Tuesday, May 12, 2015

GWIJI LA TAARAB SITI BINTI SAADI



GWIJI LA TAARABU SITI BINTI SAADI
 
Ukitaka kuzungumzia historia ya muziki wa taarabu, jina la Siti binti Saadi kamwe haliwezi kukosa kutajwa.
Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji.Alipokuwa akiimba sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali maili nyingi.
Mama huyo ilifikia wakati ambapo sherehe ilishindwa kufana kama Siti binti Saadi hakuwepo Jukwaani kutumbuiza.
Alizaliwa mwaka 1880 katika kijiji cha Fumba huko visiwani Zanzibar.
Mara alipozaliwa alipewa jina la 'Mtumwa'. Hii ni kwa kuwa alizaliwa katika kipindi cha Utumwa wa Kiarabu waliomuwa wakatwala visiwa hivyo.
Jina la Siti alipewa na Kabaila mmoja wa Kiarabu wakati huo.
Baba yake bwana Saad alikuwa ni wa kabila la Kinyamwezi kutoka Tabora na mama yake alikuwa ni Mzigua toka Tanga.
Wazazi wote hao walizaliwa Zanzibari. Yaelezwa kwamba hali ya maisha ya familia yao ilikuwa ni duni sana.
Walijishughulisha zaidi katika kilimo na ufinyanzi, kazi ambazo Siti alijifunza na kuzimudu vizuri pia.
Kama waswahili wasemavyo “kuzaliwa masikini si kufa masikini” Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji. Kipaji hicho kilimsaidia sana tangu siku za awali za maisha yake kwani alitumia uimbaji wake kuuza vyungu vya mama yake alivyokuwa akimsaidia kuvitembeza.
Siti alipoimba sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali maili nyingi na hii ndio ilikuwa ishara ya watu kujua kwamba vyungu vya kina Mtumwa vinapita leo.
Alifananishwa kuwa na mapafu yenye nguvu kama ya simba kutokana na alivyoweza kupaza sauti yake mbali na bila kuachia pumzi.
Kutokana na wakati huo elimu kwa watoto wa kike kutotiliwa mkazo, Siti hakuwahi kwenda shule wala kuhudhuria mafunzo ya Koraani.
Mnamo mwaka 1911, aliona ni bora ahamie mjini  Unguja, ili kubooresha maisha yake zaidi. Ujio wake wa mjini humo ulikuwa wa neema kwani alikutana na bwana mmoja wa kundi la muziki wa Taarabu la ‘Nadi Ikhwani Safaa’ aliyeitwa Muhsin Ali.
Katika kipindi hicho kundi hilo ndilo lilikuwa pekee la muziki wa taarabu, lililoanzishwa na Sultani aliyekuwa akipenda starehe na anasa, bwana Seyyid Barghash Said.
‘Nadi Ikhwani Safaa’ lilikuwa ni la wanaume peke yake, wanawake hawakuruhusiwa kujiunga na vikundi vya muziki kwa vile ilikuwa ikichukuliwa kama ni uhuni.
Bwana Muhsin alikiona kipaji cha pekee cha Siti na hivyo akajitolea kumfundisha kuimba kwa kufuata vyombo vya muziki na lugha ya kiarabu.
Baada ya hapo alikwenda kumtambulisha kwa wanamuziki wenzie wa ‘Nadi Ikhwani Safaa’ ambao bila kusita wakaanza kufanya naye maonesho mbalimbali katika jamii.
Walipata mialiko mingi hasa kutoka kwa Sultani na matajiri wengine wa Kiarabu, pia katika harusi na sherehe zingine mbalimbali.
Siti alikuwa ni ‘moto’ wa kuotea mbali, jina lake lilivuma kwa haraka sana hadi nje ya mipaka ya nchi na bara la Afrika. Punde Siti alianza kufananishwa na 'Umm Kulthum', mwimbaji mahiri wa kike aliyetamba wakati huo kutoka Misri.
Kama nilivyosema moto wa Siti ulikuwa si wa kuusogelea karibu, mwaka 1928  Kampuni ya kurekodi muziki ya Columbia and His Master's voice yenye makazi yake huko Mumbai nchini India, ilisikia umaarufu wa Siti binti Saadi. Hivyo ikamwalika yeye pamoja na kundi lake kwenda kurekodi kwa lugha ya Kiswahili ili kujaribu kama muziki wake utauzika.
Kampuni hiyo haikuweza kuamini jinsi muziki ule ulivyouzika kwa kasi kubwa kwani wastani wa santuri 900 ziliweza kuuzika katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo. Hadi kufikia 1931 santuri 72,000 zilikuwa zimeuzwa.
Kutokana na kusambaa kwa santuri hizo, umaarufu wa Siti ulizidi kuongezeka mara dufu watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia walikuwa wakija Zanzibar kumuona.
Mambo yalizidi kuwa mazuri kwa Siti hadi ikafikia hatua kampuni ya kurekodi ya Columbia kuamua kujenga studio ya kurekodi muziki palepale Zanzibar maalumu kwa ajili ya Siti binti Saadi.
Hatua hiyo ya hadi kujengewa studio iliwaumiza wengi wenye wivu. Wakaanza kumtungia nyimbo za kumkejeli ili kumpunguzia kasi hasa walitumia kigezo kwamba hakuwa na uzuri wa sura.
Nyimbo nyingi ziliimbwa lakini huu ndio uliovuma sana:
    Siti binti Saadi kawa mtu lini,
    Kaja mjini na kaniki chini,
    Kama si sauti angekula nini?
Na yeye kwa kujua hila za wabaya wake, akaona isiwe taabu akajibu shambulio kwa namna hii:
   Si hoja uzuri,
   Na sura jamali,
   Kuwa mtukufu,
   Na jadi kebeli,
   Hasara ya mtu,
   Kukosa akili.
Kwa kujibu shambulio hilo kwa namna yake aliwafunga midomo wale wote waliokuwa wakifuatafuata.
Siti pia alikuwa ni mwanamke wa kwanza mwanaharakati katika kipindi chake, alitetea wanawake na wanyonge kwa ujumla. Katika kipindi chake watu waliokuwa matajiri walikuwa wakiwaonea masikini na walipofikishwa mbele ya haki waliweza kutoa hongo na kuachiwa huru, halafu wewe uliyeshitaki ndiye unayefungwa.
Utunzi wake wa wimbo wa ‘Kijiti’ ulimpatia sifa kubwa kwani ulikuwa ukielezea kisa cha kweli kilichomkuta mwanamke mmoja mgeni kutoka Bara. Mwanamke huyo alipofika alikutana na tajiri mmoja ambaye alijifanya amempenda. Hivyo akamchukua na kulala naye halafu baadaye akamuua.
Tajiri yule alishitakiwa kwa bahati nzuri walikuwepo mashahidi wawili walioshuhudia tukio lile. Lakini kwa vile ni tajiri huyo alitoa hongo, kesi ikawageukia wale mashahidi na wakafungwa.
Siti akatoa wimbo huu :
   Tazameni tazameni,
    Eti alofanya Kijiti,
    Kumchukua mgeni,
    Kumcheza foliti,
    Kenda naye maguguni,
    Kamrejesha maiti.
Siti aliendelea kumwambia katika nyimbo zake kwamba asijethubutu kwenda Dar er Salaam kwa maana watu wenye hasira wanamsubiri na wameapa kwa ajili yake.
Siti aliendelea na shughuli zake za muziki hadi uzeeni. Muda mfupi kabla ya kifo chake alikutana na mwandishi maarufu na mwanamashairi Shaaban Robert, ambaye alimhoji na kuweza kuandika wasifu wake katika kitabu alichokiita "Wasifu wa Siti binti Saadi" Wasifu huo unaonekana kuwa ndio bora zaidi uliowahi kuandikwa katika fasihi ya Tanzania. Kitabu hicho kinatumika kufundishia shule za sekondari za Tanzania.
Ilipotimu Julai 08, 1950 Siti binti Saadi alifariki dunia na kuacha pengo kubwa katika fani ya Taarabu.
Japo pengo hilo haliwezi kuzibika, lakini kuna watu wengi walioweza kuibuka na umaarufu wa kuimba taarabu kupitia kwake, mfano hai ni marehemu Bi. Kidude.
Hata baada ya kifo chake jina lake bado linatumika sana kama kielelezo cha ushujaa wake. Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA), kimetumia jina lake kulipa jina gazeti la chama chao "Sauti ya Siti". Hadi leo hii Siti hutumika kama kipimo cha kufundishia uimbaji wa Taarabu. Na anakumbukwa katika historia yake ya kuwa mwanamke wa kwanza Afrika mashariki kurekodi muziki katika santuri.
Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi amina.

Mwisho.


No comments: