Saturday, April 16, 2016

BOZI BOZIANA ‘MZEE BENZI NA CHOC STARS



BOZI BOZIANA ‘MZEE BENZI NA CHOC STARS

“Nzawisaa, Nzawisaaa maama Nzawisaaa..Yeloo!!!..” 

Haya ni baadhi ya maneno alikuwa akiyatamka kama vibwagizo katika nyimbo za mwanamuziki maarufu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bozi Boziana.

Jina lake halizi anaitwa Mbenzu Ngamboni Boskill, ni mtu mzima aliyetimiza umri wa miaka 63, baada ya kuzaliwa   mwaka 1952 huko Jamhuri ya Kidemkokrasia ya Kongo.

Amepigia bendi nyingi kubwa na ndogo nchini mwake zikiwa ni pamoja na Bamboula de Papa Noel, Minzoto Sangela, Zaiko Langa Langa, Isifi Lokole, Yoka Lokole, Langa Langa Stars na Choc Stars

‘Mzee Benzi’ kama anavyojulikana na wengi baadae aiunda bendi yake Orchestra Anti-Choc, anayeiongoza hadi sasa.

Licha ya utunzi na uimbaji, pia ni mkung’utaji mzuri wa gitaa kulishambulia jukwaa akishirikiana na akina dada wawili Betty na Scolla Miell.

Mzee Benzi alianzia muziki wa Afro-Pop katika  bendi ya Air Marine lakini aliyaona mafanikio ya kazi zake ilipotimu mwaka 1974, alipojiunga na bendi ya Zaiko Langa Langa

Zaiko LangaLanga ilikuwa na waimbaji  mashuhuri wakati huo  wakiongozwa na mkongwe  Papa Wemba na mwezake Evoloko Jocker.

Lakini haikuzidi mwaka, Papa Wemba na Evoloko waliondoka  bendi hiyo baadae hata Bozi Boziana aliwafuata  kwenda kuanzisha bendi mpya ikaitwa Isifi Lokole

“ Fahari wawili hawakai zizi moja” usemi huo ulijidhirisha baada ya wanamuziki hao kushindwa kukubaliana katika maswala mbalimbali ya msingi yaliyopelekea wanamuziki wake akina Papa Wemba, Boziana, Mavuela Somo na wengine kuondoka bendi ya Isifi Lokole. Walienda kuunda bendi yao mpya iliyopewa jina la Yoka Lokole.

Bendi ya Yoka Lokole ilipata  mafanikio makubwa mwaka 1976, japokuwa ilipotimu mwinshoni mwa mwaka huo, Papa Wemba aliicha bendi hiyo na akaenda kuanzisha bendi ya Viva la Musica

Bozi Boziana naye mwaka 1977 naye aliicha bendi hiyo ya Yoka Lokole, licha ya bendi hiyo kuwa maarufu kwa kipindi kifupi.

Kwa miezi michache  Boziana alishirikiana na mwanamuziki Efonge Gina, ambaye naye alikuwa katika bendi ya Zaiko Langa Langa. 

Walirekodi nyimbo kadhaa kama vile Selemani iliyotungwa na Bozi Boziana na  Libanko Ya Ngai utunzi wake Gina.

 Kiamuangana mwaka 1981, aliibadilisha  bendi ya Soukous super group  na kuita  Langa Langa Stars ikiwa imesheheni vipaji vya wanamuziki kaiwemo Evoloko Jocker, Dindo Yogo na  wnengine wengi.  

Bozi Biziana aliakwa kujiunga vijana hao naye akaubali na kuicha  Zaiko Langa kwa mara ya pili.

Langa Langa Stars ilidumu kwa miaka michache iliyofuatia kabla na Boziana naye akaondoka kwenda kujiunga na bendi kubwa nchini humo  Choc Stars aliyokuwa chini Ben Nyamabo ambako alipiga hadi mwezi Novemba 1985.

Akiwa na bendi hiyo ya Choc Stars Boziana alirekodi baadhi ya nyimbo ambazo zilikuja kuwa maarufu za Sandu Kotti, Alena, Mbuta-Mutu na Retrouvailles a Paris.


Anti –Choc ilikuwa na wanamuziki wengi wenye vipaji lukuki wakiwemo akina Fifi Mofude, Djo Nolo, Koffi Alibaba, Wally Ngonda, Rigo Star, Ngouma Lokito, Deesse Mukangi, Marthe Lamugenia, Ngimbi Yespe na Maoussi Solange

Mpiga gita wa kwanza katika bendi hiyo alikuwa Matou Samuel ambaye  kwa sasa anaimba muziki wa Injili  na nafasi yake ilishikwa na Dodoly ambaye kabla ya kujiunga humo alitokea katika bendi ya mwanamuziki Lita Bembo ya Orchestre Stukas.

Dodoly alipachikwa jina bandia la ‘The sewing machine’ kwa umahiri wake wa kutumia vidole vyake kucharaza nyuzi  kwa kasi kubwa.

Tokea miaka ya 1980  Boziana aliendelea katika bendi yake ya Anti-Choc ikiwa ni pamoja na kurekodi nyimbo  akishirikiana na wanamuziki wengine mahiri.

Boziana aliwahi kushinda zawadi ya Kora All-African kwa album yake kuwa bora toka nchi za Afrika ya Kati.

Kwa wapenzi wa muziki hapa nchini watamkumbuka Bozi jinsi alivyoteka wapenzi katika maonesho kadhaa aliyoyafanya hapa nchini kwa ushirikiano walioonshea kati ya Bozi Boziana, Deesse Mukangi na Joly Detta walivyokuwa wakilishambulia jukwaa kwka staili ya ‘Nzawisa’ katika nyimbo za Tembe na Tembe, Palpitation na zingine nyingi zilifanya watu kuviacha viti vyao kwenda kuwatuza.

Bozi Boziana ana sauti nzuri, yakupendeza akimba huku akipokezana na timu yake ya wanadada wawili, Joly pamoja na Deesse.

Sifa nyingine za mwanamuziki huyu mzee Benzi ni kwamba muziki wake hauna mwingiliano kati ya sauti ,gitaa na synthesizer katika nyimbo zake zote.

Mfano katika wimbo wa ‘Ngoyartong020’ tune tatu za mwanzo Boziboziana amemshirkisha Jolly Detta na Deesse,  na sehemu ya pili ya wimbo huo aliongeza nguvu kwa kumuongeza waimbaji na wanenguaji  Scola Miel maarufu kwa jina ‘Nzawissa’ na Betty. 

Bozi alifyatua vibao vingi vilivyompa sifa nyingi ukiwemo wa La reine de Sabah, Lelo Makambo Lobi Makambo Evelyne na Fleur de Lys ambazo alimshirikisha mwimbaji wa kike Joly Delta.

Boziana aliachia wimbo mwingine akimshirikisha Deesse na Ba Bokilo.

Bozi Boziana na bendi yake bado anaendeleza muziki akiwa na bendi yake na watanzania watakumbuka kwa mara ya mwisho alikuja hapa nchini kwa mwaliko wa African Stars Entertainment Tanzania (ASET) iliyo chini ya uongozi wa Mkurugenzi Asha Baraka.

Mwisho.



No comments: