Sunday, March 10, 2013

KUANZISHWA KWA BENDI YA WESTERN JAZZ.


MTAMBUE MWANZILISHI WA  WESTERN JAZZ

               MZEE  IDD NHENDE 


Febr. 2013.

BENDI YA WESTEN JAZZ ilikuwa kongwe ambayo ilianzishwa mwaka 1959, kabla ya nchi yetu haijapata Uhuru.
Umaarufu wa bendi hiyo ulipanda ‘chati’ zaidi  baada ya wimbo wake wa Vigelegele kuibwa na bendi kongwe toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya Soukos Stars.
Jina la Idd Nhende  ni geni masikioni wa wapenzi wa muziki wa dansi hasa kwa kizazi kilichoiona dunia baada ya miaka ya 1970.
Western jazz ikajipatia umaarufu mkubwa hapa nchini na nje ya mipaka yetu hadi ilipotoweka katika medani ya muziki mwishoni mwa miaka ya 1970.

Pamoja na umaarufu wote huo, historia ya bendi hiyo ya Western Jazz haiwezi kukamilika  iwapo utaliweka pembeni jina la  Mzee Idd Nhende ambaye ndiye aliyepata wazo la kuazisha bendi ya hiyo mwaka 1959.

Wasifu wa Mzee Idd Nhende anaeleza kwamba alianza muziki akiwa bado mdogo katika bendi ya shule ya msingi huko Nzega. Mwaka 1944 alichaguliwa kujiunga  katika shule ya Sekondari ya wavulana ya Tabora,  huko akakuta kikundi cha blass band, akajiunga nacho akipiga ala iliyojulikana kwa jina la Cornet.

Baada ya kumaliza masomo ya Sekondari, alikwenda Dar es Salaam na akajiunga na Chuo cha Afya, Sewa Haji Medical Training Center.
Baada ya kumaliza mafunzo akaajiriwa katika Bohari ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili.
Upenzi wake wa muziki ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na bendi ya Rufiji Jazz kama mpiga tarumbeta.
Bendi hiyo kwa wakati huo ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre iliyokuwa eneo linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia walikuwa wakipiga muziki katika ukumbi wa Arnatougro.
Kutokana na miji ndio kwanza ilikuwa ikianza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au kuwaunganisha, watu wa sehemu mbalimbali.
Wakoloni waliokuwa wanatawala nchi yetu ya  Tanganyika wakati huo, waliigawa katika majimbo mbalimbali. Majimbo hayo yalikuwa ya Northern Province, Southern Highlands Province na Western Province


Wanamuziki wa wakati huo walianzisha bendi wakizipa majina ya maeneo yale  wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika. Kwa  vile Nhende alitoka Nzega huko Tabora ulikuwa katika jimbo la Magharibi yaani Western Province, akaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi ndipo alipoanzisha bendi ya Western Jazz mwaka 1959.

Mzee Idd aliweza kupata fedha baada ya kuuza ng’ombe kadhaa wa mama yake na kufanikiwa kununua vyombo aina ya Grampian toka duka la vyombo vya muziki lililojulikama kama Souza Junior lililokuwepo mtaa wa Mkwepu, jijini Dar es Salaam.

Wakati huo katika bendi za aina yake, ni Dar es Salaam Jazz  pekee ambayo ilikuwa na magita ya umeme. Kufuatia hali hiyo,  Mzee Nhende akawa na kazi ya kuwatafuta wapigaji ambapo alimfuata mpiga gita la umeme wa kwanza Haus Dibonde ‘msukuma’, aliyekuwa anapigia bendi ya Dar es Salaam Jazz  iliyokuwa chini ya Mzee Muba.
Baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka bendi ya Ulanga Jazz. Wakati huo chombo cha Banjo kilikuwa muhimu, hivyo akamtafuta mpiga Banjo toka bendi ya Cuban  Marimba  ambayo wakati huo ilikuwa na tawi jijini Dar es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu.

Mwaka mmoja baadae alipata uhamisho wa kwenda mji wa Morogoro, akalazimika kuongeza wasanii wengine  ili kuimarisha bendi wakati yeye akiwa hayupo.
Akampata mwimbaji mahiri wakati huo David Makwaya,  Ally Rashid (huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo) na  mpiga Saxophone toka Zanzibar.
Kwa bahati mbaya yule mpiga gita Haus akapatwa na kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani mkubwa wa bendi uliokuwepo.
Hivyo basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz. Wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi huko Mwanza, ikiitwa Kimbo Twist Band na wakahamia Tabora Jazz. Waliochukuliwa kutoka Tabora Jazz kwenda Western Jazz walikuwa akina Rashid Hanzuruni, Kassim ponda na Omary Kayanda.

Baada ya kazi nzuri sana, Rashid Hanzuruni ambaye alikuwa mkung’utaji wa gita la solo, nae akarukwa na akili katika mazingira yaleyale ya yule mpiga solo wa kwanza Haus Dibonde.  Bendi ikalazimika kumrudisha Hanzuruni Tabora ambako alikaa mpaka mauti yake yalipomfika.
Baadaye Wema Abdallah akachukua nafasi ya Hanzuruni ya  kupiga solo.

Nidhamu ilikuwa ni moja ya kigezo cha kuwa mwanamuziki katika bendi ya Western wakati huo. Haikujali umaarufu wa mtu kwani  mwanamuziki yeyote alikuwa na nafasi kubwa ya kutimliwa kwa utovu wa nidhamu. Hivyo tatizo la utovu wa nidhamu lilifanya Wema  Abdallah kuondolewa katika bendi hiyo ya Western Jazz.

Bendi ikiapata ‘kifaa’ kingine baada ya kumnyakua  mpigaji mzuri wa gita la solo, Shamba Abdallah kuziba pengo la Wema.
Shamba alionesha umahiri mkubwa kwa kushiriki katika kupiga solo kwenye nyimbo za Rosa na zingine nyingi.
Ukumbi wa nyumbani wa bendi ya Western Jazz ulikuwa ukiitwa Alexander Hall, ambalo baadaye ukaja kuitwa Ukumbi wa DDC Kariakoo.
Ushindani wa bendi na bendi uliendelea miaka hiyo, hivyo  iliilazimu bendi ya Western kununua drums baada ya wenzao wa bendi ya Kilwa Jazz kuzipitisha drums zao walizonunua kwa minajiri ya kuwaringishia.

Walinunua toka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers. Western walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliyousaini kwa  Lebo ya Phillips ya Kenya. Hatimae Western jazz akipiga katika mtindo wao wa Saboso,  walitoweka katika anga za muziki  mwishoni mwa miaka ya 1970.
Wetern kabla ya hapo ilitoka na vibao vingi vilivyopendwa na mashabiki wake hapa nchini. Baadhi ya nyimbo zao hizo zilikuwa za Rosa, Jela ya Mapenzi, Helena no 1& 2  na Vigelegele.

Kwa ruhusa yako msomaji wa makala haya naomba nikudonyolee kipande cha wimbo wa Vigelegele. Unanza hivi  “Vigelegele ndiyo furaha jamaa hehehe!!!  utamu wa ngoma ni kushangiliwa  jamaa hehehe!!! chereko chereko na mayowe mengi, hehehe!!!  mkofi mengi na vibwebwe,  ndiyo furaha, hayo,  hutokea ? pamoja!!  Western, mayowe!!  kwa wingi,,   njoo uonee,  furaha furaha…”
Wimbo huo wa Vigelegele uliwatoa ‘udenda’ wakongwe  wa muziki toka   Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya Soukous Stars, na kujiamlia kuukwiba pamoja na ule wa Dada Asha wa Tabora jazz. Kwa utaalamu mkubwa walionao, Soukous  wakazichakachua nyimbo hizo pamoja na nyingine na kuziweka katika album moja iitwayo Nairobi by Night.


Mwisho.

No comments: