “Allez-y frères Soki”

Kwa kupitia nembo hiyo waliachia vibao viwili vilivyoandikwa  “Dizzy Mandjeku”, ambavyo ndivyo vilivyowaingizia fedha nyingi kuliko kazi nyingine yoyote walizowahi kuzifanya kabla ya hapo. 

Baada ya vibao hivyo, vilifuatia vingine vyaMwana yoka toil”, “Menga”, “De base”, “Tikela ngai mobali”, “Pambindoni”, “Nganga”, “Houleux-houleux” na “Zamba”.
 
Ukwasi ulipowakolea walifikia kuanza kukodi vikundi vingine wakitaka kufanya maonesho kwa niaba yao.

Mwaka 1977, wakati wakiwa kwenye maonesho huko Ulaya, Emile akaanza kupatwa na maradhi yaliyosababisha kuchanganyikiwa.

Maradhi hayo hayakumpa nafasi tena ya kucheza muziki, akalazimika kuacha bendi.
Maxime alijitahidi kufufua upya bendi yao baada ya kupwaya kwa kiasi kikubwa, lakini wale wanamuziki alioanza nao wengi walikuwa wamekwisha ondoka.

Licha ya wanamuziki nguli akina Kanda Bongoman na Diblo Dibala kujiunga, hata nao walishindwa kuirudisha bendi katika uhai wa enzi zake.

Maji yalipozidi unga, Maxime Soki Vangu hatimaye aliiacha bendi yake ya Bella Bella na kuhamia nchini Ujerumani.

Maxime Soki Vangu aliyezaliwa Agosti 08, 1947, aliishi nchini humo hadi mauti yalipomfioka Mei 18, 1990 akiwa mjini Cologne.

Nduguye Emile Soki Dianzenza aliyezaliwa Kinshasa, Dec. 14, 1954, alifariki dunia Mei 04, 1990 akiwa na umri mdogo wa miaka 36. 

Orcherstra Bella Bella haipo tena kwenye taswira ya muziki, lakini nyimbo zake bado zinarindima.

Mungu azilaze roho zao pahala pema peponi, amina.

Mwisho.

No comments: