Tuesday, May 12, 2015

UNAMKUBUKA BINGWA WA DRUMS ABUU SEMHANDO?






           
           

UNAMKUBUKA BINGWA WA DRUMS ABUU SEMHANDO?


Miaka, miezi, wiki na siku hazigandi. Unakaribia mwaka wa tano sasa tangu mwanamuziki mashuhuri hapa nchini, Abuu Semhando kufariki dunia.
Kila mwanadamu hujipangia mambo yake akitaraji kukamilisha mipango hiyo. Lakini juhudi zote hizo hupanguliwa kwa uwezo wake mungu, kwa kuyakatisha maisha yako hata kabla ya kutimiza ndoto alizojiwekea.
 Abuu Semhando alifariki dunia kwa ajali ya Pikipiki aliyokuwa aikiindesha mwenyewe  usiku wa Jumamosi ya Desemba 18, 2010 akitokea kazini.

Semhando katika maisha yake alichangia mafanikio ya African Star Entertainment Tanzania (ASET), kwa asilimia kubwa kutokana na kujitoa kwa kila hali.
Alidumu kwa kipindi kirefu katika bendi hiyo toka alipojiunga na vijana hao wa Twanga Pepeta mwaka 1998 akitokea bendi ya Diamond Sound wana Kibinda Nkoi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa ASET Asha Baraka alimuelezea Abuu kuwa aliitumikia Twanga kama mali yake binafsi.

Kifo cha Semhando kilimitia simanzi yeye binafsi pamoja na wapenzi wote wa Twanga Pepeta ndani na Nje ya Nchi.

Alitamka kuwa Semhando alikuwa ni chachu ya mafanikio ya albamu zote 10 ambazo wamezitoa kutokana na kushiriki katika kuandaa muziki na kusimamia nidhamu ya bendi.

Kifo cha Abuu Semhando katika familia yake kilimgusa sana binti yake Sharifa, ambaye siku ambayo alikuwa anatakiwa kufungishwa ndoa na baba yake ndiyo mauti yalipomkuta na kufanya sherehe hizo kugeuka msiba.

Wasifu wa nguli huyo unaeleza kuwa jina lake kamili lililkuwa Abuu Ally Semhando maarufu ‘Lokassa’ au ‘Baba Diana’

Alikuwa mcharazaji mahiri wa drum  wakati huohuo alikuwa ndiye Meneja wa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’.

Abuu Ally Semhando “Lokassa” alizaliwa mwaka 1953 Kijiji cha Kibanda Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.

Alianza shughuli za muziki mwanzoni mwa miaka 1970 akiwa katika bendi ya Tanga International na baadaye kwenda kuwa mmoja kati ya waasisi wa bendi za Tanza Muzika na Orchestra Tomatoma kabla ya kutua Safari Sound Orchestra (OSS)

Abuu Ally Semhando na Hamza Kalala ni miongoni mwa wanamuziki waanzilishi wa bendi ya Super Matimila na ndio waliomkaribisha Mosese Fanfan na marehemu Dk. Remmy Ongala.
Baadae Semhando alijiunga na bendi ya Vijana Jazz ‘Pamba Moto’, ambapo kwa uwezo wake wa kuongoza alikabidhiwa nafasi ya kuwa Katibu wa bendi.
Abuu alishiriki kupiga drums kwa kiwango kikubwa katika nyimbo nyingi ambazo ziliiletea mafaniko ya bendi hiyo.

Akiwa katika bendi hiyo, mwimbaji maarufu toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Kasaloo Kyanga, alimpachika jina bandia la Lokassa.

Licha ya kuwa mpiga drums, Sembando alikuwa ni mwanamuziki mwenye kipaji kikubwa cha uongozi wa bendi (Music Band Management) na kushiriki katika kuandaa muziki ili kuhakikisha bendi yoyote aliyopitia inapata mafanikio. Jambo hilo lilimjengea umaarufu katika kila bendi aliyopitia.

Historia inaonyesha kuwa kila bendi alizowahi kupitia akiwa kiongozi baada ya kuondoka, ziliyumba na zingine kutokomea kabisa katika medani ya muziki wa dansi.

Lakini si Matimila pekee yake hata alipokuwa na Vijana Jazz ‘Saga Rhumba’ ambako alikuwa Katibu chini ya uongozi wa Hemed Maneti, alikuwa mmoja wanamuziki walioshiriki katika kuiletea mafanikio kwa miaka yote hiyo kabla ya kujiondoa.
Yaelezwa kuwa Abuu pia alikuwa muasisi wa ‘Vijana Day’.

Katika bendi hiyo ya Vijana alishiriki kwa kiwango kikubwa kutengeneza nyimbo akiwa na waimbaji kina Hemed Maneti, Saidi Hamis, Fred Benjamin, Cosmas Chidumule na Kida Waziri.
Aidha wapiga vyombo wakati huo walikuwa akina Kurwa wa Milonge, Hamza Kalala, Hassan Dalali, Aggrey Ndumbalo na Disfa Semhando (mdogo wake), aliyekuwa akiliungurumisha gitaa la besi. Alikuwepo mpiga gita la solo Shabani Yohana “Wanted” na wengine wengi.

Akiwa na wanamuziki hao ambao ni baadhi tu ya kundi alilokuwa nalo, walishiriki kutengeneza nyimbo kali kama ‘Bujumbura’, ‘Mary Maria’, ‘Tambiko la Pambamoto’, ‘Mundinde’, ‘Ali Hassan Mwinyi apewe Kura za Ndiyo’, ‘Wifi Zangu Wananinyanyasa’, Stella, ‘Penzi Haligawanyiki’ na nyingine nyingi nzuri kupindukia.
Nyimbo hizo zilitikisa anga ya muziki chini ya uongozi shupavu wa Hemed Maneti aliyekuwa Kiongozi, Hamza Kalala alikuwa ni Kiongozi msaidizi na Abuu Semhando mwenyewe  aliyekuwa Katibu.
Katika kudhihirikisha uwezo aliokuwa nao alipojing’atua Vijana Jazz, ndipo jinamizi na anguko la bendi hiyo lilipoanza kuinyemelea. Tangu hapo bendi hiyo haijafanya vyema katika medani ya muziki nchini.
Baadhi ya wanamuziki aliofanya nao kazi walimzungumzia marehemu Semhando akiwemo  John Kitime ambaye alisema kuwa ataendelea kumkumbuka Abuu Semhando kwa ucheshi wake, na vilevile alimpokea na kumtafutia malazi jijini mwaka 1989, wakati anajiunga na Vijana Jazz akitokea Tuncut Almasi ya Iringa.

Kwa upande wake mkung’utaji wa gitaa la solo Aldof Mbinga ambaye naye alisema tasnia ya muziki wa dansi imepoteza Jemedari ambaye alikuwa hayumbi katika misimamo yake jambo ambalo liliiletea mafanikio Vijana Jazz akiwa Katibu na ASET.
Mbinga alifanya kazi na Semhando kwa kutengeneza albamu ya kwanza ya Twanga Pepeta ya ‘Kisa Mpemba’ na ‘Jirani’.


Wengine waliomzungumzia marehemu ni Waziri Ally ambaye ni mwanamuziki wa bendi The Kilimanjaro ‘Wana Njenje’ akimtaja Semhando kama nguzo iliyokatika ghafla wakati watu wakihitaji huduma na ukongwe wake katika muziki.
Ushuhuda mwingine ulitolewa Isihaka Kibene, ambaye alisema, Twanga Pepeta imepoteza mpiganaji na mtawala mahiri kutokana na kuwa kiungo katika kufanya majukumu ya kila siku ya bendi. “Huyu jamaa ni rafiki yangu sana ambaye niliwahi kufanya naye kazi kiwanda cha uchapaji cha Printpak miaka ya 1970, na hata alipoanza shughuli za muziki tuliendelea kuwa marafiki..." alisema Kibene.
Abuu Ally Semhando ameacha mke na watoto 10 na kaburi lake lipo kijiji cha Kibanda Wilaya ya Muheza alipozaliwa.

Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi, Amina.

 Mwisho.


No comments: