Sunday, March 10, 2013

TABU LEY ROCHEREAU ATIMIZA MIAKA 72.


TABU LEY ROCHEREAU ATIMIZA MIAKA 72.

Novemba 20, 2012

TABU LEY ROCHEREAU ni mwanamuziki mkongwe katika tasnia ya muziki ambaye  mwezi huu wa Novemba amesherehekea miaka 72 ya kuzaliwa kwake.

Jina lake halisi ni Pascal Sinyamwe Tabu. Ni kiongozi wa  bendi ya Orchestra Afrisa International aloyoiunda mwaka 1970 na ni mmoja kati ya waafrika  maarufu kwa utunzi, uimbaji  na kuandika nyimbo amabye amejijengea umashuhuri Afrika.

Tabu Ley Rochereau ni mwanamuziki mwenye historia ndefu katika tasnia hiyo aliyezaliwa Novemba 13, 1940 huko Bandundu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC)

Kwa kushirikiana na mpiga gitaa Dr. Nico Kasanda waliasisi muziki wa Soukous ambao uliwafurahisha waafrika kwa muda wa miongo minne, wakiutangaza muziki huo kimataifa kwa kuunganisha muziki wa asili ya Kongo na Cuba, Caribbean na Rumba ya Latin Amerika.

Mwaka 1954 akiwa na umri wa miaka 14, Tabu Ley aliandika wimbo wake wa kwanza ulioitwa Bessama Muchacha aliourekodi na Bendi ya African Jazz ya Joseph Kabasele (Grand Kale) na baada ya kumaliza elimu ya juu alijiunga na bendi hiyo kama mwanamuziki kamili.

Tabu Ley aliimba wimbo wa kupigania uhuru wa watu weusi ulioitwa ‘cha cha’ ambao ulitungwa na Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ kipindi Kongo ilipopata uhuru mwaka 1960, wimbo ambao ulipelekea yeye kupata umaarufu mkubwa.

Alibakia na bendi ya African Jazz mpaka mwaka 1963 wakati yeye na Dr. Nico Kasanda walipounda kundi lao lililoitwa African Fiesta. 

Miaka miwili baadaye Tabu Ley na Dr. Nico walitengana  na Tabu Ley aliunda kundi lake lililoitwa African Fiesta Nationale pia bendi hiyo lilifahamika kama African Fiesta Flash. Kundi hilo lilikuwa na mafanikio kwa kuongoza mauzo katika historia ya Afrika.

Mwaka 1970 Alirekodi wimbo uliokuwa umeshika chati za juu za  kiafrika uliojulikana kama Afrika Mokili Mobimba na uliuza zaidi ya nakala milioni moja. Mzee huyo alifyatua nyimbo zingine kali za Ibragimu, Sukaina, Ponce Pilate, Cadance Mudinda na Boya Ye. Zingine zilikuwa Mbanda ya Ngai, Maze,Nzale, Sima Mambo Revens Itou, Nalingi yo Linga,  Nadina na nyingine nyingi.
Papa Wemba na Sam Mangwana walikuwa ni miongoni mwa wasanii maarufu wa muziki wa kiafrika ambao walikuwa sehemu ya kundi hilo.
Sambamba na kundi la Franco Luambo Lwanzo Makiadi lililoitwa T.P.OK. Jazz, kundi la Afrisa lilikuwa moja ya kundi  kubwa la kifrika. Walirekodi nyimbo kama vile Sorozo, Kaful Mayay, Aon Aon na Mose Konzo.

Katikati ya miaka ya 1980 Tabu ley alivumbua vipaji vya waimbaji na wachezaji, Mbilia bel aliyesaidia kuipa bendi yake umaarufu zaidi. Mbilia Bel alikuwa  muimbaji wa kwanza wa kike wa muziki wa Soukous na kukaribishwa kwa shangwe Africa nzima. Baadaye Tabu ley Na M’bilia Bel walioana harusi yao ilifungwa ndani ya ndege wakiwa hewani na baadaye wakafanikiwa kupata mtoto mmoja aitwaye Melodie.

Mnamo mwaka 1988  Ley alimtambulisha  mwimbaji  mwingine wa kike Faya Tess. Lakini baada ya ujio wa Tess katika bendi hiyo kulimfanya  M’bilia  kuondoka kwa kile kilichoelezwa kuwa wivu wa kimapenzi baina wana ndoa hao ulioingilliwa na Faya Tess.
Mara baada ya Mbilia Bell kujitoa katia kundi la Afrisa  Intrenationale pamoja na upinzani wa mkubwa na kundi la T.P.OK. Jazz, Bell aliendelea kupoteza umaarufu.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990 Tabu Ley aliishi Kusini mwa Califonia na alianza kurekebisha muziki wake uendane na mashabiki wa kimataifa kwa kuingiza lugha ya Kiingereza katika mashairi yake. Alifyatua Albamu za Muzina, Exil Ley, Africa Worldwide na Babeti Soukous.
Alipata mafanikio kwa kutoa albamu kama vile Muzina, Exile Ley, Africa worldwide na Babeti soukous.


Mwaka 1996 Tabu ley alishiriki katika albamu ya Gombo Salsa iliyotengenezwa na Salsa Music Project Africando. Wimbo uliojulikana kwa jina la ‘Paquita’ kutoka katika albamu hiyo ikiwa ni toleo jipya alioimba mwishoni mwa miaka ya 1960 katika bendi ya African Fiesta ulishika chati katika medani ya muziki.
Salsa akiwa na bendi ya Africando.



Mwishoni mwa miaka ya 1990 Rais Mabutu Sese Seko Kuku Ng’endu Wazabanga alipoondolewa madarakani, Tabu ley alirudi Kinshasa na alipewa nafasi ya uwaziri katika Baraza la mawaziri katika Serikali mpya ya Rais Laurent Kabila.
Kufuatia kifo  cha Laurent Kabila Tabu Ley aliendelea na Wadhifa huo chini ya Rais Joseph Kabila.

 Tabu Ley hali yake ki-afya si nzuri akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi.

Mwisho.



No comments: