Tuesday, May 19, 2015

PAPA WENDO MTUNZI WA 'MOKOLO NAKOKUFA'



PAPA WENDO MTUNZI WA 'MOKOLO NAKOKUFA'


Yasemekena mwanamuziki Antoine Wendo Kolosoy ndiye mtunzi halali wa wimbo wa Mokolo Nakokufa aliopigwa na bendi ya African Fiesta National.

Katika makala haya itanamzungumzia mwanamuziki nguli Antonie Wendo Kolosoy, historia ya maisha yake  na muziki.

Wasifi Wendo unaeleza kuwa alizaliwa Aprili 25, 1925 katika  Wilaya ya Mai-Ndombe Magharibi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Pamoja na kuwa alibatizwa kwa jina la Antoine Kalosoyi, alipewa jina la Wendo kutokana na jina la mmoja wa Watawala wa Uingereza aliyeitwa Duke of Windsor.

Hilo Windsor lilianza kubadilika na kuwa Wendo Sor na hatimae likabakia Wendo peke yake.

Ni utaratibu wa Waafrika kuheshimu wakubwa ndivyo ilivyokuwa kwa Wendo ambaye kwa utu uzima wake alikuja kuitwa Papa Wendo.

Akiwa na umri wa miaka saba, baba yake alifariki dunia. Lakini kwa mapenzi ya mungu muda mfupi baadae mama yake ambaye nae alikuwa muimbaji akafariki pia.

Baada ya matukio hayo makubwa, Wendo akapelekwa kuishi katika kituo cha watoto yatima kilichokuwa kikiendeshwa na Society of the Missionaries of Africa. Alipofikisha umri wa miaka 11 akaanza kupiga.

Alipofikisha umri kati ya miaka 12 na 13, akafukuzwa katika kituo hicho kutokana na kutunga nyimbo ambazo hazikuwapendeza Wafadhili wake.

Wendo akaanza kupiga muziki wa kuburudisha wasafiri katika Pantoni zilizokuwa zikifanya kazi katika Mto Kongo. Mto Kongo ndio unaotenganisha nchi ya Kongo Brazzaville na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwenye mwaka 1941 alianza kupiga muziki katika jiji la Leopordville (Kinshasa) akiwa na bendi yake ya Victoria Bakolo.
Katika harakati za muziki  wakati huo alikutana na mmoja ya wale ndugu wawili wa Kigiriki walioanzisha Record Label ya kwanza huko DRC, Nicolas Jeronimidis.
Walikubaliana kutoa nyimbo zake chini ya label ya Ngoma.

Mwaka 1948 akiwa na mpiga gita Henri Bowane, wakafyatua kibao ambacho kiliweza kupata umaarufu hata nje ya Kongo. Kibao hicho  kiliitwa Marie-Louise.
Kibao hicho kilitokea kupendwa sana katika nchi za Afrika Magharibi.

Papa Wendo aliendelea kuimba nyimbo nyingi kwa lugha mbalimbali ikiwemo ya Kiswahili. 

Kuna kitendawili kikubwa kilijitokeza cha nani aliyetunga wimbo wa Mokolo Nakokufa.

Kuna waliosema ni wimbo uliotungwa na Wendo Kolosay maarufu kama Papa Wendo na aliuimba mwaka 1966  kwenye msiba wa Paul Mwanga kule Kongo Brazzaville.

Kwa ushuhuda ni kwamba aliyempigia gita katika wimbo huo alikuwa Honoré Liengo.

Kwa maelezo yalijiri kuhusu wimbo huo ilikuwa kwamba Rochereau Tabu Ley alimkaribisha Papa Wendo auimbe wimbo huo wa Mokolo Nakokufa katika bendi yake ya African Fiesta National.
Kwa kuwa Wendo alikuwa na matatizo ya fedha wakati huo, akakubali haraka.
Tabu Ley Rochereau akamuahidi Papa Wendo kumpa haki zake zote za utunzi.

Hatimae Rochereau akaurekodi wimbo huo kwa jina lake na arrangement yake. Hili ni jambo ambalo hujitokeza mara nyingi katika bendi za Afrika ambapo kiongozi huweka jina lake katika tungo zilizorekodiwa.

Wendo aliendelea kuweko katika kundi la African Fiesta National kwa miaka miwili mpaka pale lilipotokea tafrani wakiwa katika jiji la Brussels nchini Ubelgiji. Bendi hiyo ilikuwa huko kwa mwaliko wa Ubalozi wa DRC nchini humo, ambako bendi yao ikatapeliwa malipo ya safari hiyo.

Tabu Ley Rochereau akawaacha ‘Solemba’ wanamuziki wengine huko wasijue la kufanya.

Mmoja wa wanamuziki hao Papa Wendo ambae akaamua kuiacha bendi hiyo, akajiunga na mwanamuziki mwingine maarufu Dewayon.

Mpaka mwaka 1990 alipokuwa akiulizwa ni utunzi wake gani alioupenda kuliko wote, Papa Wendo daima alikuwa akisema Mokolo Nakokufa.

Kwa kipindi kirefu sana Wendo alipotea katika ulimwengu wa  muziki. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo

Laurent Kabila na baadae mwanae Joseph Kabila kushika madaraka nchini humo, walimsaidia  Papa Wendo kuanza kurekodi tena sanjari na kuanza kufanya maonesho.

Aliwahi kufanya tamasha la MASA Cultural Festival kabambe nchini Ivory Coast mwaka 1998,  akiwa na kundi lake alilokuwa bado akiliita Victoria Bakolo Miziki.

Onyesho lake la mwisho alilifanya mwaka 2004 na hatimae kufariki 2008.

Mwaka huohuo alifariki dunia Julai 28, 2008 wakati Tabu Ley alifariki Desemba 03, 2013.

Je, wewe msomaji wa makala haya unaona ni nani mtunzi wa wimbo wa Mokolo Nakokufa?

Mungu azilaze roho za Pawa Wendo Kalosoyi na Tabu Ley Rochereau pahala pema peponi, Amina.





No comments: